Bujibuji,
Nilibahatika kuingia Muthaiga Club Nairobi mwaka wa 1989 na aliyeniiingiza ni Ally Sykes.
Mimi nilikuwa nakaa 680 Hotel nakaa hapo na vilevile ndipo ilipokuwa mahali nahudhuria mkutano.
Bwana Ally akawa anakuja Nairobi akanambia nikamuone Muthaiga Club kwani hapo ndiyo mafikizio yake kila akija Nairobi.
Mimi nilikuwa siijui Muthaiga Club wala sijapata kuisikia hata siku moja.
Baada ya kumaliza mkutano na kiza kilikuwa kinaanza kuingia nikashuka chini nikachukua taxi ya Mkikuyu mmoja nikamwambia anipeleke Muthaiaga Club.
Jamaa akaniuliza, ''Unakwenda Muthaiga Club?''
Nikamjibu ndiyo.
''Unafata nini Muthaiga Club?''
Hapa nikapigwa na mshangao kidogo kwa swali lile kwani taxi driver ukimfahamisha unapokwenda sana sana atakuuliza sehemu unayokwenda kama yeye haujui vyema lakini hakuulizi unakwenda Gymkhana Club kufanya nini.
''Baba yangu anakaa Muthaiga Club,'' nilimjibu.
''Baba yako anakaa Muthaiga Club?''
Mkikuyu akaniuliza kwa mshangao.
Nikamjibu kuwa hapo ndipo anapofikia kila akija Nairobi.
''Hii mutu ya Tanzania bwana kubwa!''
Mkikuyu sasa anajaza ''dots'' mwenyewe.
Nilipofika Muthaiga ndipo nilipojua kwa nini Mkikuyu yule alishangaa kuona kitoto kidogo kama mimi kinakwenda Muthaiga Club.
Muthaiga Club wanachama Waafrika huwaoni wote Wazungu tena wazee wamepinda migongo na wote mamilionea.
Ukimuona Mwafrika mle ndani jua mtumishi.
Malipo yote hapo unaweka sahihi hakuna kulipa fedha taslimu.
Ukiomba unachama unafanyiwa mahojiano na wanataka kukujua nje ndani, ndani nje.
Unafuata nini katika club.
Unasoma vitabu?
Unapenda kuangalia filamu na zipi?
Lukuki ya maswali wanataka ujibu.
Wenyewe wanasema wanachukia mtu awe mwanachama na aje club kunywa pombe kisha anaondoka.
Wanataka mwanachama akifika club anaingia maktaba kuangalia vitabu vipya na kuazima kwenda kusoma.
Lakini hii yote babaisha ubaguzi umewaelemea hawataki watu katika club yao.
Yapo mengi na haya mengi alikujanieleza Peter Colmore nilipomhoji kuhusu Muthaiga Club.
Peter Colmore ndiye aliyemdhamini Ally Sykes kuwa mwanachama mwaka wa 1967.
Nishamweleza sana huyu mtu Colmore hapa.
Mtafuteni.
Huwezi kuamini.
Gavana wa Kenya wakati wa ukoloni anaomba uanachama na anaweza kukataliwa kuwa mwanachama wa Muthaiga Club.
Gavana hana hela.
Ukitaka kuijua nguvu ya "Capitalism," fika Muthaiga Club Nairobi.
Lakini kubwa ni kuwa ukishafanikiwa kuwa mwanachama wa Muthaiga Club basi ni kuwa tayari ushaunganishwa na club nyingine kama hizo kwingi ulimwenguni.
Fursa ikitokea nitakupa kisa cha Ally Sykes na genge la Roy Wellensky wa Rhodesia pale Wellensky na wenzake walipomuona Ally Sykes Harare Club wakamtolea ufedhuli kwani hawakupatapo wao kumuona mwanachama Mwafrika ndani ya club ile ila waiter, mhudumu wamemvisha unifomu inayowapendeza wao wakimtuma kwa dharau.
Rhodesia ilikuwa Zimbabwe na Salsibury ni Harare na nchi iko huru na Robert Mugabe ndiye rais lakini Wazungu hawataki kuamini.
Tuje kwenye Saigon Club.
Ally Sykes alikuwa mwanachama.
Wewe ndugu yangu Bujibuji unataka kuwa mwanachama lakini hata kabla hujawa mwanachama unatukebehi ati Saigon ndiyo tunaamua nani awe rais wa Tanzania.
Leo unauliza ufanye nini uwe mwanachama wa chama chenye nguvu ya kuunda serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwani ukitaka kuwa mwanachama wa CCM, Yanga au Simba mtu anafanya nini?
PICHA:
Picha ya kwanza Ally Sykes na M-wandishi Muthaiga Club 1989 na ya pili Ally Sykes wa kwanza kulia, Sheikk Issa Ausi, na wa mwisho Juma Abeid (Spencer) wakiwa kwenye Khitma ya Saigon 2010,
View attachment 1871567
View attachment 1871573