Faida lukuki mashirika ya umma kuweka fedha BoT

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
KATIKA siku zisizozidi 100 ambazo serikali ya Awamu ya Tano imekuwa madarakani, imefanya mambo mengi yanayolenga katika kuijengea uwezo wa kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi sambamba na kuhakikisha wananchi pia wanaondokana na mizigo mbalimbali inayowalemea.

Katika muktadha wa kubana na matumizi, kujijengea uwezo na kuyafanya mabenki kukopesha wananchi kwa riba nafuu, hivi karibuni serikali iliagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya biashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizoko katika akaunti hizo kwenda akaunti zitakazofunguliwa Benki Kuu (BoT). Taasisi za umma zinazohusika na agizo hilo inaelezwa kwamba ni pamoja na serikali za mitaa na taasisi nyingine zote katika mihimili mitatu ya dola, yaani bunge, mahakama na serikali kuu.

Agizo hilo ambalo limepongezwa na wananchi wengi, huku wachache wakilipinga na kuzua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, liliwataka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za umma, kufunga akaunti zao katika mabenki ya biashara na kuhamishia fedha zao BoT. Pili, watendaji walitakiwa kufungua akaunti ya mapato yao kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea, kama ni kwa fedha za kigeni au za Tanzania, katika tawi la karibu yao la BoT haraka.

Baada ya kufungua akaunti hizo, watendaji hao walitakiwa kuelekeza makusanyo yote ya fedha za ofisi zao, ikiwemo fedha za ruzuku zinazotoka serikalini kwenda katika akaunti mpya zilizofunguliwa katika matawi ya BoT. Taarifa ya serikali ilisema kwamba uhusiano pekee kati ya mashirika hayo na mabenki ya biashara utabaki kwa kuwa na akaunti itakayohifadhi fedha za uendeshaji ambayo imetakiwa kuwa na fedha zinazotosha uendeshaji wa shughuli za taasisi zao kwa mujibu wa matarajio ya matumizi yao ya kila mwezi.

Katika agizo hilo, watendaji hao wameaswa kuhakikisha fedha yoyote itakayokuwepo katika akaunti hizo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za taasisi, ihakikishwe inapata mapato ya riba kulingana na viwango vya riba vilivyopo katika soko. Mwanzoni mwa wiki hii, kulikuwa na taarifa kupitia gazeti hili kwamba mashirika mengi na taasisi za umma zilikuwa zimeshatoa taarifa za utekelezaji wa maagizo hayo.

Ilielezwa pia kwamba akaunti zingine za mashirika na taasisi za umma ziko katika akaunti za muda maalumu katika benki hizo za biashara, hivyo kabla ya kuzifunga na kuhamisha fedha husika, kulihitajika majadiliano kati ya shirika au taasisi husika na benki yake. Sababu za hatua hiyo Kabla ya agizo hili, pesa nyingi za mashirika ya umma na taasisi za serikali ikiwemo mifuko ya ustawi wa jamii zilikua zinawekwa katika akaunti za mashirika ya umma zilizoko katika mabenki binafsi.

Pesa hizi ni zile za miradi mkubwa ya muda mrefu, makato ya viinua mgongo vya wafanyakazi, tozo mbalimbali na mapato mengine ambayo ni mabilioni mengi ya pesa. Hali hii ilifanya mabenki binafsi kuwa na pesa nyingi ambazo wamekua wakizifanyia biashara, kutoa mikopo yenye riba kubwa, wakati mwingine kuikopesha serikali yenyewe na hivyo kupata faida kubwa. Serikali ilikuwa hainufaiki vizuri na pesa hizi za mashirika yake zilizokua kwenye mabenki hayo.

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru anafafanua kwamba wakati mwingine mashirika hayo ya umma hupelekewa fedha za ruzuku nyingi kuliko mahitaji yao ya wakati huo na Serikali inapopungukiwa na hivyo kulazimika kutafuta fedha za kukopa kutoka vyanzo vya ndani, mabenki hayo huchukua fedha hizo za ruzuku na kuzikopesha kwa Serikali kupitia mnada wa hati fungani za Serikali.

“Katika mazingira hayo, Serikali hujikuta ikikopeshwa fedha zake yenyewe na wakati wa kulipa mikopo hiyo, hulazimika kulipa na riba ambayo ni fedha ya wananchi inayotumika kulipa mabenki hayo, wakati ingeweza kufanya kazi zingine za maendeleo ya wananchi,” ilisema taarifa ya serikali. Mmoja wa wanaounga mkono hatua hii ya serikali, Ally Hapi anasema: “Agizo hili maana yake ni kuwa serikali ndiye mmiliki wa pesa zote za taasisi na mashirika hayo, hivyo sasa zitatunzwa katika benki ya serikali, yaani BoT.”

Hoja za wapingaji

Kama ilivyodokezwa hapo juu, wapo wanaopinga hatua hii na hoja zao, kabla ya kuangalia faida za hatua hii ya serikali ni kama ifuatavyo. Wanadai kwamba uamuzi huo unaweza kudumaza uchumi wa nchi kwa madai kwamba fedha hazijawahi kukaa benki kuu zikakuza uchumi badala ya kuwa katika mzunguko na kuzalisha mali kupitia katika benki za biashara.

Wanaona kwamba wafanyakazi wengi wa serikali wataathirika kwa sababu benki hazitakuwa na fedha za kuwapa mikopo kama zilivyokuwa zikifanya. Kwa mantiki hiyo wanaona kwamba huenda wafanyakazi watarudi kwenye hali ya miaka ya nyuma ambapo mtumishi wa umma akinunua gari au kujenga nyumba alikuwa anaonekana kuwa tofauti sana na wengine.

Wanadai kwamba usafirishaji wa fedha za serikali kutoka sehemu moja kwenda nyingine utakuwa na gharama kubwa na kwamba taasisi nyingi za serikali zitakosa mapato makubwa yaliyokuwa yanapatikana kwa njia ya kuwekeza kwenye akaunti za muda maalum wakati wa kusubiria miradi ya serikali kuanza. “Benki kuu huwa hazifanyi biashara, bali zinasimamia uchumi wa nchi usianguke kupitia katika benki za biashara,” anaandika mchangiaji mmoja katika mitandao ya kijamii.

Faida zaidi

Lakini kwa mujibu wa wanaounga mkono hatua hii ya serikali akiwemo Ally Hapi, wanasema, hii ni hatua ya kukaribisha kwa mikoani miwili kwani sasa serikali ndiyo itakuwa inamiliki pesa zake na hivyo kuwa na hazina ya kutosha Benki Kuu. Hapi anazidi kusema kwamba serikali itaweza kupunguza gharama ya mikopo ambayo ilikuwa ikikopa kwa mabenki binafsi na hivyo sasa itakuwa inaazima fedha hizo BoT.

Tatu, anasema Benki Kuu inaweza kuwa na utaratibu wa kutoa mikopo nafuu kwa taasisi binafsi na mabenki hivyo pesa hizo kufanya biashara ambayo faida yake itakuwa inarudi kwenye benki ya umma, yaani BoT. Anasema Benki Kuu itakuwa na udhibiti wa karibu wa uchumi wa nchi na maendeleo ya kiuchumi ya mashirika na taasisi za serikali. Faida nyingine anasema serikali itakuwa imeongeza uwezo wake wa kuhudumia wananchi na kufanya miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa kuwa itakua na uwezo wa kiuchumi.

Serikali itakuwa imepunguza gharama kubwa ambazo ilikuwa inaingia wakati pesa hizo zilipokuwa katika mabenki binafsi. Gharama hizo ni kama mikopo yenye riba kubwa ambayo huongezeka kila ulipaji wa deni unavyochelewa. Kuhusu mtazamo kwamba mzunguko wa fedha utapungua, Msajili wa Hazina, Mafuru, anasema wenye mtazamo huo wanasahau kwamba BoT ni benki na mabenki yanapopungukiwa fedha, hukopeshana yenyewe kwa yenyewe na kutozana riba, lakini pia yana fursa ya kwenda kukopa BoT.

Kwa mujibu wa Mafuru, kwa kuwa BoT kwa hatua hiyo itakuwa na fedha nyingi, mbali na kuikopesha Serikali wakati itakapopungukiwa fedha, pia itakopesha mabenki ya biashara pale yatakapopungukiwa fedha. Katika hatua hiyo, anasema BoT itakopesha mabenki ya biashara kwa riba ndogo kuliko inayotumika na mabenki hayo wakati wa kukopeshana yenyewe kwa yenyewe, hivyo kutumia fursa hiyo kudhibiti riba ya mabenki hayo kwa mikopo itakayotolewa kwa wananchi.

Kwamba sasa itakuwa rahisi kwa BoT kuongeza mzunguko wa fedha, kwa kuwa na yenyewe itakuwa ikikopesha mabenki hayo kwa riba ndogo, ili mabenki hayo ya biashara yakopeshe wananchi kwa riba ndogo pia. Anasema hali hiyo itakuwa ni sawa na kuyadhibiti mabenki kibiashara kuliko kushinikiza mabenki kupunguza riba, wakati yapo katika soko la ushindani.
 
Hapo naona majukumu ya BOT yanakuwa sawasawa,sio BOT na serikali kukopa bank binafsi hii ni aibu. Ngoja tuone mambo baada ya 6 month
 
Hii itakuwa ngumu kwa biashara ambazo azipo kisheria, kama biashara za utakatishaji pesa haramu
 
Back
Top Bottom