Demokrasia na utawala wa sheria nchini miaka sita toka mauaji ya tarehe 5 januari 2011 Arusha

Francis12

JF-Expert Member
Sep 30, 2016
7,380
2,000
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
CHADEMA MKOA WA ARUSHA

TAARIFA KWA UMMA
5 JANUARI 2017

DEMOKRASIA NA UTAWALA WA SHERIA NCHINI
MIAKA SITA TOKA MAUAJI YA TAREHE 5 JANUARI 2011 ARUSHA

Leo Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla bado una kumbukumbu chungu ya tukio la mauaji yalitokea katika Jiji la Arusha ambalo lilipekea kuuwawa kwa wananchi watatu walioripotiwa Denis Shirima, George Njuguna (Mfanyabiashara Mkenya ambaye alikuwa ameshuka kutoka Namanga kwa safari ya kibiashara) na Omari Hamisi. Pamoja na wengi sana kujeruhiwa kwa risasi za moto, mabomu yaliyofyatuliwa na polisi na kugongwa na magari. Arusha Mjini ilishuhudia damu ikimwagika, hospitali za jijini Arusha zilipokea mamia ya wanaume, vijana, wanawake hadi watoto waliopigwa kwa risasi pasipo na hatia hata kidogo.
CHADEMA Mkoa wa Arusha pamoja, familia za wote waliofiwa na wapenzi wao na Watanzania wote tunaungana kukumbuka damu za ndugu zetu zilivyomwagika. Ni majonzi makubwa sana na kamwe haitasahaulika katika historia ya mapambano ya kudai utawala wa kidemokrasia katika nchi hii. Maandamano hayo yalitokana na namna uchaguzi wa kumpata MEYA wa Jiji la Arusha ulivyobaka Demokrasia na kufanya uchaguzi kihuni ya wazi wazi kabisa. Maandamano haya ya amani yalikuwa na lengo la kupaza sauti za wengi katika kudai HAKI na kuzingatia sheria na kanuni. Leo Arusha tunajivunia uimara na umathubuti wa kisiasa.
CHADEMA Mkoa wa Arusha tunaendelea na tutaendelea kuenzi tukio hili kwa heshima ya Wakazi wa Jiji la Arusha ambapo wananchi wa Jiji hili walishuhudia uchokozi wa polisi pale walipokuwa katika viwanja vya NMC kwenye mkutano wa hadhara siku hiyo hiyo mabomu yalifyatuliwa na kupelekea maelfu ya wakazi waliokuwa wakifuatilia mkutano huo kutawanyika na kukanyagana uwanjani hapo. Tukio hili lilisababisha majeruhi wengi sana sana. Hata mara baada ya tukio hili wakazi wa Jiji la Arusha ndio waliendelea mara MIA zaidi kuipenda CHADEMA na kuwaamini zaidi viongozi wa chama maana walielewa msingi wa kile tulichokuwa tumekisimamia kama chama, HAKI na UTAWALA WA SHERIA.

Kati ya tarehe 10 13 Januari 2011 mara baada ya tukio hilo Tume ya Haki za binadamu na utawala bora (Taasisi iliyopo chini ya serikali) ilikuja Arusha ili kufanya utafiti na ufuatiliaji wa tukio hili kubwa lililopelekea mauaji haya. Tume ilimteua Mhe Kamishna Joaquine De-melo akiandamana na Afisa uchunguzi Phillip Sungu kuja Arusha na kufanya uchunguzi wa tukio hili. Lengo kuu la uchunguzi huu ikiwa ni kubaini chanzo cha vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu kama ulikuwepo ili kutoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka husika. Mapendekezo na maoni ya TUME hii yalidhihirisha chanzo ni nani na jinsi ambavyo kulikuwa na kiwango cha kutisha cha uvunjwaji wa haki za biandamu.
Baada ya kukutana na pande zote kwa maana ya Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha na Wilaya, uongozi wa CHADEMA Mkoa na Wilaya, Madaktari, Majeruhi, baadhi ya wananchi na wakazi wa jiji la Arusha na kupitia nyaraka kadhaa ambazo wote CHADEMA na jeshi la polisi walizitoa kwa ajili ya uchunguzi huu, tume ilifikia kutoa maoni na mapendekezo yafuatayo ambayo yalisainiwa na Jaji (Mstaafu) Amiri Ramadhani Manento tarehe 1 Machi 2011.
MAONI NA MAPENDEKEZO YA TUME
Tume imeona kuwa, kitendo cha polisi kuzuia maandamano ya amani na halali ilikuwa ni uvunjwaji wa haki za Binadamu na ukiukwaji wa Mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia ilikuwa ni kinyume na Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali za nchi. Ukiukwaji huo ulipelekea maafa makubwa ikiwemo vifo vya watu watatu (3) na wengine wengi kujeruhiwa, uharibifu wa mali na wananhi kukosa imani na polisi (serikali). Hivyo ni vema serikali kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika na mauaji na uharibifu wa mali ili haki itendeke na wananchi kurudisha imani kwa serikali yao.
Ni vema kushirikiana na vyombo vinavyohusika na kurekebisha sheria kupitia na kurekebisha sheria kandamizi na zinazokinzana ili kuondoa migongano katika sheria hizo.
Kuelimisha jamii, viongozi, wadau na wataalam mbalimbali, kuheshimu maamuzi na mitazamo mbali mbali ya kisiasa, kiitikadi, kidini na kitamaduni kwa utashi, kuvumiliana na kuheshimiana. Kuna haja ya kuweka mikakati mahususi ya kuhakikisha kuwa jamii inaufahamu wa kina wa Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, elimu ya Haki za Binadamu, sheria za nchi, na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa nchini inaeleweka na kuzingatiwa, kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.
Serikali iangalie kwa undani kero za watumishi wa umma hasa jeshi la polisi ambalo limegubikwa na changamoto nyingi za kiutendaji na kimaadili ikiwemo rushwa ili kuboresha hali za kimaisha kwa askari na kufuata maadili ya kazi zao.
Kuandamana ni haki ya kikatiba na Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamii (civilian). Kama nchi inayozingatia demokrasia serikali haipaswi kuzuia haki ya kuandamana bali kuhakikisha haki hii inatekelezwa bila kuathiri amani na utulivu wa nchi.
Kwamba, kazi kubwa ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hakuna namna jeshi hili litatimiza malengo haya bila ushirikishwaji wa wananchi, kwani makundi haya yanategemeana. Hivyo ni vema serikali kuhakikisha inatimiza wajibu wa kuheshimu, kulinda na kutekeleza haki za wananchi ili wananchi nao wawajibike kuheshimu, kutii na kutekeleza sheria za nchi. Hii itajenga uhusiano mwema baina ya polisi(serikali) na wananchi na kupunguza uhasama na chuki iliyojengeka kati ya makundi haya.
Leo ukiyasoma mapendekezo haya unayaona kabisa yapo hai kwa maana yanahitaji kufanyiwa kazi.
CHADEMA MKOA WA ARUSHA leo tuikumbushe au pengine tuiambie serikali ya awamu ya tano kwa nia njema na kwa mapenzi mema na nchi yetu kwa kuzingatia maoni na mapendekezo ya TUME YA HAKI ZA BINADABU NA UTAWALA BORA, kwa kuangalia mwenendo mzima wa nchi kwa kipindi hiki;
Serikali ya awamu ya tano izingatie utawala wa sheria. Kwa bahati mbaya sana kuna mwenendo unaonekana kwa dhahiri kuwa nchi inaendeshwa kimatamko tamko. Nchi kuendeshwa kwa matamko na kauli mbiu maana yake ni kupoteza uelekeo (FOCUS) wa ajenda au kushindwa kusimamia ajenda ambayo mwanzoni walijinadi kusimamia.
Jeshi la polisi lisifanye uadui na vyama vya siasa. Jeshi la polisi hawalali isipokuwa kwa kuwaza CHADEMA au vyama kadhaa vya upinzani watawadhibiti vipi. Picha inayotafsirika kuwa wanatumika na chama tawala kwa maana ya serikali kuua na kugandamiza upinzani. Athari ya muonekano huu ni mbaya maana vyama na wananchi wanaweza kuungana dhidi yao. Hii ni tahadhari.
Serikali ionyeshe kuthamini maisha ya watu wake. Serikali ione kufedheheka iwapo wananchi wake wanakufa kwa sababu zozote zile (ajali, njaa, ugaidi, nk), kupotea kwa sababu zozote zile. Hii ni sambamba na iwapo wananchi wanapata majanga ambayo ni ya kiasili serikali ionyeshe huruma kwa matamshi yake na matendo ya huruma ya kijamii. Ni aibu ni fedheha na ni uongo kusema unawapenda watu wako halafu iwapo wananchi wanapata majanga unawasimanga. Serikali kupitia matamshi yake ni vema ionyeshe kujali.
Serikali iboreshe maslahi ya watumishi wa umma hususani Jeshi la Polisi. Hatua za kinidhamu kwa wale watumishi wasio waadilifu zisiendane na kuwaachia wengine hofu. Hofu inayojengwa kwa watumishi wa umma inaondoa ufanisi wa kazi. Watumishi wa umma wapate stahiki vizuri na isionekane kama ni anasa watumishi wa umma kulipwa vizuri. Ni vibaya kuwachonganisha watumishi wa umma na wananchi kiasi kwamba wanaonekana kuwa wabadhirifu na wanajilipa hovyo hovyo, hapana sio sawa wachache wabadhirifu waondolewe na wanaobaki waheshimiwe na walipwe vizuri.
Serikali ya awamu ya TANO ijifunze kuwa WAVUMILIVU. Uvumilivu ni pamoja na kuwa tayari kusikia wapinzani wako wanasema nini. Kuambiwa kuwa hufanyi vizuri mahali fulani sio DHAMBI na SIO DHAMBI hata kidogo. VIkao vya Bunge vionyeshwe LIVE (MUBASHARA) na wananchi wafuatilie kazi za wabunge wao, aidha maneno ya kukosoa utendaji yasionake kama vile ni uchochezi.
Serikali ya awamu ya tano isipotoshe kuwa siasa zinazuia maendeleo ya nchi. Hii si kweli na sio kweli hata kidogo. Siasa ni maisha na siasa ni uchumi. Kupitia siasa yaani mikutano ya hadhara wananchi wanaweza kupaza sauti zao na kusikika kuhusiana na masuala mbalimbali yanawahusu ya kimaendeleo.
Serikali ya awamu ya tano na kimaalumu sana kwa MHE RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kwa heshima abatilishe kauli yake ya kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa. Kwa kauli ile hatudhani kama kwa kuzuia mikutano ya hadhara ndio italeta maendeleo kwa haraka, hatudhani. Siasa ni kazi na awaache wanasiasa nao wafanye kazi yao (SPECIALIZATION). Kauli ile ni kinyume kabisa kabisa na katiba ya nchi na sheria zetu tulizojiwekea.
KWA UMUHIMU
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe Godbless Lema kupitia maadhimisho haya ya miaka 6 ya tukio la mauaji ya Arusha, tunamtamka kama SHUJAA MASHUHURI WA SIASA ZA ARUSHA. Hivi sasa yupo gerezani kisongo kwa kile ambacho kimetufedhehesha wengi kwa kunyimwa dhamana ambayo iko wazi kuwa ni haki yake kwa shitaka analotuhumiwa nalo. Haki yake hii inacheleweshwa lakini itafika tu maana hakuna marefu yasiyo na nchi na wanaohusika na hila hii watalipa gharama ya hila hii. Hizi zinazoitwa sarakasi za kisheria (Legal Acrobatics and Technicalities) anazofanyiwa Mhe Lema zitafika kwa mwisho mbaya na wa aibu kwa hao wanaofanya. Haki ni Haki tu huwa haichezewi kwa sarakasi za kisheria. (MUNGU NI MUNGU WA HAKI ANA WIVU JUU YA HAKI NA HASIRA KWA ASIYETENDA HAKI).

Imetolewa leo
Tarehe 5 Januari 2017
Amani Golugwa
MWENYEKITI CHADEMA MKOA WA ARUSHA.
Arusha.
Na KATIBU KANDA YA KASKAZINI.
 

Francis12

JF-Expert Member
Sep 30, 2016
7,380
2,000
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe Godbless Lema kupitia maadhimisho haya ya miaka 6 ya tukio la mauaji ya Arusha, tunamtamka kama SHUJAA MASHUHURI WA SIASA ZA ARUSHA. Hivi sasa yupo gerezani kisongo kwa kile ambacho kimetufedhehesha wengi kwa kunyimwa dhamana ambayo iko wazi kuwa ni haki yake kwa shitaka analotuhumiwa nalo. Haki yake hii inacheleweshwa lakini itafika tu maana hakuna marefu yasiyo na nchi na wanaohusika na hila hii watalipa gharama ya hila hii. Hizi zinazoitwa sarakasi za kisheria (Legal Acrobatics and Technicalities) anazofanyiwa Mhe Lema zitafika kwa mwisho mbaya na wa aibu kwa hao wanaofanya. Haki ni Haki tu huwa haichezewi kwa sarakasi za kisheria. (MUNGU NI MUNGU WA HAKI ANA WIVU JUU YA HAKI NA HASIRA KWA ASIYETENDA HAKI).
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom