Diwani Mbeya afichua ufisadi michango ya shule

engmtolera

JF-Expert Member
Oct 21, 2010
5,150
1,437
WANANCHI wa Kata ya Mwakibete jijini Mbeya wamekuja na ufumbuzi wa michango kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari, lakini Mkuu wa Wilaya hiyo, Evans Balama, anawaona ni wapinga maendeleo, kisa wanachangishana 3,000/= badala ya 10,000/= anazozitaka yeye.

Kamati ya Maendeleo ya Kata (KAMAKA) hiyo ya Mwakibete ikiwa chini ya uongozi wa Diwani Lucas Mwampiki kutoka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) iliamua kiwango cha mchango kiwe 3,000/= kufanikisha ujenzi wa vyumba saba vya madarasa katika shule yao ya sekondari badala ya kiwango kilichozoeleka cha 10,000/=.

Msingi wa hoja ya KAMAKA inajengwa na ukweli kwamba kiwango cha 10,000/= kilikuwa kikilalamikiwa sana na wananchi kwamba hakina ufanisi, kwa maana thamani ya fedha kutonekana kwenye kazi, kwamba hakikukusanywa kwa ufanisi na hata makusanyo yake halisi hayakufahamika.

Wananchi wanaiona michango hiyo kama sehemu ya mradi wa viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi wilayani, kujikusanyia mapato kwa kisingizo cha ujenzi wa shule.

Hesabu ya Kamati hiyo ya Maendeleo Kata ya Mwakibete ni rahisi sana, wamechukua idadi ya wakazi wenye uwezo wa kuchangia wakazidisha na shilingi elfu tatu wakapata shilingi milioni 22.5 ambazo wanasema zinawatosha kujenga vyumba saba vya madarasa, kila chumba kikigharimu shilingi milioni tatu ambayo ndiyo inayoelekezwa na serikali.

Pamoja na hesabu kuonyesha kuwa fedha hizo zinatosha, bado Kamati hiyo iliweka angalizo na kukubaliana na wananchi wake kwamba iwapo patakuwapo na mapungufu basi watakaa tena na wananchi kupanga kiasi gani wachangie kulingana na mahitaji yatakayojitokeza.

“Tukianza na shilingi elfu tatu tunaangalia impact yake. Tunalinganisha na gharama halisi, iwapo hazitoshi tunakaa tena na wananchi kuangalia kiasi kinachopungua tunachangia tena. Wananchi walikata tamaa, kupunguza ni kuwa motivate waone kile kidogo walichochangia kimefanya kazi. Itawahamasisha zaidi,” anasema Diwani Mwampiki.

Anaongeza Mwampiki: “Wananchi wanapenda kuchangia maendeleo. Wanakatishwa tamaa na sisi viongozi kwa kutokuwa wawazi kwenye masuala yanayohusu michango yao.”

Mwalimu wa shule moja ya sekondari jijini Mbeya ameiambia Raia Mwema kwamba wananchi hao wa Kata ya Mwakibete wamekabiliana na tatizo la ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa uhalisia zaidi kuliko msukumo wa kisiasa ambao hutoa mwanya kwa wajanja wachache kujinufaisha na michango hiyo.

“Jambo la msingi hapa ni vyumba kujengwa. Hawa wananchi wametumia busara zaidi, wamepiga hesabu wakaona shilingi elfu tatu inatosha kukamilisha vyumba wanavyovihitaji, na impact yake inaonekana, hata ikifeli ni wazi watakuwa na moyo wa kuchanga zaidi kwani kazi inaonekana,” anasema mwalimu huyo na anaongeza:

“Watu wamehamasika. Kazi inaponekana wanahamasika zaidi. Ile michango ya 10,000/= wananchi hawakuona kazi yake na wala kupewa mrejesho. Naona diwani amehamasisha vema. Watu walishajenga mtazamo hasi na hii michango.”

Utaratibu wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kama unavyoelekezwa na Mpango wa Maendeleo ya Shule za Sekondari nchini ni kwamba wananchi wanajenga maboma hadi kiwango cha lenta au ring beam na serikali inamalizia.

Hadi Machi 05, mwaka huu wananchi wa Kata hiyo ya Mwakibete, kwa michango yao hiyo hiyo ya 3,000/ walikuwa wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu na sita vikiwa katika hatua mbalimbali. Miongoni mwa vyumba hivyo tisa, vyumba saba vinajengwa kwa nguvu za wananchi huku viwili vikijengwa kwa michango ya wazazi wenye watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shuleni hapo.

“Watu wameitikia sana. Nina mitaa saba katika Kata yangu. Kila mtaa unajenga chumba kimoja. Kuna mitaa wamefikia kwenye lenta wanasubiri mchango wa Serikali,” anasema Diwani Mwampiki.

Wananchi wanahoji, iwapo Kamati ya Maendeleo ya Kata ndiyo yenye kusimamia ujenzi na iliyo karibu zaidi na wananchi, iweje Mkuu wa Wilaya ang’ang’anie 10,000/=, analenga kumnufaisha nani, na wanahoji zaidi uharaka wake kwamba kwa nini asisubiri matokeo ya kiwango walichokubaliana cha 3,000/= iwapo kina ufanisi au la?

Mkuu wa Wilaya hiyo alifika kuonana na Kamati ya Maendeleo ya Kata hiyo na kuishutumu kwa hatua yake hiyo huku akidaiwa kumtishia Diwani Mwampiki kwamba anao uwezo wa kumfanya lolote kwa kuwatumia Usalama wa Taifa na kutamba kuhusu ukada wake kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Diwani Mwampiki anaweka wazi vitisho hivyo katika barua yake ya malalamiko aliyomwandikia Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, akimnukuu Mkuu wa Wilaya akisema:

“Nina uwezo wa kukufanyia kitu chochote na jambo lolote kwa kuwatumia Usalama wa Taifa ili kukuondoa katika nafasi hiyo ya udiwani, japokuwa kufanya hivyo ni dhambi mbele za Mungu lakini nitamuomba Mungu anisamehe,” kisha katika barua hiyo Mwampiki anaendelea kumnukuu DC Balama akisema:

“Mimi nimezaliwa ndani ya CCM, nimekulia ndani ya CCM, nimesomea ndani ya CCM, ninafanya kazi ndani ya CCM, hivyo sitakuwa tayari kuona vyama
uchwara na sera zake uchwara ndani ya mamlaka yangu.”

Diwani Mwampiki hakuishia kumwandikia Meya wake tu bali amewapelekea nakala ya barua yake hiyo, ya Desemba 30, 2010 (nakala tunayo), viongozi kadhaa mkoani Mbeya wakiwemo, Mkuu wa Mkoa, Afisa Usalama Mkoa, Kamanda Polisi Mkoa, Katibu Mkuu CHADEMA Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini, Katibu CHADEMA (W) na Mkuu wa Wilaya mwenyewe.

“Nawasilisha kwako ili Ofisi yako ilione hili pia ipate ufafanuzi wa kauli hatarishi na za kiimla kama hizi. Katika zama hizi za utawala bora ambao naamini Serikali anayoitumikia yeye ni muumini wa dhana hii ya utawala bora, je, hayo ndiyo matumizi ya Uslama wa Taifa,?” anahoji Diwani Mwampiki kwenye barua yake hiyo kwa Meya Jiji la Mbeya.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya hakanushi madai hayo ya kumtishia diwani huyo, zaidi anasisitiza kwa kuwaelezea wapinzani wa michango ya 10,000/= kuwa ni wahuni, wapinga maendeleo na wavunja sheria za nchi, kwake thamani ya kazi si jambo la msingi.

“Hao ni wahuni, wapinga maendeleo, michango imepitishwa kisheria, ipo kwa mujibu wa sheria za Jiji, walipitisha 10,000/= . Huyo anayesema ufanisi wa 3,000/= nani huyo. Kama unataka kubadilisha sheria unafuata taratibu za kisheria zilizopo. Kwanza mimi nimesamehe tu, ningeweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” anasema Mkuu huyo wa Wilaya katika mahojiano na Raia Mwema yaliyofanyika kwa njia ya simu na anaendelea kuweka msimamo wake:

“Yeyote anayepinga sheria nitamshughulikia. Huwezi kumuondoa mtu katika nafasi yake ya uongozi hivi hivi. Zipo taratibu za kisheria kumuondoa. Nilisema hivi, anayekwamisha shughuli zetu za maendeleo nitamshughulikia. Nitamuondoa katika nafasi yake kwa mujibu wa sheria.”

Wakati Mkuu huyo wa Wilaya akiendeleza msimamo wake huo, baadhi ya maafisa waandamizi ndani ya Usalama wa Taifa mkoani humo wanamuona kuwa ni kiongozi mkorofi na asiye na uwezo wa kusoma alama za nyakati, wanabainisha wazi kukerwa kwao na kauli yake kutumia idara hiyo kuwatisha viongozi wa kutoka vyama vya upinzani.

“Hata mimi nilimuona yule diwani ana akili zaidi kuliko sisi. Tatizo hawa ma DC wengi wamepata nafasi hizo kutokana na ukada wao kwa chama. Wako nyuma ya wakati. Bado hawaamini mambo yamebailika. Wanadhani upinzani ni uhaini,” anasema afisa mmoja mwandamizi wa idara hiyo nyeti.

Wakati Mkuu huyo wa Wilaya aking’ang’ania kiwango cha 10,000/= kumekuwapo na shaka miongoni mwa wakazi wa Jiji hilo juu ya ufisadi kwenye michango hiyo ya ujenzi wa shule za sekondari.

Shaka hiyo inajengwa na aina za stakabadhi zinazotolewa zinazodaiwa kutengeneza mwanya wa wizi pamoja na baadhi ya wachangishaji kutumia kopi za stakabadhi zenye namba aina moja.
RAIA
 
Back
Top Bottom