Fukuza fukuza ya CCM katika mtazamo wa kihistoria

Massivve

JF-Expert Member
Jun 4, 2015
274
368
Anaandika Mwl Elias Mhegera.

Jana nilipata wakati mgumu kidogo pale nilipoombwa kwa njia za inbox Facebook, Whatsapp na wengine wakanipigia simu ili nitoe maoni yangu japo kwa kifupi kuhusu fukuza fukuza ndani ya CCM.

Pamoja na kuunga mkono jitihada za Rais John Pombe Magufuli kuweka nidhamu ndani ya chama chake bado ninaamini kwamba maridhiano na kupatikana kwa muafaka katika migogoro ni jambo lenye tija zaidi kulikoni fukuza fukuza.

Lakini pia ieleweke kwamba hii si fukuza fukuza ya kwanza na wala siyo kubwa kuliko zote, kwa mfano katika kikao chake mjini Tanga, Oktoba 15, 1968, NEC ya TANU ambayo ndiyo ilizaa CCM iliwafukuza uanachama wabunge WANANE nitakaowataja punde.

Hawa walifukuzwa katika kile kilichoitwa “kukiuka maadili ya chama, kwa mtazamo, kwa vitendo na kwa kuonyesha upinzani dhahiri kwa chama, siasa na sera zake” (Msekwa: Towards Party Supremacy, uk 48).

Waliofukuzwa uanachama na kupoteza ubunge walikuwa Fortunatus Masha (Buchosa), Modestus Kivatama Chogga, G. Kaneno (Karagwe)(jina lake la pili silipati aliyenalo atusaidie), Thomas Bakampenja (Ihangiro); Joseph Kasella – Bantu (Nzega Mashariki); Wilfrem Mwakitwange (Taifa) na Steven Kibuga (Mufindi).

Wengine walikuwa ni Oscar Kambona (Morogoro Mashariki na alikuwa Waziri pia) na Elly Anangisye (Rungwe Kaskazini na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa TANU wa zamani – TYL). Hawa walifukuzwa kwa “kutokuwa waamini wa TANU na itikadi yake ya Ujamaa”.

Anangisye alifukuzwa baada ya kuwa amewekwa chini ya uchunguzi kwa takribani miaka miwili ya misuko suko ya kisiasa.

Unaweza pia kuwasoma hapa: Dk. Masha: Nilikosa ajira sababu ya Nyerere
Kwa hiyo fukuza fukuza siyo jambo jipya ndani ya CCM ambayo ni mtoto wa TANU. Pamoja na hayo kumekuwapo na misuguano na misigano mikubwa na midogo katika uhai wote wa chama.

Misigano hiyo, majungu na maseng’enyo ni sehemu ya siasa na wakati mwingine huchochewa na udini, ukabila na ukanda na hata wakati mwingine mipishano katika madaraja ya elimu kati ya wanasiasa wasomi na wale wenye ‘elimu ndogo’.

Baada ya Mwl. Julius Nyerere kustaafu katika mkutano mmoja wa CCM kule Dodoma Marehemu Ditopile Mzuzuri akiwa ni Mbunge wa Ilala na Mjumbe wa NEC alipata kumtamkia Mwl Nyerere, “Mwl mimi siogopi kukumbia ukweli…wewe ulikuwa na chuki na uliwakandamiza sana Waislamu katika utawala wako”.

Kauli hiyo ya Ditopile ilitoka kinywani wakati Mwl Nyerere akiwa bado ni mwenyekiti wa CCM. Ikumbukwe mwalimu alistaafu urais lakini aiendelea kuwa mwenyekiti hadi mwaka 1990. Na Mwl. Nyerere akamjibu Ditopile, “mimi siwezi kujibizana na wahuni”.

Ditopile alipopewa ukuu wa mkoa wa Dar es Salaam akiipa mitaa kadhaa majina ya Waislam ambao aliamini Nyerere aliwakandamiza kwa mfano Bara bara ya Bibi Titi Mohamed, Barabara ya Rashid Kawawa na hata Mtaa wa Mzuzuri huko Ilala kama siyo Buguruni na mingine kadhaa.

Pamoja na hayo yote ni kwamba misigano iliendelea katika utawala wa Mzee Ali Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa na hata wa Jakaya Kikwete. Ukiniuliza maoni yangu katika marais wote ni nani alifanikiwa kukiweka pamoja zaidi chama chake nitakuambia ni JAKAYA MRISHO KIKWETE!

Rais Kikwete aliwahi kugombana na Prof. Mark Mwandosya akiwa kabu mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati na Kikwete akiwa naibu waziri. Mwandosya akamfahamisha Rais Mwinyi na akamhamishia Viwanda na Biashara hata hivyo Mwandosya hakuridhishwa na uongozi wa Mzee Cleopa Msuya na hivyo akaamua kurejea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufundisha.

Hata hivyo pamoja na tofauti hizo Kikwete ameendelea kumbakiza Mwandosya katika Baraza la Mawaziri katika muda wote wa utawala wake hata pale prof huyo alipougua kwa muda mrefu, mifano ipo mingi japo nimetumia michache.
Pamoja na ufisadi mkubwa uliokuwapo katika utawala wake Kikwete alifanikiwa sana kuwaweka wana CCM pamoja hata kama kulikuwa na malumbano yasiyoisha.

Kwa mfano kundi la watu wote waliofukuzwa au kuonywa sasa ni wale waliokuwa wanamkosoa chini chini Kikwete wakiwa ndani ya CCM kwa kumdhalilisha rafiki yake wa zamani Edward Lowassa.

Ninayasema hayo bado nikikumbuka vyema mvutano uliochangiwa kwa kiwango kikubwa kati ya misigano kati ya Spika Samuel Sitta (R.I.P) na waziri mkuu wake Edward Lowassa ambayo ililiyumbisha sana Bunge.

Kikwete alihujumiwa vilivyo wakati wa kampeni zake jijini Mwanza mwaka 2005 wakati akitafuta kuungwa mkono mkoani Mwanza na aliyeongoza hujuma alikuwa ni mkuu wa mkoa kwa wakati huo Bw. Daniel Ole Njoolay ambaye Kikwete alimhamishia mkoa wa Rukwa na baadaye akampa ubalozi nchini Nigeria.

Kikwete alifikia hata mahali pa kuwataja hadharani watu waliokuwa katika kambi ya Mzee Frederick Sumaye ambao bado aliwapatia uwaziri katika awamu yake huku akifahamu fika jinsi ‘walivyompiga kiatu’ ili kumbeba Sumaye, miongoni mwao akiwa ni mama Mary Nagu.

Fukuza fukuza ya sasa ni kiashiria cha mengi yanayoendelea ndani ya CCM na pia kwamba makundi au kambi za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 bado hazijavunjwa rasmi, swali kubwa ni je kwa nini safari hii hazijavunjwa wakati miaka yote zilikuwa zikivunjwa mara baada ya uchaguzi?

Najua fika kwamba fukuza fukuza ya sasa ililenga kufanya ‘timing’ kwa ule mpango mahususi wa baadhi ya makada wa CCM kupinga jinsi nchi inavyendeshwa chini ya JPM. Rejea kauli ya Spika wa Bunge Job Ndugai “tukiendesha nchi ki-ubabe ubabe tutaivuruga” kauli hiyo ilikuwa na maana pana zaidi kuliko hapo ilipoishia.

Ilimaanisha kwamba Bunge linajipanga mahali pake na kutaka kuondokana na mkono wenye nguvu wa rais ambaye pia ndiye mwenyekiti wa CCM. Kauli hiyo iliwafurahisha sana wabuge wa upinzani ambao wanaona kwamba nchi hii kwa sasa inaendeshwa kwa ‘mkono wa chuma’ au kwa lugha ya kimombo ‘tyranny’.

Vyovyote iwavyo ipo haja ya kujifunza kuwa ‘accommodative’ yaani kuyapokea mawazo hata ya wale wanaokupinga ili uweze kuwa kiongozi bora. Nimeyatoa mawazo yangu haya kwa moyo mweupe kabisa na kwa kuzingatia maombi yenu wadau wangu na iwapo yatachukuliwa vinginevyo basi hilo halikuwa kusudio langu.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
 
Magufuli ameivuruga nchi na anapoelekea ni kuvunja vigingi vyote ili atawale apendavyo!
 
Hao waliofukuzwa waendage tu wakaungane na boss wao anayewatuma kuvuruga chama chetu
 
Kufukuzwa chama sio tatizo ila tatizo ni chuki na visasi vvya kundelea ambvyo ndivo vitkavyotrejesha nyuma
 
Hoja yako inaonyesha tu jinsi ccm ilivyogawanyika wakati kuliko wakati mwingine wowote nasi tunasema kwa faida ya nchi hii tunahitaji kuondoa aina yeyote ya kuhodhi madaraka iwe kwa taasisi, chama au kundi lolote, kugawanyika ccm ni heri kwa taifa.
 
Back
Top Bottom