nankumene
JF-Expert Member
- Nov 12, 2015
- 7,340
- 8,127
Ethiopia Airlines ndiyo ya kwanza Afrika kununua ndege aina ya Airbus A350 XWB
Ethiopia imekuwa taifa la kwanza barani Afrika kununua ndege ya kisasa aina ya Airbus A350 XWB.Ndege hiyo, Airbus A350, ndiyo ya hivi karibuni kuzinduliwa na kampuni ya ndege ya Airbus ya Ufaransa.
Ndege hiyo, iliyo na uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 300, ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Kenya Jumatano jioni ikitokea mjini Addis Ababa, Ethiopia.
"Ndege hii ya kisasa itasaidia katika utoaji wa huduma zetu, kuimarisha mtandao wetu wa usafiri, na kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya hewa chafu inayotolewa wakati wa usafiri wa ndege,” Mkurugenzi mkuu wa shirika la Ethiopian Airlines Tewolde GebreMariam amesema.
Ndege hiyo ni ya kwanza kuwasilishwa kwa kampuni hiyo, huku nyingine 13 ilizoagiza kutoka kwa kampuni ya Airbus zikisubiriwa hivi karibuni.
Safari ya kwanza ya ndege hiyo ilifanyika tarehe 2 Julai iliposafiri kutoka Ufaransa hadi mjini Lagos, Nigeria.
Viwango vya juu vya teknolojia iliyotumika kuunda ndege hiyo, vinachangia katika kuinua utendakazi wake, kupunguza matumizi ya mafuta pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafu.
Kampuni ya Ethiopian Airlines inaorodheshwa ya kwanza barani Afrika kwa faida na pia idadi ya maeneo inayosafirisha abiria.
Mwaka wa 2012, shirika hilo pia lilikuwa la pili duniani na la kwanza barani afrika kununua ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner, ya kampuni ya Boeing, yenye afisi zake kuu Chicago, Marekani.
Kampuni ya Airbus na Boeing zinaongoza duniani katika utengenezaji wa ndege za kisasa, japo Airbus ina umaarufu mkubwa na imeipiku Boeing kwa faida na uuzaji wa idadi kubwa ya ndege.
Chanzo: BBC swahili