FISADI Chenge aiponza Takukuru

BASIASI

JF-Expert Member
Sep 20, 2010
9,735
5,005
Chenge aiponza Takukuru Send to a friend Thursday, 11 November 2010 21:03 0diggsdigg

chengeeee.jpg
SIKU moja baada ya Uingereza kupingana na taarifa ya Takukuru iliyotolewa kumsafisha Mbunge Mteule wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge dhidi ya kashfa ya rada, wasomi wameibuka na kusema taasisi hiyo nyeti na muhimu katika kulinda masilahi ya taifa ifutwe.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema hivi sasa taasisi hiyo haina maana, wala sababu ya kuendelea kuwepo kwa sababu imepoteza dira na mwelekeo.
Novemba 8, mwaka huu, Takukuru iliwasha upya moto wa kashfa ya ununuzi wa rada baada ya kutoa taarifa kuwa Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hakuhusika kwenye kashfa hiyo.

Takukuru ilitoa taarifa hiyo siku moja baada ya Chenge ambaye ni mbunge mteule wa Bariadi Magharibi, kuitisha mkutano wa waandishi na kutamba kuwa hahusiki na kashfa ya rada.

Taarifa ya Takukuru kumsafisha Chenge ilitolewa mara baada ya kutangaza kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuuponda uongozi wa Sitta kwa ulisababisha makundi na chuki ndani ya Bunge.

Hata hivyo, juzi serikali ya Uingereza kupitia ubalaozi wake hapa nchini, ilikanusha kufungwa sakata hilo ikisema kuwa hakuna kitu kama hicho kwa kuwa kesi hiyo bado hajafikishwa mahakamani

Mhadhiri Chuo Kikuu cha Tumaini cha Iringa Harod Tairo, alisema: “Sasa Takukuru imeonyesha wazi kuwa haiko makini, hivyo inapaswa kufutwa na kuundwa taasisi nyingine huru”.

Alipendekeza kuwa taasisi hiyo huru iundwe chini ya usimamizi wa bunge na kuwajibika moja kwa moja bungeni badala ya serikali ya kuu ambako inatumika kulinda maslahi ya vigogo.

"Sio kwamba hawakufahamu (Takukuru) kuwa kesi ya rada bado inaendelea, ili walifanya kusudi kumsafisha huyu (Chenge) ili aendelee kugombea uspika na bahati nzuri ameanguka," alisema Tairo.

Aliendelea kuichambua taasisi hiyo akisema: "Kitendo hicho sio tu kinaifanya taasisi hiyo ionekane imepoteza mwelekeo, bali pia Watanzania hawaiamini tena, hivyo inapaswa ifutwe".

Alisema Takukuru imeenda kinyume na matarajio ya Watanzania kwamba ingesaidia kuondoa uozo kwani inaonekana kuutunza na kulifedhehesha na kulitia taifa aibu.

Profesa Abdallah Safari wa Chuo Kikuu Cha Dar es salaam, alisema hatua ya Serikali ya Uingereza kupinga taarifa ya Takukuru, inaonyesha kuwa kuna madudu na Chenge anahusika kwenye sakata hilo la rada.

"Nawashangaa sana Takukuru. Uingereza wana vithibitisho vyote kuhusu sakata hili. Wenyewe (Takukuru) wanasemaje hana hahusiki. Kama si kulitia aibu taifa ni nini?" alihoji Profesa Safari n kuongeza:

"Tamko la Uingereza ni la kidiplomasia. Kwa kawaida huwa hawana tabia ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi, ukiona wameingilia, ujue suala hilo ni zito na wana ushahidi wa kutosha."

Profesa Safari amependekeza Takukuru ivunjwe na kuundwa taasisi nyingine huru itakayogusa matarajio ya Watanzania katika kuongoza vita dhidi ya rushwa.

Gasper Mpehongwa wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), alisema Takukuru imepoteza dira katika utendaji wake wa kazi, kwani inaonekana kuwa inafanya kazi kimaslahi.

"Hii ni mara ya pili kuwasafisha viongozi wanaotuhumiwa na kashfa nzito. Awali walitaka kumsafisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa na kashfa ya Richmond na sasa inataka kumsafisha Chenge," alisema Mpehongwa.

"Wanachofanya Takukuru, wakiona mtu mzito ambaye wanaamnini kuwa atakawasaidia, wanamtetea lakini wakiona mtu ni adui yao wanamkandamiza," alisema Mpehongwa.

Mpehongwa alieleza kuwa tabia hiyo ya Takukuru inalitia taifa aibu mbele ya jumuiya ya kimataifa, hivyo inapaswa kuvunjwa kwa maslahi ya nchi na Watanzania kwa ujumla.

Naye Dk Farles Ilomo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, alisema Takukuru inafanya kazi kisiasa zaidi kuliko maadili.

"Inakuwaje imsafishe Chenge katika kipindi ambacho anagombea uspika?" alihoji Dk Ilomo na kuongeza: "mwanzoni walikuwa wapi? Taasisi hiyo ivunjwe kwa maslahi ya taifa.


Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sengodo Mvungi amemtaka Dk Hosea ajiuzulu.

“Anachotakiwa kufanya Dk Hoseah ni kuwaomba radhi wananchi au kujiuzulu kwa sababu anaivunjia heshima ofisi yenye mamlaka makubwa katika serikali,” alidai Dk Mvungi.

Dk Mvungi alidai, kitendo cha Hosea kumsafisha Chenge kinaonyesha kuwa kuna urafiki mkubwa kati yao, kwa sababu Takukuru haikuwahi kufungua kesi yoyote inayomhusisha na tuhuma za rada.

“Hoseah hakuichunguza kwa kina kesi hiyo na kuona kuwa Chenge hana hatia, hivyo anachokifanya ni urafiki kati yake na mtuhumiwa kwa sababu bado hana uhakika na anachokisema,”alidai Mvungi.

Kauli ya Dk Mvungi iliungwa mkono na aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid ambaye ametaka Dk Hoseah ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uwongo.

Hamad ambaye ameongoza kambi ya upinzani bungeni katika bunge lililopita, jan alisema atakufa na Dk Hoseah bungeni mpaka ajiuzulu kama hataki kufanya hivyo kwa hiari yake.

"Unajua huyu Hoseah ameshazoea, yaani anamsafisha mtu wakati mtu huyo bado anaonekana kuwa na matatizo mahakamani, akisema hadharani kuwa hana tatizo. Hii ni hatari kubwa kwa nchi," alisisitiza Hamad.

Jana gazeti hili lilimtafuta Dk Hoseah ili azungumzie tuhuma hizo, alijibu kwa kifupi akisema: "Sina cha kuongea. Zungumza na Ofisa Uhusiano wangu."

Alipotafutwa Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani naye alijibukwa kifupi akisema: "Nilishaongea na waandishi wa habari jana (juzi), mkawaulize wenzenu. Siwezi kurudia kila siku jambo hilo hilo".

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kapwani, uchunguzi wake kuhusu kashfa ya rada pamoja na ule uliofanywa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, umeshindwa kumhusisha Chenge na kashfa hiyo.

“Tunapenda kuujulisha umma kuwa uchunguzi na ushahidi uliokusanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Shirika la Upelelezi - SFO la Uingereza kuhusu tuhuma za rushwa katika ununuzi wa rada umeshindwa kumhusisha, Andrew Chenge, katika tuhuma hizo,” ilisema taarifa hiyo fupi yenye aya mbili.

Lakini Serikali ya Uingereza ilisema taarifa hiyo ya Takukuru sio sahihi, kwani suala hilo halijafikishwa mahakamani.

"Wakati huu kesi inayoihusu kampuni ya BAE na wahusika wake nchini Tanzania, haijafikishwa mahakamani. Kwa hiyo haiwezekani kuhitimisha suala hilo kwa namna yeyote ile ikiwamo kuwaondoa wahusika waliohojiwa na SFO," ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Februari 5 mwaka huu, SFO ilitangaza kuwa imefikia mwafaka na kampuni ya BAE katika uchunguzi wake wa mkataba wa ununuzi wa rada hiyo na serikali ya Tanzania.

"BAe ilikiri kuwa imeshindwa kuweka rekodi sahihi za kihasibu katika uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini. Hivyo ilikiri kosa na kukubali kulipa Paundi 30 milioni kama faini na fidia kwa serikali ya Tanzania," ilisema taarifa hiyo.
Lakini taarifa hiyo ikaongeza kuwa, Mahakama Kuu ya Uingereza ambayo itaanza kusikiliza kesi hiyo ya rada Novemba 23, mwaka huu, ndio yenye mamlaka ya kupanga kiasi cha faini na fidia inayopaswa kulipwa na kampuni ya BAe.

"Makubaliano hayo kati ya SFO na BAE ndiyo yaliyohitimisha uchunguzi wa taasisi hiyo ya makosa makubwa ya jinai kuhusu suala hilo la rada," ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

"Lakini kwa kuwa makubaliano hayo hayajathibitishwa na Mahakama, sio sahihi kusema sasa kwamba, suala hilo limemalizika."

Habari hii imeandaliwa na Hussein Issa, Petro Tumaini, Zaina Malongo na Minael Msuya Dar, Boniface Meena na Habel Chidawali, Dodoma
 
Back
Top Bottom