Fanya uamuzi ulio bora mwana Arumeru-Mashariki

Geza Ulole

JF-Expert Member
Oct 31, 2009
58,776
78,447
Tunapoongelea hali ya chama cha kushika hatamu kuchoka tunamaanisha dira, muelekeo na mtazamo wa makada wake kuanzia wazee na hata vijana kukosa msisimko, mvuto na kusadikisha; vilevile tunaangalia sera na itikadi za chama na kwa jinsi gani makada wanazisimamia sera na itikadi hizo. Ni katika mtazamo huo uchaguzi wa sasa unaoendelea huko Arumeru-Mashariki umevumbua mambo mengi yanayozuwa maswali mengi kuhusu mustakabli wa chama cha Mapinduzi ikiwemo pia ni kwa namna gani stadi, staha na uvumilivu wa chama cha hatamu alias magamba kilivyokosa mvuto na kufikia mahala kinaburuzwa kinakuwa chama cha kujibu hoja zinachosemwa na chama madhubuti cha upinzani yaani CHADEMA! Ni hivi juzi tumeona kuhamaki kunavyoweza futa hamasa na stara za mhusika (mpiga debe) na kumuondoa katika mstari mnyoofu wa kukinadi chama na kumkuta akikididimiza na kukidumbukiza chama anachokitetea katika korongo la kupoteza badala ya kukipeleka kilele cha mafanikio pasi kujielewa!

Katika kampeni za juzi tumeshuhudia kupitia rekodi ya video youtube kada anayesadikika bora ndani ya CCM kwa jina la Livingistone Lusinde (Mh), aliyeletwa mahsusi baada ya kuchaguliwa kati ya wale wote walio CCM akinyesha mvua ya matusi ambayo mbali ya kutukana uongozi mzima wa CHADEMA alifanya hayo mbele ya watoto wadogo walio chini ya miaka 18 yaani wasioweza kushiriki kupiga kura bali kushiriki kunasa utaalam wa kutusi toka kwa viongozi wa nchi yake iliyokosa mwelekeo na pia alifanya hivyo akijua fika kuwa kwa kejeli na dhihaki zake alidharaulisha jinsia ya mwanamke na pia alidhihaki mila na desturi za makabila yetu kupitia kwa mababu zetu! Kivipi basi? ndugu zangu mnaweza kuuliza ametusi vipi jinsia, wazee (wa rika) wanaoheshimiwa katika mila na desturi za Watanzania? Na pia kutukana mila na utamaduni zetu?

Ndg Lusinde akijiita "Kibajaj" katika maudhui yake yaliyoambatana na lugha chafu mbele ya jamii, ametumia tendo lenye tunu ya heshima katika kuanzisha uhai wa mwanadamu (yaani la kutunga na kuzaa) katika hadhi ya kukinaisha na kufedhehesha! Na kwa kufanya hivyo ameshiriki katika kuwakosea heshima na ustaarabu wanawake wote akiwemo pia yule aliyemleta duniani. Ndg huyu amewatusi wanawake wote kwa kupotosha fursa pekee iliyotukuka aliyopewa mwanamke na Mola kwa manufaa ya kupitisha ujumbe wake usio tu wa matusi bali dhihaka kuu! Kwa hali ya kawaida na iliyozoeleka maumbile ya mwanaume hayaruhusu kubeba mimba lakini bwana huyu aliyeonyesha dalili zote za kufyatuka kiakili aliwaongelea wenzie wanaume walio na familia zao kama yeye katika hali ya ujinsia wa kike ambao ulitumika kama usio na heshima na kudharaulika! Kitendo chenye kufedhehesha ndani ya jamii na hata kwa familia kwa kukosa misingi ya familia kama tunavyofahamu. Bwana huyu kwa makusudi alienda mbali zaidi pia kudharau uchungu wanaopitia dada zetu kipindi wanapojifungua kwa kufananisha na uchungu wa hisia za moyo! Zaidi ya hayo alifananisha alama ya V ya CHADEMA na kutungwa mimba ya mapacha ambayo kwa utamaduni wa Kiafrika ni baraka! Pia Bwana huyu katika kujaribu kudanganya umma kuhusu swala lenye utata wa kama Bwana Sumari amewahi kuukana Uraia wa Kenya kama katiba na sheria za Uchaguzi zinavyosema, kwa kupotosha alifananisha kitendo cha uchungu apatacho mwanamke anayejifungulia ndani ya ndege na suala tata la Uraia huku ikijulikana rasmi (kwa sharia za kimataifa)kiumbe kinachozaliwa katika anga ya kimataifa kina haki ya kudai Uraia wa nchi ya kwanza ndege inapotua! Huku ni katika ule mwendelezo wa kukosa heshima kwa mwanamke ambaye ni mzizi wa jamii yeyote duniani.

Mbali ya hayo Bwana huyu "Kibajaj" alienda mbali kudharaulisha mila na tamaduni za makabila ya Kitanzania kwa kupotosha na kusubutu kufananisha kutoga na kutoboa masikio! Katika tamaduni za mababu zetu na mpaka leo kwa baadhi ya makabila yanayodumisha mila kama Wamasai, Wagogo na Wamakonde wanajitambulisha kwa kutoga masikio na si kutoboa masikio! Mimi binafsi sijawahi kuona mzee yeyote wa kiume aliyetoboa masikio bali nimeona wazee waliotoga masikio. Na nimeona wakina mama na wakina dada waliotoboa masikio ambapo jamii inaafiki hilo kama urembo wa jinsia ile! Kwa ueleo wangu mie, kutoboa masikio kwa Wanaume si utamaduni wa Mtanzania, bali umeletwa na utandawazi toka nchi za Magharibi; na hata huko Magharibi kutoboa masikio kuna maana zake kama utambulisho! yaani Kuna aina ya watu wa kuime (kwa hiyari yao hujitambulisha wao) wanawakilisha kundi Fulani kwa kutoboa masikio! Mara nyingi harakati za fursa sawa kwa wote zinapelekea watu kuwa na misimamo na mrengo Fulani wa maisha yao. Mimi binafsi nafahamu makundi yafuatayo mabaharia (mwanzo alama maalum ya utambulisho kwa manahodha), wanamichezo, wanamuziki na mashoga(ambao kinadharia wapo katika sekta/fani zoote hata ambazo nimezitaja)! Sasa tukijaribu kuangalia kwa yule aliyehusishwa na sokomoko hili yeye si kwanza si Baharia, yeye si mwanamichezo, yeye si mwanamuziki bali yeye ni mtu mwenye fani yaani mwanasheria! Je, Bwana huyu anasimama katika kundi gani? na kama jibu ni gumu kutolewa ni haki bwana huyu kufananishwa na Mababu zetu? waliotoga? Au Bwana Lusinde alidhamiria kutusi Wazee wetu wakiwamo wa kihistoria kama Chifu anayeheshimika wa Wazanaki na wale wa Arumeru-Mashariki? pia je, hizi ni sera za chama chake cha CCM? nathani utashi wa wana Arumeru unaweza kung'amua alimaanisha nini hasa!

Tukiangalia misingi ya hoja zilizokuwa zinatolewa na Bwana Lusinde tunaona Mh huyu aliamua kuwekea uzito katika hoja zilizokosa mshiko zenye kuhusu watu binafsi pasipo kueleza chama chake kimefanya na kitafanya nini? na katika hali halisi ya kampeni zilivyokuwa tunaweza kusema maudhui yake yanahusika kwa namna moja ama nyingine na maagizo ya chama chake kwa wanajimbo wa Arumeru. Na kama ni hivyo basi sina burdi kusema chama cha CCM kimepotoka na kukosa adabu kwa wananchi! Badala ya chama chake kueleza kimewafanyia nini wana Arumeri katika miaka 50 ya kushika hatamu Bwana huyu pasi haya wala soni aliporomosha matusi kama vile ndo ustaarabu unaokubalika kwa wanajimbo waliopata kuiunga mkono CCM miaka yote!

Ni katika misingi hii wana Arumeru-Mashariki wanapaswa kuamua sawia, ule muda wa kutumia lugha chafu na mabavu katika kampeni za majimboni umekwisha na ufahamu wa wananchi ni zaidi ya jinsi wana CCM wanaweza kufikiria! Ni muda muhafaka kwa wana Arumeru-Mashariki kuwaamsha wana CCM katika kujitambua kuwa hawawapendezi wananchi kwa kukosa hoja zenye mshiko! Isitoshe Arusha inajulikana kuwa kitovu cha mabadiliko yote yaliyowahi kutokea hapa nchini si Azimio la Arusha si kipindi cha uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na si hata katika uchaguzi uliopita! Hime wana Arumeru-Mashariki fanyeni yale yenye mustakabali chanya kwa nyie na kizazi chenu kijacho kwa kuchagua Bwana Nassari ikiwa kama kuonyesha msisitizo wa kutokubali lugha chafu za matusi zinazotumiwa na CCM na pia kukataa ukatili na uuaji wa Green Guard katika kushurutisha wapiga kura kuichagua CCM. Ni muda muhafaka wa CCM kujitambua. Aprili moja ni tiki kwa Bwana Nassari mwakilishi bora mwenye kudhamini hali halisi ya wana Arumeru-Mashariki.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom