6 Ilipoishia:
Lakini sifa yake kubwa
ilikuwa ni tabia yake ya
kuendesha magari kwa
mwendo kasi. Hata kama
alikuwa akienda sehemu
ya karibu, alipenda
kulikimbiza...
Sasa Endelea...
Mama yake Tonny alikuwa
uani kwake akifua nguo za
mtoto wake wa mwisho,
Subby wakati akitaniana na
kaka yake Tonny aliyeitwa
Santo. Santo alikuwa
akisoma darasa la saba
katika Shule ya Msingi
Bunge na siku hiyo ya
Jumamosi, hakwenda shule.
Mama Tonny alikuwa
akimpenda sana Santo na
mara nyingi walikuwa
wakitaniana. Leo, wakiwa
hapa, mama alikuwa
akimshambulia Tonny
kwamba ni lazima atafeli
kwa sababu ya kupenda
sana filamu. Na kweli, Santo
alikuwa shabiki mkubwa wa
filamu, hasa za Kizungu,
ingawa pia alivutiwa na zile
za Kihindi na Kibongo.
Baada ya kuzidiwa utani na
mama yake, Santo akaamua
kuondoka lakini akamvizia
akiwa amejisahau,
akamtekenya kwenye mbavu.
Mama alipata mshtuko
mkubwa na akiwa na hasira,
aliinuka na kuanza
kumfukuza kijana wake
aliyekuwa anakimbilia nje ya
geti!
***
Baptist alikuwa anakata kona
maarufu mtaani kwao
iitwayo Kwa Kipira, akiwa
katika mwendo wa kasi kama
kawaida yake. Mtaa ulikuwa
kimya na hakukuwa na mtu
barabarani. Akiwa anakaribia
kwenye geti la nyumba ya
Mzee Komba, ghafla
akamuona mtu akitokeza
kwa kasi na kuingia
barabarani.
Hakuweza kujizuia,
hakuweza kulizuia gari,
kishindo kikubwa kikasikika
na mtu mmoja alionekana
akirushwa juu na
alipoanguka chini, akabakia
kuwa mtulivu pale chini
alipofikia.
Alikuwa ni Santo!
Kishindo kile kilileta kelele
kubwa mtaani na mara
moja, kila mtu aliyekuwepo
alitoka nje ya nyumba ili
kushuhudia kilichotokea.
Bap alifanikiwa kusimamisha
gari mita chache mbele,
akatoka nje ya gari na
kumkimbilia mtu
aliyemgonga!
Kishindo kile kilikuwa kama
nyundo iliyopiga katika
kichwa cha mama yake
Tonny, alitambua kabisa
kwamba aliyegongwa ni
mtoto wake. Naye pasipo
kutarajia alianguka na
kupoteza fahamu muda
uleule mwanaye
alipogongwa.
Ndani ya dakika moja, watu
wengi walijazana pale
alipokuwa amelala Santo,
mwili wake ulijaa damu na
watu wakawa kama
waliochanganyikiwa. Kwa
muda wakawa hawajui
wafanye nini hadi akili
zilipowarejea.
Baptist alikuwa wa kwanza
kumshika Santo, akamgeuza
vizuri na kumtazama, akatoa
ishara kwa wenzake
wambebe, wakampakia
kwenye gari alilomgonga
nalo. Watu wengine wawili
wakaingia ndani ya gari lile,
kwa kasi ya ajabu,
likaondoka kuelekea
hospitalini!
Watu wengine nao mtaani
wakawasha magari yao na
kulifuatilia gari lililombeba
Santo. Baptist aliendesha
gari kwa kasi hadi alipofika
katika Hospitali ya Mico
iliyopo Tegeta Basihaya.
Madaktari wakampokea
haraka mgonjwa na moja
kwa moja akapelekwa
chumba cha upasuaji!
Nyumbani kwa akina Santo,
baadhi ya majirani
walishtuka baada ya
kumuona mama yake Santo
akiwa amelala chini, tena
kwa namna ya kutisha.
Walipomchunguza,
wakagundua kwamba
alikuwa amepoteza fahamu.
Wakamfanyia huduma ya
kwanza, kisha wakambeba
na kumwingiza ndani kwake.
Alirejewa na fahamu baada
ya nusu saa, akashangaa
kuona watu wamemzunguka
sebuleni alipolala kwenye
kochi.
Vipi? aliwauliza wanawake
wawili waliokuwa karibu
yake, akiwemo mama yake
Juddy.
Tulia, tuliza akili kwanza,
upo salama? mama Juddy
alimwambia mwenzake huku
akimtengeneza vizuri kanga
zake alizojifunga.
Kuna nini kimetokea dada,
niambie haraka, mama yake
Santo alimwambia mama
Juddy huku akimshika
mikono yake kwa nguvu
kubwa.
Tumekukuta umeanguka
pale mlangoni kwako, ndiyo
tukakubeba na kukuingiza
ndani, alijibiwa!
Mnenikuta nimeanguka?
aliuliza tena na kuanza
kuvuta kumbukumbu.
Je, nini kitatokea? Usikose
kufuatilia simulizi hii
katika toleo lijalo.