Aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa OAU na waziri mkuu wa Tanzania Dr Salim A. Salim ametaka haki itendeke Zanzibar kwa kumtangaza mshindi wa uchaguzi na si kurudia uchaguzi kama ilivyotangazwa na ZEC. Amesema tangazo hilo limeishutua dunia.
=======================
=======================
Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ameshangazwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi visiwani humo.
Amesema jumuiya za kimatifa zilishtushwa na uamuzi huo.Salim amesema kutokana na hali hiyo, kinachotakiwa hivi sasa ni haki itendeke kwa kila kila upande kukaa na kutafuta suluhisho la kudumu.
“Tanzania haijazoea migogoro ya siasa jambo ambalo si jema katika sura ya kimataifa,” alisema.
Mwanadiplomasia huyo wa kimataifa ametoa kauli hiyo,baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana.
Siku chache zilizopita, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa Machi 20 mwaka huu.
Mwanadiplomasia huyo wa kimataifa aliwahi kushika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa inatambulika kama Umoja wa Afrika (AU).
Alisema hatua ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar ni jambo lililowashangaza wengi kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku waangalizi wa ndani na nje wakiusifia katika ripoti zao.
“Ni hatua ambayo imewashangaza wengi…imeibua sintofahamu kubwa katika nchi yetu kwa sababu uchaguzi uliopita Tanzania ilipata sifa,baada ya uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu. Lakini kitendo cha kufutwa kumewashangaza wengi na bado suala hili halieleweki.
“Pia hili jambo sidhani kama ni la mtu mmoja…sidhani kama ni la Jecha peke yake. Huu si mustakabali mzuri kabisa, Zanzibar ni nchi ndogo, lakini ina historia kubwa kisiasa hivyo juhudi za pamoja zifanyike kutatua mgogoro huu kwa matakwa ya Watanzania kwa ujumla.
“Viongozi wasisitize amani na utulivu na katika hili la Zanzibar kwa kweli haki itendeke na waache ushabiki wa vyama iwe CCM au Upinzani, wote waweke ushabiki pembeni na watatue mgogoro huu kwa mustakabali wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla,” alisema Dk. Salim.
Alisema ingawa viongozi mbalimbali wamekutana na kufanya mazungumzo bila kupata suluhu,pande zote ziendelee kukutana hadi suluhu ya pamoja ipatikane.
Salim, alisema kuendelea kuachia hali hiyo iendelee kuna hatari ya kujenga uhasama zaidi hivyo ni vema viongozi wafikirie zaidi masilahi ya Zanzibar.
“Nchi ipo katika hali mbaya, migogoro iko kila pahala,Watanzania hatujazoea. Jambo hili la Zanzibar likiendelea litazaa matatizo makubwa katika Taifa letu.
“Waliangalie kwa uzito hata kama tarehe ya uchaguzi imetangazwa waendelee na mazungumzo,” alisema mwadiplomasia huyo wa kimataifa.
Dk. Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipoulizwa kama Kamati Kuu ya chama tawala katika vikao vyake ilijadili suala la Zanzibar, alisema limegusiwa ingawa haikuzungumzwa na ni nini kifanyike.
“…japo sikushiriki vikao vyote hivi karibuni kwa sababu nilikuwa katika majukumu mengine, jambo hili limezungumzwa japo halikugusiwa nini kifanyike.
“Jambo hili, linastahili kupewa kipaumbele hata katika vikao vya Kamati ya Kuu ya CUF (Chama cha Wananchi) na vyama vingine kwa sababu madhara yakitokea yataathiri kila upande,” alisema.
Chanzo: Mtanzania