Dunia yaifungulia tena milango Zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dunia yaifungulia tena milango Zanzibar

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by abdulahsaf, Mar 8, 2011.

 1. a

  abdulahsaf JF-Expert Member

  #1
  Mar 8, 2011
  Joined: Aug 31, 2010
  Messages: 859
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0  Written by administrator // 07/03/2011 // Habari, Sauti // 10 Comments

  [​IMG]
  • Asema afya yake sasa ni poa kabisa
  • Kurejea Zanzibar kwa kishindo
  Na Salma Said,
  Ziara ya Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mataifa ya Ulaya na Uarabuni, imeelezwa kuwa ya mafanikio makubwa na ya matumaini mema kwa maendeleo ya taifa zima. Hayo yameelezwa na Maalim Seif mwenyewe alipoongea na vyombo mbalimbali vya habari mapema jana, akiwa nchini India, anakoendelea na matibabu.
  Mahojiano na M.Seif kupitia idhaa ya DW:

  Maalim Seif ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na ziara hiyo iliyodumu kwa takriban mwezi mmoja hadi sasa. Alisema mataifa ya Falme za Kiarabu (UAE) na yale ya Ulaya, ikiwamo nchi ya Uholanzi, wameahidi kukuza uhusiano mwema na kiwango cha misaada yao kwa Zanzibar .
  “Ziara imekuwa ya faraja kubwa na ya matumaini ambayo bila shaka itakuwa ni hatua muhimu kwa maendeleo ya nchi na watu wote,” alisema Maalim Seif.
  Ziara hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwezi uliopita mjini The Hague, Uholanzi, ilimkutanisha Maalim Seif na viongozi wa Jumuiya ya Watu na Mataifa Wasiowakilishwa katika Umoja wa Mataifa (UNPO), ambako alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 20 ya Jumuiya hiyo. Zanzibar, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), imekuwa mwanachama wa UNPO kwa kipindi cha miaka 20, na Maalim Seif amewahi kuwa raisi wa Jumuiya hiyo kwa vipindi viwili mfululizo.
  Hata hivyo, kutokana na sasa chama chake kuwa miongoni mwa vyama vinavyoongoza serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, CUF, kimsingi, haiwezi tena kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo. Akiwa nchini Uholanzi, Makamo huyo wa Kwanza wa Rais alikutana pia na watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, kuzungumzia haja ya kuendeleza misaada katika sekta mbali mbali, ikiwamo ile ya afya visiwani Zanzibar, ambayo inafadhiliwa sasa na Uholanzi.
  Huko Maalim Seif na ujumbe wake ukihusisha watendaji kutoka Wizara ihusikayo na Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Wizara ya Fedha na watendaji wakuu wa sekta mbali mbali nchini, aliweza pia kushuhudia Maonyesho maalumu ya kibiashara nchini Uholanzi, ambapo ujumbe huo uliondoka na changamoto muhimu kupitia sekta za biashara na uzalishaji. Maalim Seif na ujumbe wake walifika katika Mataifa ya Falme za Kiarabu, UAE, ikiwamo Dubai, Sharjah, na Oman, ambako walipokelewa kwa mikono miwili.
  Huko waliweza kukutana na Baraza la Wafanyabiashara na Wazalishaji (Chamber of Commerce) walioeleza imani kubwa ya kushikamana na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wazalishaji ya Zanzibar (ZNCCIA) ili kuleta msukumo wa kiuchumi kati ya pande husika zenye mshikamano wa asili ambao ulitetereka kutokana na suitafahamu ya kisiasa katika visiwa vya Unguja na Pemba miaka kadhaa iliyopita. “Walichoahidi ni kurejea tena kuitambua Zanzibar kama awali kwani kipindi kilichopita cha mizozo wanasema walihofia kuambiwa wanaingia mambo ya nchi za watu”, alifafanua Maalim Seif juu ya msimamo huo wa sasa wa Mataifa ya Falme za Kiarabu, kwa Zanzibar .
  Ujumbe wa Maalim Seif uliweza kutembelea Mji wa Vyuo Vikuu vya UAE, ambako walipokelewa na kuifungua milango muhimu ya uhusiano wa kitaaluma katika ngazi za elimu ya juu, ambapo fursa imetolewa ya mshikamano baina ya vyuo vikuu nchini na vile vya Uarabuni, licha ya ahadi za nafasi za masomo. Pamoja na ziara hiyo kukamilika rasmi, Maalim Seif alirejea nchini India, kwa ajili ya matibabu, kama alivyoahidiwa na madaktari wa huko, alipozuru kabla mnamo Februari, 2010. Baada ya uchunguzi wa takriban siku 2, Maalim Seif alilazimika kufanyiwa upasuaji wa magoti yake mawili, baada ya kubainika haja ya kufanya hivyo, ingawa sasa hali yake ni bukheri wa afya.
  “Walinifanyia uchunguzi na wakasema nifanyiwe upasuaji wa magoti wakaniweka ICU siku moja siku ya pili wakataka nifanye mazoezi nikatembea kwa miguu yangu na sasa niko vizuri Alhamdulillahi nalazimika kuzidi kufanya mazoezi”, alibainisha Maalim Seif.
  Maalim Seif ameeleza shukurani zake za dhati kwa wananchi wote waliomuombea dua katika matibabu hayo na safari ya ujumbe wake kwa ujumla.
  Alipoulizwa ni lini anatarajia kurejea nchini, Maalim Seif alisema “siku yoyote kuanzia sasa nasubiri na sitaki nije kufikia kitandani bali kuendelea na kazi kama kawaida”. Wananchi na Serikali kwa ujumla wanamsubiri kwa hamu kubwa kiongozi huyo ambaye amekuwa akileta hamasa kubwa ya utendaji na utekelezaji wa majukumu tangu kuja kwa mfumo wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
   
Loading...