Eti! Nchi ilibebeshwa mimba na mafisadi ! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Eti! Nchi ilibebeshwa mimba na mafisadi !

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by leseiyo, Jan 15, 2009.

 1. leseiyo

  leseiyo Senior Member

  #1
  Jan 15, 2009
  Joined: Oct 25, 2007
  Messages: 116
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  NCHI IMEBEBA MIMBA BILA KUTARAJI,TUKO TAYARI KUMPOKEA MTOTO?
  Kubeba mimba kulingana na maana inayotolewa na mtandao wa ‘wordnet home page’ kuna maanisha kubeba mbegu ya uhai au kuwa katika hali ya kutaraji kuzaa kitu chenye uhai.
  Mimba humaanisha hali ya kutaraji na mara zote inapotokea kwenye familia na jamii zetu basi wazazi husika hufanya matayarisho mbalimbali ili kujiandaa na namna ambavyo kiumbe kipya kitapokelewa na kulelewa kwenye ulimwengu wake mpya. Wazazi husika hununua nepi, huandaa fungu la fedha litakalotumika kumhudumia mtoto pindi pale mahitaji yatakapotokea. Kwa maana nyingine mtoto mtarajiwa huongeza bajeti ya nyumba husika.
  Nchi ya Tanzania kwa hivi sasa iko katika iko katika hali ya kuumwa, ina maradhi na maradhi hayo ni kuwa imebeba mimba. Tanzania iko katika kipindi kigumu cha kulea ‘ujauzito’lakini ‘ujauzito’ au ‘mimba’ si hali ya kuiogopa, kama tukiangalia maana ya kwenye ‘Wordnet home page’ mimba ni ishara ya neema, ni ishara ya mbegu ya uhai inataka kuzaliwa, kwa hiyo watanzania wangetakiwa waifurahie mimba hii katika hali ya kawaida. Lakini kinyume na matarajio, watanzania wako katika hali ya wasiwasi na hofu, kwasababu, mimba iliyobebwa na ‘nchi’ ni mimba iliyoingia bila kutaraji au kwa bahati mbaya, mimba imeingia katika kipindi ambacho ‘wazazi’ (watanzania) wakiwa katika hali ngumu kiuchumi na kimawazo. Watanzania wako katika ukata mkubwa sana wa kimaisha, migogoro ya kifamilia na misongo ya kimawazo kutokana na kukabiliwa na mambo makubwa ya kuyatatua kuliko uwezo wake.
  Dalili za nchi kuwa na mimba zinaonekana kila mahali, mishahara ya wafanyakazi na watendaji muhimu wa serikali iko chini kupita kiasi, mazingira ya kufanya kazi yanakatisha tamaa, bei za vitu zinapanda kiholela, mashirika ya serikali yanakufa kwa uzembe, ufisadi umeenea kila pembe ya nchi, watoto wanakomaa kabla ya umri wao, uongozi wa kisanii na ahadi za uongo uongo zimegeuka fasheni na mbaya zaidi ubinadamu umepotea.
  Kwa kawaida mimba inapopatikana kwa njia isiyo halali ‘mbebaji’ hujitahidi kuficha dalili zisionekane kwenye jamii kwani ni kitendo cha aibu lakini kwa Tanzania hali ni tofauti dalili ziko waziwazi na walioijaza nchi mimba wanatamba na kukenua meno kila kukicha. Suala la ufisadi limekuwa ni tatizo sugu katika nchi yetu na mafisadi ndio wanaoamua kila kitu na kila maamuzi muhimu ya nchi.
  Mfano kulingana na taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Ludovick Utuoh alizozitoa kwenye gazeti moja la kila siku alisema serikali inakabiliwa na tatizo la matumizi makubwa kuliko makusanyo.
  Ripoti ya Bw. Utuoh kuhusu mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2007 imesema kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Sh. bilioni 254 ikiwa ni zaidi ya malengo iliyojiwekea ya kukusanya Sh. bilioni 241. hata hivyo kulingana na mkaguzi mkuu wa serikali matumizi ya serikali yamekuwa yakiongezeka maradufu kuliko kiasi kinachokusanywa.

  Mkaguzi mkuu alibainisha katika ripoti yake kuwa watumishi wasio waaminifu hutumia mbinu kama vile; manunuzi mabovu, matumizi ya magari, hususan matengenezo na mafuta, ununuaji wa samani, safari za kikazi, semina na warsha mbalimbali kujinufaisha binafsi na hakuna kanuni au sera inayoonyesha viwango vya samani ama magari ambayo ofisa wa serikali anatakuwa kununua na hivyo kila mmoja anaweza kutaka samani yoyote inayomfurahisha.
  Wakati ukosefu huu wa kanuni na sera za kusimamia matumizi serikalini ukiwanufaisha viongozi mafisadi, watendaji wakubwa na muhimu kama vile walimu, madaktari, mainjinia, mahakimu wa mahakama za wilaya na za mwanzo, manesi, wanajeshi, polisi, wakulima wadogo wadogo na watendaji wengine muhimu kwa maendeleo ya taifa wanazidi kuteseka na kuishi katika manung’uniko makubwa. Mi naita kuishi huku ukiwa umekwisha kufa.
  Mayo; mwanzilishi wa nadharia ya ‘mahusiano ya binadamu’ anataja malipo mazuri na mazingira ya kuridhisha ya kazi kama vitu muhimu sana katika kumhamasisha mfanyakazi kufanya kazi kwa moyo na kwa bidii. Na anawataka waajiri wahakikishe kwa uwezo wao wote wanatengeneza mazingira bora kwa wafanyakazi wao ili kuwazuia na vitendo vya ubadhirifu. Lakini hii ni tofauti na Tanzania ambapo katika mazingira ya kazini kuna matatizo mengi.
  Serikali inaonekana kuwa na mipango mingi na mizuri ya kuyaboresha Maisha ya wafanyakazi lakini utekelezaji umekuwa haba.
  Akiwasilisha mada kuhusu ‘ Umuhimu wa maboresho ya malipo ya huduma za jamii ili kupunguza rushwa kwa watumishi wa Serikali Tanzania’ tarehe 26/5/2005 mshauri wa sera na ufundi katika ofisi ya seriakali huduma za jamii, bwana Gelase Mutahaba, alikiri kuwepo kwa udhaifu mkubwa katika suala zima la ulipaji serikalini ambalo alikiri kuwa ni chanzo kikubwa cha rushwa na uzembe makazini.
  Bwana Mutahaba alitoa ahadi kuwa Serikali iko katika kukagua utekelezaji wa ‘mkakati wa maboresho ya malipo ya kati’ wa mwaka 1999 ulilenga kuboresha maslahi katika maeneo ambayo Serikali ilikuwa ikipata ushindani mkubwa kupata wafanyakazi wataalamu wa sekta mbalimbali.
  Sekta kama za afya zikihusisha madaktari bingwa, na sekta nyingine muhimu zinazohusisha mainjinia, maprofesa wanaofanya kazi kama wahadhiri vyuoni, wataalamu wa miamba, wataalamu wa kuchanganya madawa na wengineo ziliainishwa katika mkakati huo kama ni sehemu zilizohitajika kupitiwa kwa makini.
  Lakini ukiachilia mbali juhudi ndogo zilizofanyika inaonekana bado kuna matatizo mengi ya kutolewa macho na matatizo hayo yote yanasababishwa na baadhi ya viongozi wachache wenye nafasi muhimu kwenye sekta za serikali.
  Matokeo ya hili ni kuwa sekta muhimu kwa maisha ya watanzania zinajiendesha kiholela na kila mtu anaamua anachokitaka.
  Akitoa taarifa wakati akizundua kamati maalum ya kitaifa ya kusimamia kemikali hivi karibuni, katibu mkuu wizara ya afya na ustawi wa jamii, Bw. Wilson Mukama alisema, “Asilimia 98 ya dawa zinazotakiwa kuthibitishwa ubora wake kabla ya kuingia sokoni zimebainika kuwa na kemikali hatari za sumu zinazochangia kusababisha madhara makubwa kiafya.
  Tukiangalia kitendo cha baadhi ya wajanja kughushi malipo hewa ya takribani bilioni 3 na zaidi ya walimu wasiokuwepo huku walimu wenyewe wakitaka kuandamana kwa matatizo yahusianayo malipo kidogo yasiyokuwa na tija inaonesha ni kwa kiasi gani mimba imekuwa kubwa.
  Mishahara ni midogo kupita kiasi na mazingira ya kazi ni magumu kupindukia, hivi majuzi kulikuwa na mgomo shirika la reli uliokuwa ukipinga mishahara midogo, mgogoro ambao ulipoteza wakati mwingi na nguvu huku tatizo la mgogoro huo likiwa limesababishwa na mkataba mbovu ulioingiwa baina ya serikali na kampuni ya Rites ya India.
  Akiuzungumzia mkataba huo mwandishi wa makala katika gazeti la Rai bwana; Abdulwakil S. Saiboko anasema, “Kinachoiponza serikali ni masharti magumu yaliyopo kwenye mkataba huo yanayoitaka serikali kukodisha injini 25 za treni na serikali kuwajibika na gharama zote za matengenezo ikiwa zimeshindwa kutengenezwa hapa nchini na kwa makadirio gharama za kusafirishia injini zote 25 ni 1,025,000,000 na mkataba huo ukiisha injini zinarudishwa India kwa gharama za serikali”
  Kitu kinachoshangaza zaidi baada ya baadhi ya wafanyakazi wa reli kuhojiwa ni kuwa injini zilizokodiwa zimeonesha kuwa na uwezo mdogo sana wa kufanya kazi. Mikataba mingine kama vile Richmond na IPTL imelalamikiwa vya kutosha na wananchi na athari zake zimeshaonekana kwa wazi kabisa lakini ukiachilia mbali ahadi, walioiingiza nchi kwenye mikataba hewa hiyo wanaonekana wakitembea kifua mbele mitaani.
  Akitoa malalamiko yake kuhusu matukio ya ufisadi na kuongezeka kwa hali ngumu ya maisha, ustaadhi mmoja aliyeguswa sana na matukio haya aliyejitambulisha kwa jina la Saidi Ngamba alisema, “ Binafsi nasikitishwa sana na hali ya nchi ilivyo inaonekana kama vile kuiba si tatizo kabisa, ila tatizo umeiba kiasi gani?’
  “..Kama mtu ameiba mabilioni (vijisenti) ya shilingi na kuyaweka kwenye akaunti za nje ili siku ikilipuka vita apate urahisi wa kukimbia na kwenda kuzitumbua kwa uwazi, mtu huyo anasamehewa lakini mtu akivunja au kuiba shilingi mia mbili mtu huyo anafungwa miaka 30 na kazi ngumu. Halafu mafisadi hawa wanaonekana wakitoa sadaka na misaada mbalimbali makanisani na misikitini. Hali kama hii ina mwisho mbaya” aliendelea kusema Ustadhi huyo.
  Sakata kama la Benki kuu, shirika la reli, ununuzi wa kiholela wa rada, mikataba feki ya madini, imeifanya Tanzania kushindwa kuwalipa vyema na kuwajali wananchi na watendaji wake wa chini na hatimaye ari ya ufanyaji wakazi kwa watendaji imepungua na watu wanaishi alimradi.
  Mfano, Kaimu Mkuu wa chuo kimoja cha maendeleo ya jamii na ufundi cha Misungwi, bwana Christiani Kimario aliilalamikia serikali kuwa wanafunzi wanakimbia chuoni kwake kutokana na upungufu wa watumishi na mazingira magumu. chuo hicho chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kilikuwa na wanafunzi 14 tu hadi Agosti 31 2007.
  Wasomi na wataalamu wetu wanakimbia kwenda nje kufuata maslahi na kuacha nchi katika ndoto alinacha za kupata maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia na hii ni kwa sababu watawala na wanasiasa wetu wanakula kupita kiasi. wanausahau msemo wa kiswahili unaosema “Ngedere anapopokonywa chakula chake, hupewa maganda ya ndizi ili kumdanganyia” wanasiasa wetu wanakula kuanzia ‘chakula’ hadi maganda ya ‘ndizi’.
  Wizi na ulafi wa watu wachache wasio kuwa na uchungu wa nchi hii umesababisha machafuko sehemu zote na hata wale waadilifu waliokuwepo wamegeuka wezi. Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu cha Dar es salaam aliwahi kusema kwenye maandamano ya wanafunzi kupinga ufisadi pale Jangwani.
  “Huwezi kuniambia katika hali ngumu kama hii ya bei ya vitu kuwa juu, mtu anapokea mshahara shilingi elfu themanini, ana watoto anasomesha, amepanga nyumba, anataka kula na kuvaa halafu mtu huyo anaweza kumudu familia, mtu huyo lazima atakuwa mwizi inabidi akamatwe apelekwe mahakamani” Alisema mwanafunzi huyo
  Mimi nasema kuna namna mbili za kuweza kuishi Tanzania ‘kuiba ili uishi timamu au kuishi ukiwa chizi freshi kwa mishahara na mazingira ya kazi ya kitanzania’.
  Nchi ya Tanzania kulingana na takwimu za kituo cha utafiti wa umaskini uliokithiri cha umoja wa mataifa ilikadiriwa kuwa ni nchi ya nane kutoka mwisho kwa umaskini. Lakini inaonekana ni nchi yenye matumizi makubwa kuliko inachokipata.huku matumizi hayo yakiwa hayamgusi moja kwa moja mtu wa kawaida anayelipa kodi. Swali ni je hawa ‘mabwana wakubwa wanaovuna wasichokipanda’ wanazipata wapi hizi fedha?
  Kila mahali sasa kuna wasiwasi, mimba za mashuleni zimeongezeka, watoto wetu wa kike wanakuwa wakinamama kabla ya umri wao, vichaa wanaotokana na hali ngumu wameenea na mafisadi wanazidi kunenepeana.
  Swali ni Je hii mimba itakapotimu muda wa kutoa mtoto watanzania halafu baba wa mtoto akiwa amekimbilia nje kutumbua ‘mihela’ na kutuachia mtoto, tuko tayari kumpokea mtoto?
   
Loading...