FALSAFA YA ELIMU YA KUJITEGEMEA KULINGANISHA NA SERA YA ELIMU BURA YA LEO

Omary Kipingu

Member
Feb 22, 2016
40
48
FALSAFA YA ELIMU YA KIJITEGEMEA KULINGANISHA NA SERA YA ELIMU BURE YA LEO.

Na Mchambuzi Alexander Mhando.

Utangulizi;

Tunapozungumzia elimu katika Taifa letu la Tanzania hauwezi acha kumtaja na kumzungumzia Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere. Kwani Mwalimu Nyerere alitaka kila mtanzania apate elimu, na juhudi zake katika kuhakikisha hili linafanikiwa zilianza kabla ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Katika mikutano mbalimbali ikiwemo mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1956, kati ya mambo aliyoyazungumzia Mwl Nyerere alipopata nafasi kuzungumza na hadhira hiyo ya UN, lilikuwa ni suala la la ubaguzi wa Elimu wakati wa ukoloni, ambapo elimu ilikuwa ikitolewa kwa makundi huku watoto wa kiafrika wakiwa katika kundi la chini kabisa. Katika hili mwalimu alinukuliwa akisema “Nchini Tanganyika elimu inatolewa kibaguzi, watoto wote wa kizungu na wakiasia wanakwenda shule lakini asilimia 40 tu ya watoto wa afrika ndiyo wanakwenda shule” ilisema sehemu ya hotuba yake, ambayo iliashiria mtazamo aliokuwa nao wa baadae juu ya Tanganyika huru.

Falsafa ya Elimu baada ya Uhuru wa Tanganyika;

Baada ya Uhuru, Mwalimu alikuwa tayari ana mitizamo tofauti wa kuibadili elimu iliyokuwa ikitolewa na wakoloni na kubadili mfumo ambao ulikuwa wa kibaguzi kwani kulikuwa na shule za wazungu, wahindi na za watu weusi. Mwalimu alitumia mfumo wa kuwachanganya wanafunzi kutoka maeneno mbalimbali bila kujali dini , rangi wala kabila katika mashule , akiamini katika dhana ya usawa wa binadamu kwamba elimu ni haki ya kila mtu.

Mwalimu Nyerere pia alitumia juhudi kubwa kuhakikisha kuwa kila mtu anapata elimu kuanzia watoto hadi watu wazima, bila kujali kama ni matajili au masikini ili mradi tu ni Mtanzania na anaakili timamu. Na watu hawa wote walipata elimu hii bure kabisa ambapo iliwasaidia hata wale ambao hawangeweza kulipia masomo, waliweza kusoma hadi vyuo vikuu bila malipo.

Falsafa ya Mwalimu Nyerere Juu ya Elimu ya Kujitegemea;

Elimu ya kujitegemea (Educationa for self Reliance) ilianzishwa na kuasisiwa March ,1967 na Mwalimu Nyerere ilikuwa imejikita katika elimu iliyokuwa na lengo la kuwajenga Vijana kujifunza zaidi kazi za uzalishaji mashuleni, na kuziwezesha shule zijitegemee kutokana na uzalishaji huo.

Mbali na hizo shule kujitegemea, kazi hizo ziliwawezesha wanafunzi kujengwa kwa namna ambayo iliwapevusha fikra zao, na hivyo kuleta mtizamo chanya na mabadiliko ya kweli katika jamii kufuatana na ujuzi walioupata.

Pia nje ya wanafunzi kupewa elimu ya darasani, vile vile walipewa elimu ya stadi za maisha. Dhana hii ya Mwl. Nyerere aliyoiasisi juu ya Elimu ya Kujitegemea iliondoa mapungufu mengi yaliyokuwepo kwenye elimu ya mkoloni ambayo iliegemea zaidi katika jamii ya kibepari kwani iliandaa watu kutawaliwa na sio kujitawala.

Mpango huu wa elimu ya kujitegemea ulifanya wanafunzi wafanane na maisha ya kitanzania na kuwafanya wanafunzi watambue wajibu wao kwa jamii baada ya kumaliza shule na vyuo vikuu.

Falsafa ya Elimu Bure itolewayo Leo;

Unapozungumzia dhana ya elimu bure kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha nne kwa sasa, hauwezi itenganisha na sera ya serikali juu ya elimu bure na pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilinadiwa na aliyekuwa mgombea wa uraisi October 2015, kupitia CCM ambaye kwa sasa ndio Raisi mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Dr. John Pombe Magufuli pamoja na mwenyekiti wa Chama na Raisi Mstafu Mh. Jakaya M. Kikwete kwani waliona mbali katika kuendeleza falsafa za mwalimu Nyerere juu ya Elimu yetu.

Elimu bure inayotolewa sasa ilikuwa na lengo na shabaha ya kuwasaidia watoto wote wa Tanzania kupata elimu bila kujali tofauti zao za kiuchumi katika familia zao. Na hii ni kutoka katika sera ya serikali juu ya elimu bure na ilani ya CCM. Kabla ya elimu kutolewa bure motto wa kabwela au wa mlala hoi alikuwa na nafasi finyu ya kusoma elimu ya sekondari hadi elimu ya juu ukilinganisha na motto anayetoka familia yenye uwezo mkubwa kiuchumi.

Nini kifanyike kuboresha dhana ya elimu bure kuendana na falsafa ya Elimu ya kujitegemea;

Kwanza ni vema kuendelea kuipongeza serikali katika kusimamia vizuri mpaka sasa swala la kutoa elimu bure kwani tumeshuhudia shule zote mpaka sasa hazitozi malipo yoyote, hili linapaswa kupongezwa na kuendelea kuungwa mkono.

Lakini pia katika mpango huu mpya ni vizuri kila mmoja akatambua tulipotoka katika swala la elimu katika Taifa letu ili aone hatua tulizopiga katika elimu tokea uhuru mpaka sasa na ndipo aweze kutoa mchango sahihi katika kuboresha mpango huu wa elimu bure kwa sasa na sio kukosoa tu na kulalamika bila kufanya utafiti na kujua nini ashauri ili kuboresha.

Tunaamini mpango huu wa elimu bure bado unahitaji kuongezwa uboreshaji ili kwamba usiishie tu kutoa elimu bure kwa kufuta ada na michango lakini pia yafuatayo ni vema pia wakafanyiwa kazi katika kuboresha elimu yetu:

· Kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo posho na mishahala pamoja na malupulupu yote yanayostahiki kwa walimu .

· Kujenga makazi(Nyumba) za walimu katika kila shule na hili linawezekana kama serikali itaamua kutengeneza utaratibu mpya kwa kulitumia shirika la nyumba la Taifa katika kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu.

· Kutengeneza na kuhakikisha uwepo wa miundombinu mizuri ya kufundishia ikiwemo madarasa, madawati, Vitabu , maabara n.k. vinavyotosheleza na vinavyoendana na wakati.

· Kutoa elimu ya kifikra kwa watu wote juu ya kutoka katika mtizamo tegemezi kwa serikali na kurudi katika misingi ya “elimu ya kujitegemea” (Education for self Reliance) .

· Kusimamia elimu inayotolewa iwe elimu ambayo itapanda mawazo ya Taifa la kijamii tunalotaka kulijenga na sio Taifa la kibepari.

· Kuandaa mtaala mpya wa elimu ambao utahakikisha kwamba wale waliosoma wanajitambua kwamba ni sehemu ya Taifa na kwamba kwa kuwa wamepata nafasi zaidi, basi wajibu wao kwa Taifa ni mkubwa zaidi.

· Serikali itenge bajeti ya kutosha angalau asilimia 30 ya bajeti ya serikali na pia kuipa kipaumbele cha kwanza sekta ya elimu kwani ndio msingi wa kila maendeleo tunayohitaji kama Taifa.


Mwisho;

Nitaendelea kuipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na CCM chini ya Raisi Dr. John Pombe Magufuli kwa ubunifu na uweledi katika utendaji ambao unajikita katika KAZI TU. Pia ninaomba serikali ihakikishe elimu inayotolewa izingatie kuwajenga vijana wa Tanzania katika misingi tuliyoachiwa na Mwl. Nyerere juu ya elimu ya kujitegemea na kuhakikisha kuwa watoto wetu waelimishwe kuwa raia wa wema na wenye uzalendo wa kesho na watumishi wa wananchi walio sawa katika Taifa tunalolijenga la kijamaa na sio kibepari, bila kusahau maslahi ya walimu na mazingira bora ya kufundishia.

Copy and Paste
 
Pia ninaomba serikali ihakikishe elimu inayotolewa izingatie kuwajenga vijana wa Tanzania katika misingi tuliyoachiwa na Mwl. Nyerere juu ya elimu ya kujitegemea

Niliwahi ongea na baadhi ya wazee waliosoma zamani wakaniambia zamani walisoma shule za msingi zilizokuwa na masomo ya Ufundi zote(TRADE SCHOOLS).Wakitoka walikuwa wanaweza kujitegemea kwani walikuwa wanaweza fanya kazi kama za useremala nk

Ili mwanafunzi akitoka awe na uwezo wa kujitegemea nashauri katika mipango ya elimu shule zote za sekondari masomo yaliyoko VETA yawe sehemu ya masomo ya lazima mwanafuzi kusoma.Masomo yatakayoingizwa kwenye mitaala yawe yale yanayohusiana hasa na mazingira yetu yanayotuzunguka.Masomo yanayoweza kuwemo ni kama kilimo,ufugaji wa mifugo mbali mbali ikwemo ufugaji wa samaki,Upishi,utengenezaji bidhaa mbali mbali kutokana na vile tunavyozalisha nchini

Watoto wengi wamekuwa wakionekana kama hawapendi kilimo na ufundi sababu ni kuwa hawafundishwi mashuleni.Hawajui kulima wala kufuga sababu nyumba wanazoishi hazina shughuli hizo.Mtoto kazaliwa gorofani kakulia gorofani unategemea atapenda kilimo na ufugaji wapi wakati saa zote anasoma vitabu tu vya tuition kutwa? Ndio maana lazima kama nchi iwasaidie masomo yawepo sekondary kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.Hii itawasaidia pia watoto baadaye wa mijini wapende kwenda kuishi vijijini sababu waweza enedesha shughuli za kilimo na ufugaji walizojifunza

Nimependekeza sekondary sababu walau watoto wanakuwa wakubwa kidogo ndio umri wa kufundishwa kujitegemea
 
Back
Top Bottom