Fahamu yote kuhusu elimu kombozi

Tutor B

JF-Expert Member
Jun 11, 2011
9,025
6,554
ELIMUKOMBOZI

1.0 Utangulizi

Elimu ni suala la jamii ambalo mipango na taratibu zake zinahitaji kushirikisha wadau wote katika jamii. Madhumuni ya Elimu kwa ujumla ni kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi watu wa kizazi cha leo na vizazi vijavyo. Inakusudiwa kuwapa watu maarifa na ujuzi watakaoutumia vizazi na vizazi ili kuwasaidia kupata njia mpya na bora zaidi ya kutatua matatizo yao ya kiafya, kiuchumi, kijamii na mengine yanayohusu mazingira wanayoishi.

Elimu lazima imkomboe binadamu kiakili na kimwili, imuwezeshe binadamu kujikwamua na kumpa binadamu uwezo wa kupambana na matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha. Inapaswa kuipa jamii utambuzi au ujuzi kuwa wao ni nani, wanatoka wapi, wanakwenda wapi, na wajipange vipi ili wafike huko wanakotaka kwenda.


Malengo ya msingi ya elimu ni kumkomboa binadamu. ‘Kumkomboa maana yake ni kumweka huru, na kumweka huru kutoka hali au jambo fulani’ (Nyerere 1974). Inamaanisha kuwa kuna vikwazo ambavyo lazima avishinde. Tanzania mara tulipopata uhuru mwaka 1961 tulisema kuwa tuna maadui watatu: ujinga, maradhi na umaskini. Maadui hawa bado tunao hadi leo; ni vikwazo ambavyo tunaweza kuvishinda tukipata elimu, na hasa tukipata Elimukombozi.


2.0 Elimukombozi ni nini?

Mwalimu Nyerere alifafanua Elimukombozi kuwa ‘ni aina ya elimu inayomkomboa Mwafrika kutoka mawazo ya utumwa/kitumwa na ukoloni na kumfanya ajihisi kuwa binadamu sawa na…binadamu wengine, mwenye haki na wajibu wa kibinadamu. Elimu inayomkomboa kutoka tabia za kukubali mazingira yanayomnyanyasa na kupunguza utu wake na hadhi yake kana kwamba hayabadilishiki na hana uwezo juu ya mazingira hayo. Pia lazima imkomboe kutoka minyororo ya ujinga wa teknolojia ili aweze kutumia vifaa vya kujiweka sawa ili kujiendeleza yeye na binadamu wenzake (Nyerere 1974).

Dhana hii ya elimukombozi hapa imetumika kumaanisha elimu inayomwezesha binadamu kujitambua, kujikomboa na kushiriki katika kuikomboa jamii yake. Katika muktadha wa Afrika na Tanzania ni elimu inayomtoa Mwafrika kutoka mawazo ya kitumwa tuliyopandikiziwa na elimu tuliyoirithi kutoka kwa wakoloni na ambayo mengi tumeyaendeleza hata baada ya Afrika yote kuwa na uhuru wa bendera.

3.0 Elimu tuliyorithi kwa wakoloni na athari zake

Elimu yetu hivi sasa haina sifa tulizotaja za Elimukombozi. Elimu ya sasa ni elimu tuliyoirithi kutoka kwa wakoloni. Sote tumeathirika kwa kiasi kikubwa na elimu hii. Malengo yake yalikuwa kutubadili/kutugeuza (Buchert 1994) ili tuwe watumishi wema, watiifu, wasiouliza maswali, wavumilivu, wenye bidii ya kazi na wenye kukubali hali yo yote ya maisha, hata iwe ngumu kiasi gani. Ni elimu inayojenga uwoga na utiifu usiohoji hata masuala ya msingi; inayojenga

upole unaorahisisha kutawaliwa kwa maslahi ya wengine. Elimu ya kikoloni pia imetugeuza na kutufanya tudharau mambo yetu na kujidharau au kukosa kujiamini. Elimu hii imetugeuza kuwa watumwa kiasi kwamba sasa, miaka zaidi ya 56 tunajiendesha wenyewe kama ilivyokusudiwa na mkoloni.

Kwa maneno mengine, tunajigeuza kuwa watumwa wa ukoloni sisi wenyewe kwa manufaa ya nchi tajiri na gharama ya kujigeuza kuwa watumwa tunailipa sisi. Mbaya zaidi, hatuamini kwamba hicho ndicho tunachokifanya. Elimu pia imetufanya kuthamini kipato kuliko huduma tunazotoa kwa jamii zetu; tukidai kuwa thamani yetu katika soko ni juu zaidi kuliko mshahara tunaolipwa Tanzania. Mwalimu Nyerere (1974) alisema ‘binadamu pekee wenye thamani katika soko ni watumwa’. Yaani bila kujitambua tunasema kwamba ‘elimu hii tuliyopata imetugeuza kuwa bidhaa za kuuzwa sokoni kama pamba, katani au kahawa’

Katika mustakabali wa utandawazi na soko huria, elimu tuliyoipata na tunayoendelea kutoa haitusaidii kama jamii, kwa kuwa haitukomboi katika utumwa bali inatuweka tayari kuwa watumishi wema, watiifu, wasiouliza maswali, na wavumilivu wa mataifa tajiri. Elimu yetu imekuwa mradi wa mataifa tajiri wa kuendeleza ukoloni wao hata baada ya uhuru wa kisiasa.

Haijatuandaa kutafuta suluhu au kujiuliza namna ya kujikwamua. Tunakuwa tumebaki kulalamika na kukosa matumaini. Hata viongozi, maprofesa, madaktari wasomi wa falsafa tunalalamika; tumechanganyikiwa, hatujui tulipokosea na tunaamua kuukataa ukweli tunaoujua! Naamini kabisa kuwa haya ni matokeo/matunda ya elimu tuliyorithi na tunayoendelea kutoa katika taifa letu na hata bara zima la Afrika.


Elimu tuliyopata imetuandaa kuulimbukia utandawazi (na mengine yote watakayosema nchi tajiri) bila kutambua kuwa ni mwendelezo wa ukoloni. Hatutambui kuwa elimu tuliyopata imetulea tuamini kuwa hivi ndivyo inavyopaswa kuwa; ndiyo maana tukakubali na tukayaendeleza hadi leo. Ni muhimu tujiulize kama tunapenda kuendelea na hali hii ya utumwa wa kujitumikisha wenyewe kwa manufaa ya mataifa tajiri huku tukilipa gharama za kujigeuza watumwa, au tujikomboe na tuondokane na utumwa huu. Njia mojawapo ya kujikomboa ni kurudi katika misingi ya Elimukombozi kama alivyoainisha Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere.

Tukitambua kuwa haitatusaidia hata kama tukijitahidi kujidharau na kuamini kwamba tukikataa mambo yetu, tutakuwa kama wazungu, kamwe hatutakuwa, na hatatuweza kujibadilisha. Tutabaki Waafrika kama tulivyo. Ni heri tujikubali na tuanze kujithamini na kujiheshimu kama binadamu wengine. Tuondokane na utumwa huu kwa maana hata hao tunaotaka kufanana nao hawatutaki na kwa kweli hawataturuhusu tuwe kama wao hata tungejaribu vipi. La msingi ni kwamba hatuhitaji kuiga kila kitu kiasi cha kujidhalilisha. Tukilitambua hilo, tutakuwa katika hatua ya kuanza kujikomboa.


4.0 Elimukombozi kuwa njia ya kujikwamua.

Kazi ya kujikomboa, hasa tunapoamini kwamba hatuna tatizo la utumwa wa kifikra ni changamoto kubwa. Kazi kubwa ya kwanza ni kuwafanya watu wajitambue kuwa sisi sote tu waathirika wa elimu ya kikoloni. Tunahitaji kushirikiana na wadau wa sekta na maeneo mbali mbali ya jamii yetu tueleweshane kwamba tunahitaji Elimukombozi. Ukisoma makala ya wataalamu katika sekta mbali mbali (Kaduma 2003, Simba 2003, Lazaro na Mdoe 2003, Likwelile 2003) utaona kwamba baadhi wanakubali kuwa tuna mawazo ya utegemezi, ambayo nayatafsiri kuwa ni dalili za utumwa. Tunapoulizana wapi tuanzie ili kuondokana na wale adui watatu: ujinga, maradhi na umaskini tulioainisha mara baada ya uhuru, wengi huwa wanajibu kwamba tuanze na kuboresha uchumi wa nchi. Yaani tuuondoe umaskini kwanza, halafu ndiyo yafuatie ujinga na maradhi.

Kwa maoni yangu, naamini ni muhimu kuanza kwenye elimu kwa kuwa ndiyo inayotupa ufahamu, uelewa na dira ya kuwa: sisi ni nani, tunatoka wapi, tunataka kwenda wapi na tunahitaji kufanya nini ili tufike huko tunakotaka kwenda. Kama alivyosema Ngugi wa Thiongo, kuwa wasomi wa Afrika tuna jukumu la kuunganisha ‘kichwa na kiwiliwili’ cha Bara letu Afrika, baada ya wakoloni kuvitenganisha. Kichwa ikiwa ni viongozi na wasomi na kiwiliwili ni jamii ya watu wa Afrika.

Kwa hiyo, jambo la uelewa wa pamoja kama jamii katika suala la kujitambua naliona ni la muhimu sana na la msingi. Kwanza, jambo la kuelewana na kukubaliana na kuweka mwelekeo halina gharama kubwa zaidi ya rasilimali watu, ambayo tunayo kwa uwingi. Pili, bila kuwa na uelewa, makubaliano na ushiriki wa wadau wengi, umaskini na maradhi ni vigumu kupambana navyo. Kwa hiyo, elimu itakayotoa ujinga, itatupa mwanga wa kuyafanya hayo mengine kwa manufaa ya jamii. Tatu, tusipoanza na hili la kuondoa ujinga, (na kujikwamua kwenye utumwa) ni rahisi tukadanganywa na wajanja kwa manufaa yao binafsi au ya jamii zao.

Wengi watahoji: tutaanzaje na elimu wakati tuko maskini? Hoja yao ni kwamba tukiboresha uchumi, ndiyo utakaotumika kuboresha elimu na kuondoa ujinga. Sikubaliani na hoja hii kwa sababu kabla hatujajikomboa kifikra na kiakili (kupitia elimu, hasa elimukombozi) siyo rahisi kukuza uchumi kwa manufaa ya jamii zetu. Tuanze katika elimu na tubadilishe mitazamo ya kutawaliwa na kutumikia wengine. Tuwe binadamu huru, sawa na binadamu wengine; kama tulivyopambana tukapata uhuru wa kisiasa (bendera) vivyo hivyo tuanze kutafuta uhuru wa kifikra, kimtazamo na kimawazo kwa kuanzia kwenye elimu na kuifanya elimu yetu iwe Elimukombozi. Ili kuwa na Elimukombozi tunahitaji kuchukua hatua kadhaa; baadhi ya hizo hatua ni kama ifuatavyo:

1. Elimu ilenge katika kuwaandaa wasomi kuwa wadadisi, wanaouliza maswali na kutafuta majibu ya matatizo yanayoikabili jamii. Wawe na uwezo wa kufikiri, kuchambua, kutafakari na kutumia taaluma walizojifunza shuleni na vyuoni kutatua matatizo ya jamii. Mitaala na mbinu za kufundishia ziendane na malengo ya elimu; ili kufanya mitaala iwe na malengo ya kujikomboa

2. Elimu iwe sehemu ya jamii, na kamwe isijaribu kuwatenganisha wasomi na jamii zao ili kuwa na mawasiliano ya karibu kufanikisha maendeleo. Wasomi wapewe changamoto ya kuandaa makala katika lugha rahisi kwa ajili ya jamii zao. Kwa kuwa ni kujidhalilisha na wala hatunufaiki kukataa utambulisho wetu kama Waafrika, bora tuikubali hali hiyo na kuanza kujithamini.

3. Tutumie wataalamu wetu kuandika vitabu kwa ajili ya shule zetu, ili tusiwe wategemezi kwa baadhi ya vitabu ambavyo siyo lazima kuagiza kutoka nje.

4. Tuanzishe tafiti zinazolenga kuendeleza jamii zetu katika maeneo ya sera na mipango. Ili elimukombozi iweze kufanikiwa, inahitaji lugha inayoeleweka kwa walimu na wanafunzi; jambo ambalo tutalijadili katika sehemu inayofuata.


5.0 Suala la Elimukombozi, lugha na upashanaji habari.

Katika sehemu hii tutajadili na kuonyesha jinsi gani Elimukombozi inavyotegemea lugha. Hapa kuna suala la lugha katika nyanja mbili: ya kwanza, ni lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni. Pili, ni lugha inayotumika na kueleweka zaidi katika jamii. Uelewa wa lugha uko katika ngazi tofauti. Ingawa ngazi hizo zinaweza kuwa nyingi, na ni za hali ya mfululizo, katika makala hii nitaainisha ngazi tatu tu kama ifuatavyo:


5.1 Ngazi ya uelewa wa lugha na uwezo wa mzungumzaji kutumia lugha hiyo

1. Uelewa mdogo sana: “Uwezo wa lugha ya kuombea maji”. Akilazimika kutumia kujifunzia lugha katika ngazi hii mzungumzaji inabidi akariri karibu kila kitu kwa kuwa ana uelewa mdogo. Huchukua muda mrefu kuelewa mambo madogo kwa kuwa lugha ni kikwazo. Haoni uhusiano kati ya maisha yake na mambo yale anayofundishwa au anayoelezwa shuleni. Masomo humchosha na mawazo huhama darasani/kutoka eneo la mazungumzo.

2. Uelewa wa kati: Uwezo wa kumpa mtu maelekezo ya namna ya kufika sehemu fulani. Uelewa wa juu juu wa mambo yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha hiyo. Tabia ya kukariri bado inaendelea, ingawa imepungua kwa kiasi kikubwa. Uwezo wa kuandika sentensi fupi fupi sahihi na kuuliza maswali rahisi. Kuna uwezekano mkubwa wa kutoelewa, au kuelewa vibaya maana iliyokusudiwa. Lugha bado ni kikwazo katika kutoa ushiriki wakati wa kufundishwa au katika mazungumzo ya kawaida.

3. Uelewa wa hali ya juu: Uwezo wa kufikiri, kutafakari, kujadili, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbali mbali yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha husika. Mzungumzaji anakuwa na uwezo mkubwa wa kutumia lugha kama nyenzo ya kuvumbua mambo mapya; ana uhuru wa kutumia lugha husika na yote atakayoelezwa katika kujikomboa kimawazo. Lugha siyo kikwazo katika kuelewa, kupambana na changamoto za maisha. Hahitaji kukariri; bali hutumia uelewa wake katika kujibu maswali au kutoa maelezo juu ya yale anayoyaelewa. Ni katika hatua hii ya uelewa ndiyo wanafunzi wanapoweza kushiriki Elimukombozi.


Tafiti nyingi (Mlama na Matteru 1978, Criper and Dodd 1984, Roy-Campbell and Qorro 1987, Rubagumya, Jones and Mwansoko 1998, Qorro 1999, Mwinsheikhe 2003, Puja 2003, Brock Utne 2004, Vuzo 2005) zimeonyesha kuwa wanafunzi wengi katika shule za sekondari na vyuo nchini Tanzania wana uwezo wa hatua ya kwanza au ya pili ya uelewa wa lugha inayotumika kufundishia. Kwa kung’ang’ania kutumia lugha wasiyoelewa, tunawafundisha wanafunzi hawa kushindwa! Wengi wa wanafunzi hawa wanajifunza kutodadisi, kutofikiri, kutouliza maswali, kunakili na kukariri, kuwa waoga, kutojiamini, kukubali kila hali, na kukata tamaa kwa kauli ya “yote maisha”. Kwa maana nyingine wanafunzi walio wengi katika shule na vyuo vya Tanzania hawapati elimu iliyokusudiwa, achilia mbali Elimukombozi, kwa kuwa uelewa wao wa lugha inayotumika kufundishia ni mdogo. Kwa hiyo, badala ya elimu yetu kutokomeza ujinga, inapalilia ujinga! Ni vema tukajiuliza, hali hii ya kuandaa vijana wasioweza kuelewa, kujadili, kufikiri, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbali mbali zinazofundishwa ni kwa maslahi ya nani? Ni wazi kwamba tunahitaji Elimukombozi; na kwamba ili kufanikisha Elimukombozi shuleni na vyuoni, ni lazima wanafunzi watumie lugha ambayo wao na walimu wao wana uelewa wa hali ya juu.


Jitihada za Serikali kubadili elimu mara baada ya uhuru hazijaendelezwa. Mwalimu Nyerere (1968) alisema kwamba, elimu inayotolewa haina budi kumchochea mtu kuwa na mambo matatu yafuatayo: akili zenye udadisi wa mambo, uwezo wa kujifunza kutokana na yale yanayofanywa na wengine, kujiamini kama mtu huru na aliye sawa na wengine katika jamii, mtu anayethamini na pia kuthaminiwa na wenzake kwa sababu ya matendo yake na siyo kwa kile alichonacho. Katika hali ambayo wanafunzi wana uelewa mdogo wa lugha, wanafunzi wa kike huathirika zaidi kwa kuwa mara nyingi huona aibu kuuliza, au kujibu maswali kwa kuogopa kuchekwa pindi watakapokosea lugha. Matumizi ya lugha wasiyoielewa vizuri huwafanya wanafunzi wengi, hasa wasichana, kuwa wanyonge, na kwa muda mwingi hunakili maadiko ya mwalimu (mengine yakiwa na makosa) kwa kadri watakavyoweza kuyasoma. Maandiko hayo kwa sehemu kubwa wengi hawayaelewi. Badala ya kujifunza masuala ya msingi, wanafunzi wanaishia kukariri maneno kwa lugha wasiyoelewa na muda mwingi unapotea na ari ya kusoma inapungua. Elimu hii ya kunakili na kukariri haiwapi uwezo wa kujikomboa bali huenda kinyume na makusudio. Badala yake huwafundisha kuwa: wavumilivu, wasikivu, na watii/watekeleza amri bila maswali. Yaani kuwa watumishi wazuri au watwana.


Hapa lugha inatumika kama kikwazo cha kuzuia wengi wasipate uelewa uliokusudiwa. Haya yalikuwa malengo ya elimu ya kikoloni; lakini kwa kujua au bila kujua tumekuwa tukiiendeleza hadi leo, miaka zaidi ya 56 baada ya Uhuru. Brock-Utne (1997) anapendekeza kwamba, ili kuleta mabadiliko kwenye mfumo wa elimu Afrika, hatuna budi kuwakomboa Waafrika kifikra; na kwamba hali hiyo itawezekana iwapo Waafrika watachukua mamlaka juu ya taratibu zinazotumika kuendesha elimu yao. Anasisitiza kwamba kuna haja ya kutunga upya vitabu vya

kiada vinavyotumiwa na wanafunzi shuleni ili viwe na mafunzo ya Kiafrika katika lugha za Kiafrika wanazoelewa wanafunzi hawa ili kuwaandaa wasomi kuwa wadadisi, wanaouliza maswali na kutafuta majibu ya matatizo yanayoikabili jamii. Wawe na uwezo wa kufikiri, kuchambua, kutafakari na kutumia taaluma walizojifunza shuleni na vyuoni kutatua matatizo ya jamii katika lugha zao. Obaro (1997) naye anakubaliana na Brock-Utne kwamba Waafrika sharti watambue umuhimu wa kubadili elimu wanayoitoa ya nchi za Magharibi ili badala yake watoe kwa watoto wao elimu ya Kiafrika. Tunahitaji kuwa na vitabu na vifaa vya kufundishia vinavyoendana kwa karibu na mahitaji na pia hali halisi ya jamii ya Kiafrika.

5.2 Elimukombozi na hali ya upashanaji habari katika jamii

Kwa kuwa lengo la elimu (MOEC 1995) ni kuwaandaa vijana kuwa sehemu ya jamii, ni vema maandalizi hayo yakafanywa katika lugha kuu ya jamii. Matumizi ya lugha moja katika elimu na jamii inaimarisha mahusiano kati ya jamii na shule au vyuo. Ili kuifanikisha Elimukombozi ifikie jamii kubwa zaidi nje ya shule na vyuo ni muhimu kutumia lugha ambayo sehemu kubwa ya jamii inaelewa. Katika hali tuliyorithi, ambapo elimu hutolewa kwa lugha ngeni katika jamii, upashanaji habari wa yale yanayotolewa katika elimu kuenea kwa jamii kubwa ni mgumu. Kwa mfano, hivi sasa maandiko mengi ya tafiti na taaluma mbali mbali katika bara la Afrika yako katika lugha za Kigeni: Kiingereza, Kifaransa, Kireno au Kiarabu. Ni vigumu, na wakati mwingine haiwezekani kabisa kwa maandiko haya kusomwa na wanajamii. Iwapo lugha ya elimu ni ile ile inayotumiwa na watu wengi katika jamii, kama ilivyo katika nchi za Ulaya na Asia, basi ujuzi na maarifa yanayopatikana katika elimu yangewafikia watu wengi katika jamii. Hali hii ingelipunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upashanaji habari, na lingenufaisha watu wengi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Kubadili lugha ya kufundishia ni hatua muhimu ya msingi katika kuboresha elimu; lakini peke yake haitoshi. Tunahitaji kubadilisha mtazamo wetu wa sasa kuwa chanya kuhusu uwezo wetu wa kutoa elimu yenye manufaa kwetu sisi. Tunahitaji kuyapitia upya malengo yetu ya elimu ili yaendane na Elimukombozi. Ili kuukabili utandawazi ni muhimu tuwe na uelewa wa kina wa mambo mbali mbali na tujifunze lugha kadhaa za kimataifa. Tushiriki katika utandawazi tukiwa binadamu wenye wajibu na haki kama binadamu wengine.


6.0 Hitimisho na Mapendekezo

Katika makala hii tumejadili hali halisi ya elimu inayotolewa katika jamii yetu. Ingawa msisitizo umekuwa kuwawezesha watoto/vijana wengi kadri iwezekanavyo kwenda shule, bado kuna umuhimu wa kutizama mbali zaidi na kujua nini kinachofanyika ndani ya darasa. Tumeona kwamba elimu tuliyorithi kwa wakoloni ya kuandaa watumishi na jamii ya watu wa kutawaliwa kirahisi bado tunaiendeleza. Lugha ya kufundishia kwa sehemu kubwa inatumiwa kama kikwazo cha kuzuia wengi wasipate uelewa uliokusudiwa. Ingawa tulidhamiria (Nyerere 1974) kuwa malengo ya msingi ya elimu ni kumkomboa binadamu, hali halisi inaonyesha kwamba yanayofanyika ni kinyume kabisa na ukombozi. Elimu yetu, miaka 56 baada ya uhuru, bado inaendeleza malengo yale yale ya wakoloni. Kwa maoni yangu, njia pekee ya haraka na uhakika ni kuangalia upya elimu yetu ili tuweze kujikomboa kifikra. Elimukombozi ni njia muafaka na ya lazima iwapo tutapenda kujikomboa. Changamoto iliyopo mbele yetu ni namna ya kuelezea dhana hii na kuifanya ikubalike miongoni mwa jamii hasa kwa wafanyamaamuzi. Ni vizuri tukatambua kuwa hii ni kazi ngumu, kwa maana mizizi ya upotofu wa elimu tuliyorithi kwa

wakoloni na kasumba za kujidharau na kuhusudu vya wengine imejikita sana miongoni mwetu.

Sisi tuliopo hapa, tukishirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na asasi zingine za kijamii tuna wajibu. Wajibu wa kuwa kichocheo cha mabadiliko. Tukumbuke kwamba, popote palipo na kukandamizwa, kuonewa, kunyimwa haki kwa aina yo yote; wanawake mara nyingi huathirika zaidi. Hata hivyo, pamoja na kuathirika zaidi, wanawake huwa ndiyo wenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika jamii.

Tushirikiane wake kwa waume, tujikomboe na tulete mabadiliko chanya katika jamii zetu na kwa ulimwengu mzima. Tujihadhari tusije tukatumia mbinu zile zile walizotumia wakoloni za kutugawa makundi zikaturudisha tulipoondokea. Tuwe na upendo, amani na mshikamano.

Angalizo: Kwa watakaoguswa na mada hii tuwasiliane ili tuweze kuisaidia jamii kupata elimu kombozi. Mimi ni Katibu wa NGO inayotambulika kwa jina la MWASENDA DEVELOPMENT INTERVENTION, (MDI). Ofisi Kuu, ziko Wilaya ya Ilemela - Nyasaka Centre - jijini Mwanza. Pia kwa wakazi wa Nzega tuko na ofisi Nkinga karibu na Hospitali. Tunakaribisha wadau wengine wilaya tofauti ili tufanye kazi wote.
 
Back
Top Bottom