Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,796
- 31,809
Daraja la Dr. Dau
Daraja la Kigamboni
‘’Lazima nikiri kuwa nilishtuka nilipofungua gazeti la “Mwananchi” na kukuta picha ya Abuu na chini yake ipo taazia iliyoandikwa na Dk. Ramadhani Dau. Haukupita muda napokea ujumbe a simu kuwa ipo taazia nyingine ya Abuu katika “Uhuru” na “Jambo Leo” zote zimeandikwa na Dk. Dau na amenunua ukurusa mzima kuomboleza kifo cha rafiki yake. Kwa hakika nilipigwa na butwaa. Mimi Abuu ni mdogo wangu kwa maana halisi ya neno lenyewe.
Kaka yake Abuu, Abdallah Mohamed Tambaza ni rafiki yangu toka utoto na tulisoma sote St. Joseph’s Convent katikati ya miaka 1960 na hadi leo ni rafiki yangu kipenzi. Isitoshe wazee wetu wakijuana.
Taazia zile tatu zote zimetoka siku moja tena kwa kurasa ya kulipiwa na ukurusa mzima kwangu mimi kitu hicho kilikuwa jambo geni. Sijapata kuona kitu kama hiki kabla. Kitendo cha Dk. Dau kumlilia rafiki yake kwa namna ile kilinidhihirishia mapenzi ya hali ya juu kati ya watu hawa wawili.
Dau aikuwapo hospitali Hindu Mandal wakati rafiki yake yuko katika sakarat maut na bila shaka ninavyomjua Dau pale alipokuwa kwa hakika kabisa Yasin ilikuwa ikimtoka. Watu waliokuwa wakipendana na wakajahitimishana namna hii ni wa kuliliwa ngoa.
Fikra zangu zilirudi nyuma mara ya mwisho mimi na Abuu tulipokuwa ofisini kwa Dk. Dau. Baada ya maskhara yao kama kawaida Dau aliagiza na mara sote wawili tukaletewa zawadi za NSSF katika mifuko maridadi.
Mimi kama mwandishi kila niwapo huwa na zana zangu za kazi. Niliwaomba niwapige picha na nikawapiga picha pamoja, ndugu wapenzi marafiki wawili. Haukunijia hata kidogo kwa wakati ule kuwa picha ile itakujakuwa kumbukumbu kubwa ya majonzi.
Msomaji wangu ungepata bahati ya kuwakuta watu hawa wawili katika barza wanazungumza wewe usingelitia lako ungekaa kimya usikize. Mimi nikifanya hivyo kila nilipokuwanao pamoja.
Kwanza ngoja nikufahamishe kitu. Ikiwa unataka kukisikia Kiswahili cha pwani kwa lafidhi yake halisi ilikuwa umsikize Abuu akizungumza. Mimi kwa vijana wa leo sijapata kumsikia kijana aliye na ulimi aliokuwanao Abuu.
Hilo moja. Sasa ngoja nirudi kwa sahib wake Dau. Dk. Dau ana ulimi kama aliokuwanao Abuu lakini hakumshinda na hili naweza kulieleza.
Ingawa wote wamekulia katika mazingira sawa ya mjini na kukisema Kiswahili kwa lafidhi ya pwani iliyonogeshwa kwa wao kusoma Qur’an iliyonyoosha matamshi yao, Dk. Dau kwa kiasi kidogo sana kaathirika na kule kusoma Kizungu sana. Matamshi ya Dk. Dau hayatoki na ile ladha unayoisikia kwa Abuu.
Sasa wanapopambana katika baraza ilikuwa raha na wote wana barza huwa kimya wakiwasikia wanavyopashana. Raha ilikuwa katika ujuzi wa lugha na pili katika kule kupeana maneno. Dau atamuambia Abuu huku akicheka sana, “Abuu leo sheikh nimekuwa sina maana, ushasahau nilivyokuwa nakuvusha barabara Morogoro Road tunakwenda shule...”
Barza itaangua kicheko. Abuu atarudisha mapigo sasa kawageukia wasikizaji, “Jamani hebu semeni wenyewe huyu kwa ukubwa gani aliokuwanao kiasi yeye anivushe mie barabara. Mimi siwezi kuwa mwizi wa fadhila kama yeye leo kasahau kama kuwa mimi ndiye nilkuwa nikiwatisha watoto wa Kihindi shule wasimpige...” Hapo vicheko vinaongozeka.
Hapo pembeni yuko mzee wetu mkubwa wa barza na mwenyekiti wa kudumu, Mzee Kissinger, Mohamed Khalil, Jamil Hizam (Denis Law), Panji (mdogo wake Abuu) na jamaa wengine dhumna inakwenda lakini watu wameshikilia mbavu kwa kicheko.
Jamil Hizam watatu waliochuchumaa kulia
Timu ya East African Cargo Handling Services
Mzee Kissinger ni kamusi inayotembea kuhusu historia ya Dar es Salaam na watu wake. Jamil Hizam alikuwa mcheza kandanda hodari katika miaka ya 1960 hadi 1970 ndiyo watoto wa mwanzo kutoka Dar es Salaam kucheza timu ya taifa ya vijana Tanzania. Jamil katika ujana wake akimuhusudu Denis Law mchezaji wa Uingereza na jina akalipata la shujaa wake.
Dau na Abuu wanatazamana kila mmoja anasubiri mashambulizi. Abuu kama vile namuona kaegemea ukuta, kofia yake kaibenjua kwa mbele. Dk. Dau na yeye yuko katika darzi yake na kofia kaiweka upande kwa mvao maarufu wa watu wa Mafia.
Dr. Dau na Marehemu Abubakar Tambaza
Hawa ndiyo marafiki wawili ndugu waliopendana na wakaonyesha mapenzi yao kwa dhati ya nafsi zao na kwa vitendo. Dk. Dau mkurugenzi wa shirika kubwa, alipata kuwa mhadhiri Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam amekaa barazani kwa rafiki yake Abubakar, Kariakoo Mtaa wa Kongo kamfuata kumjulia hali. Kwake yeye Abuu ni yule yule Abuu rafiki yake, cheo chake cha ukurugenzi na kisomo chake hakikuathiri hata chembe uhusiano wao.
Wangapi leo wanayaweza haya. Tunayo mifano mingi ya baadhi ya jamaa zetu wakiingia katika nafasi basi husahau rafiki zao wa zamani na kuwanyanyapaa wakajishughulisha na hao ambao wao huwaona ndiyo “stahili” zao kwa kuwa ni “wakubwa” kama wao. Wakawa wao ni watu wa Gymkhana Club na mahoteli makubwa ya fahari…’’
Huyu ndiye Ramadhani Dau kwa mukhtasari kwa wale wasiomjua.
Nduguze Dr. Dau
Kushoto: Marehemu Ugundo, Mzee Kissinger, Mfaume Diffu na nyuma
Kaburu
Katika upande wa akili Allah kamjaalia akili ambayo si ya kawaida. Yeye siku zote kuanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu namba yake ni moja. Ziko sifa zake nyingi lakini kwa leo tutosheke kwa haya.
Twende kwenye Daraja la Kigamboni. Watu wa Dar es Salaam wanaliita Daraja la Dau. Siku moja nilikuwa nazungumza na Dr. Dau nikamuuliza daraja linakwendaje? Hapo ndipo nikamwambia kuwa kwingi ninapopita Kariakoo jamaa wanaliita lile daraja - Daraja la Dau. Dr. Dau akatingisha kichwa akacheka.
Daraja la Dau leo limekuwa kweli. Daraja limekamilika kujengwa na leo magari yameanza kupita. Wananchi wamefurahi na picha nyingi zimepigwa na watu waliotumia daraja hilo leo. Baada ya miaka mingi ya foleni zinazochosha leo hii barabara ya kuingia Ferry kuvuka kwenda Kigamboni ilikuwa nyeupe.
Hili ni Daraja la Kigamboni. Lakini itakapokuja kuandikwa historia ya daraja hili jina la Dr. Ramadhani Kitwana Dau litaandikwa pamoja na historia ya daraja na historia nzima ya Kigamboni na Dar es Salaam yake. Hao watakaokuja baada yetu ndiyo watakuwa waamuzi waadilifu wataosimama katikakati ya mizani na kumpima ndugu yangu Ramadhani kwa mizani iliyo sawa.
Waziri wa Ujenzi Dr. Joseph Magufuli akishuhudia