Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,746
- 25,638
HADITHI: DIMBWI LA HUBA
SEHEMU: 01
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500....
...
Walitembea wakiwa wameangalia chini lakini ghafla
kila mmoja alinyanyua macho kuangalia mbele na moja
kwa moja yalitua kwenye uso wa mwenzake. Wote
waliteremsha macho chini na kuendelea na safari yao
iliyokuwa ikiwakutanisha katika njia moja.
Baada ya hatua mbili, kila mmoja hakukubaliana na alichokiona, wote
wakanyanyua tena macho kupata uhakika wa kile walichokiona. Kila mmoja
aliponyanyua uso wake, walijikuta wakitazamana tena na kuwafanya
watabasamu bila kusema kitu. Kwa vile walikuwa wamekaribiana,
walipishana bila kusemeshana, kila mmoja akatazama chini.
Baada ya kupishana, kila mmoja bado macho yake yalikuwa na hamu ya
kuona zaidi uzuri wa mwenzake. Walitembea hatua zaidi ya sita, mmoja
akaamua kugeuka kumwangalia mwenzake kwa kumuibia, wakati mmoja
anageuka na mwingine naye aliona sehemu ile inafaa kugeuka kumuangalia
mwenzake. Ikawa kama mwanzo, wakakutanisha tena macho yao, safari hii
kila mmoja alisimama na kumtazama mwenzake kwa muda kisha kila mtu
alitikisa kichwa na kugeuka kuendelea na safari yake.
Msichana Zulfa roho ilimuuma kutosikia hata sauti ya kijana mzuri
aliyeugusa moyo wake kwa ghafla, hakuwahi kupenda katika maisha yake,
siku zote moyo wake haukuwahi kuguswa kama siku ile lakini hakupata hata
nafasi ya kusikia sauti yake zaidi ya tabasamu lililousambaratisha moyo wake
na kutamani kumuona tena hata kusikia sauti yake. Lakini kwa bahati mbaya
kwake ilikuwa siku ya kwanza kumuona na hakuwa na uhakika wa kumuona
tena kutokana na muda mwingi kuwa shuleni kwenye ulinzi mkali.
Kilichokuwa kikimuudhi ni tabia ya wanaume wengi kumsumbua
kimapenzi, kwa kuwa moyoni hakuwakubali, alijisikia karaha sana. Lakini
aliyempenda hata salamu yake hakuisikia zaidi ya tabasamu.
Sued naye moyoni mwake alijilaumu kushindwa kumsalimia binti mrembo
kama yule aliyekutana naye, tena mwenye tabasamu mwanana lenye kumtuliza
simba mwenye njaa. Aliamini haikuwa bahati yake, kama ingekuwa hivyo basi
angemsalimia hata kusikia sauti yake. Aliamua kuachana naye na kuendelea na
mambo yake.
***
Sued baada ya mizunguko yake, aliingia katika ‘Internet Cafe’ kuperuzi
mitandao mbalimbali. Baada ya kulipia, alikaa kwenye kompyuta aliyoelekezwa
Akafungua tovuti aliyokuwa anaitaka, akili na mawazo yake vikazama kwenye
mtandao. Siti ya pili aliingia msichana mmoja aliyekuja kuperuzi kwenye
mtandao.
Wakati akiperuzi, kuna kitu kilimtatiza, ikabidi aombe msaada siti ya pili
alipokuwa amekaa Sued aliyekuwa amezama kwenye tovuti.
“Samahani kaka naomba msaada wa...” yule msichana alishindwa kumalizia
sentensi yake baada ya kumuona mtu ambaye hakutegemea kumuona tena.
Wakati huo Sued alikuwa amenyanyua uso wake ili amsikilize yule msichana ana
shida gani, naye akajikuta akishtuka na kushika mdomo.
“Haa!”
“Basi,” yule msichana alisema kwa aibu huku akirudi kwenye kiti chake lakini
Sued hakukubali suala hilo lipite, akanyanyuka hadi kwenye kompyuta ya yule
msichana na kumsemesha:
“Unasemaje mrembo?”
“Aah! Basi.”
“Basi nini mrembo?”
“Basi tu,” Zulfa alijibu akiwa ametazama chini kwa aibu za kikekike.
“Sikiliza mrembo, nina imani leo ni siku yetu ya kwanza kuonana na ajabu
tumeonana zaidi ya mara moja. Mara ya kwanza hatukuzungumza lakini safari
hii nimeweza kuisikia sauti yako ambayo haina tofauti na umbile mantashau
ulilobarikiwa na mwenyezi Mungu. Basi tusiipoteze nafasi hii angalau tujuane
kwa majina ili siku nyingine tukikutana tusiwe na ugeni tena.”
“Naitwa Zulfa Kipepeo.”
“Kipepeo wa Kayenzo?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Kumbe mtoto wa mkubwa?”
“Lakini ana haki ya kupendwa na wanaume wazuri kama wewe.”
“Mi naitwa Sued.”
“Jina zuri sana,” Zulfa alisema huku akimwemwesa midomo.
“Halishindi lako,” Sued alijibu mapigo.
“Langu nimelizoea naliona la kawaida lakini lako jipya akilini na moyoni
mwangu. Hakika ni jina zuri, hongera kuwa na jina zuri kama ulivyo mwenyewe.”
“Asante, lakini sikushindi wewe.”
“Kwa mwanamke kuwa mzuri ni jambo la kawaida ila wanaume ni nadra
sana.”
“Asante.”
“Na hapa mjini umefuata nini?”
“Nasoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwira.”
“Na huku mjini?”
“Siku za Jumamosi huwa tunapewa ruhusa ya kuja mjini mara mojamoja.”
“Nafikiri itakuwa nafasi yetu ya kuonana kila ukija mjini, una simu?”
“Ninayo lakini tukiwa shuleni haturuhusiwi kutumia mpaka tutakaporudi
nyumbani.”
“Shuleni unatakiwa kurudi saa ngapi?”
“Ulikuwa unasemaje?”
“Tungetafuta sehemu tukakaa tuzungumze kidogo.”
“Japo tupo chini ya uangalizi mkali lakini mimi kukutana na wewe ni bahati
kama nyota ya jaha hivyo siwezi kuipoteza.”
Walikubaliana kuondoka pale na kwenda kwenye bustani iliyokuwa karibu
na Ziwa Victoria kupunga upepo. Kila mmoja alikuwa na furaha moyoni kwa
kukipata kile alichokiamini amekipoteza.
Wakawa wanapunga upepo huku Zulfa akiwa amemlalia Sued mapajani
utafikiri wapenzi wa muda mrefu kwa jinsi walivyokuwa.
“Sued yaani Mungu wa ajabu sana,” Zulfa alivunja ukimya.
“Kwa nini mpenzi?”
“Nilijua sitakuona tena, si unajua tukiingia shule hatutoki hasa mimi mvivu
sana kuja mjini.”
“Nina imani leo Mungu alitukutanisha kwa sababu zake.”
“Halafu baby, wiki ijayo nakwenda nyumbani likizo, nina imani utanimisi sana
kwa mwezi mzima, ila kwa vile uhusiano wetu umeanza rasmi baada ya mwezi
kwisha nikirudi kila Jumamosi tutakuwa pamoja.”
“Basi nakuomba ukapajue nyumbani ili ukija uje moja kwa moja.”
“Hakuna tatizo lakini nikitoka kwenu narudi shule moja kwa moja.”
“Mwisho kurudi shule saa ngapi?”
“Saa kumi na mbili jioni.”
“Basi nina imani tuna muda wa kuzungumza mpaka jioni.”
Walikubaliana na kwenda nyumbani kwa akina Sued Mabati, walipofika
walizungumza hadi saa kumi na mbili kisha Sued akamsindikiza mpenzi wake
huyo, mtoto wa tajiri mkubwa jijini. Kabla ya kuachana, Zulfa alimueleza Sued:
“Sued mpenzi, sijawahi kupenda, wewe ndiye mwanaume wangu wa kwanza
kukupenda hata kuutambua mwili wangu, ukinitenda sitakuwa na maisha,” Zulfa alisema kwa sauti ya kubembeleza lakini yenye msisitizo.
“Zulfa nakuahidi mbele ya mwanga huu wa jioni kuwa sitakutenda, macho
yangu yamekuwa kama kipofu aliyebahatika kufumbua macho mara moja na
kukuona wewe peke yako. Nakuahidi sitampenda mwanamke yeyote chini ya
jua zaidi yako.”
“Nashukuru mpenzi wangu baki salama Mungu akipenda tutaonana.”
“Nakutakia safari njema.”
Waliagana kila mmoja akiwa na donda la mapenzi kwa kuona mwezi mmoja ni
sawa na miaka mia moja.
Itaendelea kesho