Chama cha CUF kimeibuka kuwa mpinzani mkubwa wa CHADEMA hata katika mambo ambayo chenyewe kilikuwa kikiyaamini kilipokuwa chama kikuu cha upinzani. CUF hawajiulizi ni vipi CHADEMA imepata umaarufu wa ghafla namna hii. Kwa mtazamo wangu, umaarufu wa CHADEMA sio wa ghafla bali ulijengwa taratibu. Zifuatazo ni miongoni mwa tofauti za utaratibu ndani ya vyama hivi.
- Tangu kuanzishwa, CHADEMA imekuwa na wenyeviti watatu na wawili waliostaafu bado ni wanachama wenye kuheshimika ndani ya CHADEMA tofauti na CUF yenye king'ang'anizi asiyependa mabadiliko.
- CHADEMA kimezushiwa kuwa na udini baada ya CCM kuona nguvu yake. Hali ya CHADEMA ni tofauti na CUF ambapo mwaka 1995 mwenyekiti wake alipiga kampeni misikitini wazi wazi na katika mikutano yake utakuta ni vi-barghashia vinatawala.
- CHADEMA imebadilisha karata ya ugombea urais baada ya Mbowe kujaribu bila mafanikio ndipo ilipomleta Slaa aliyetokea kuwa kipenzi cha wengi tofauti na Lipumba tunayemtarajia tena 2015.
- Dr. Slaa wa CHADEMA amekuwa maarufu zaidi kwa staili ya yake kulipua mabomu bungeni na kuwataja mafisadi bila woga tofauti na Lipumba ambaye hajawahi kukemea ufisadi kwa besi.
- CHADEMA ni walifanya ujanja kwa kuiga staili ya Obama kufanya kampeni kupitia mitandao ya simu na internet na CUF walifikiri haitawasaidia kwani vijana wengi walionekana kutopenda siasa, ikala kwao.
- CHADEMA walitengua msemo wa nabii hakubaliki nyumbani kwa kuchukua jimbo analotoka mwenyekiti wao na katibu aliyekuwa akigombea urais, tofauti na CUF waliopoteza nyumbani kwa mwenyekiti. Hii inatokana na tofauti ya kuwekeza ambapo CUF wamewekeza zaidi visiwani huku wakiutaka urais wa muungano.
- Wakati CUF wanazinduka kumleta machachari Mtatiro katika siasa zao wanasahau kuwa CHADEMA waliliona hilo mapema na kuwa na vijana kama Mnyika, Zitto, Kafulila, nk
- Wazee wa CHADEMA hawaangalii zaidi wao wanataka nini, bali watu wanataka nini. Ndio maana mwanamuziki Sugu ambaye kwa kauli za awali za wapinzani wake walimwita mhuni, akawekwa kulikwaa jimbo. CCM nao kama CHADEMA walikuwa wakiandamana na kundi kubwa la wasanii wakiongozwa na Joseph Haule. CUF walidhani kipaza sauti pekee kinatosha.
- Nguvu kubwa ya kimaamuzi CCM ipo kwa mwenyekiti, CHADEMA ipo kwa baraza kuu na CUF ipo kwa katibu mkuu.
- CHADEMA, hata kama wanakosea; wana kawaida ya kutoa tamko pale jambo linapojitokeza. Tofauti na CUF ambao wana kawaida ya kusubiri kwanza kuona upepo unavumaje.
- Siasa ni kama dini ambapo muumini huvutwa na mlengo wa chama. Kimataifa, CHADEMA kimefuata mlengo wa kulia na ndio maana kinahusishwa na vyama kama conservative cha Uingereza na Republican cha Marekani, na CCM mlengo wa shoto kikihusishwa na Labor cha Uingereza na Democrats cha US. CUF kama chama, mlengo wake hauko wazi.
Ni dhahiri basi CUF wana kazi kubwa ya kurekebisha kuanzia ndani ndipo watoke uwani. Umaarufu wa CHADEMA usiwatie wivu hata wakaamua kuwapinga katika masuala yenye manufaa kwa Watanzania. Kushiriki katika serikali ya Zanzibar kusiwe chanzo cha uswahiba na serikali ya Tanzania na kuwa mpinzani wa wapinzani wenzako.
angalizo : mwanzisha sredi sio mwana CUF wala CHADEMA
Mkuu samahani sana ktk hoja hiii inaonyesha wewe ndiye mwenye kuisakama CUF.. Matusi yote haya ya nini ikiwa Chadema imefanikiwa kwa mtazamo wako.. Labda nikwambie tu moja ya kwamba CUF wana matatizo yao na inajulikana wazi kwamba chama hiki kilizushiwa Udini kaaChadema walivyozushiwa lakini wapo wanachama wengi wanaoendesha Udini ndani ya vyama hivi. Na wewe unajionyesha wazi kwamba ni Mkristu mwenye chuki na Uislaam.. Hali halijifichi na umeliweka wazi..
Pili, Chadema wamekuwa maarufu sio kwa sababu ni chama mbadala, laa hasha ni kwa sababu CCM inakufa, CCM imepoteza mwelekeo na hivyo Chadema ndio chama pekee kinachoshindilia kidole ktk madonda ya CCM. Lakini umaarufu wa NCCR au CUF kwa wananchi na mapenzi ya chama bado kabisa Chadema haijafikia mapenzi yale kwa sababu Ukimwondoa Dr.Slaa, chama kinapoteza nguvu kubwa wakati CUF na NCCR waliondoka viongozi lakini bado wananchi waliweka mapenzi yao kwa vyama. Hawa CUF na NCCR walipambana na CCM wakati kikiwa imara na chenye mvuto zaidi ya leo hii, hivyo wape pongezi zao..
Sema tatizo la vyama hivi vyote ni uongozi wa ndani. Makosa haya yapo CUF, NCCR na hata Chadema ambako kuna Opportunist, watu wamejipanga kugombea nafasi za kazi na uongozi wajuu wa chama badala ya kujihusisha zaidi na wananchi na hii pekee ndiyo ilomtenganisha Dr.Slaa na viongozi wengine. Kwa upande mwingine Mbowe ameifanya kazi kubwa ya kuweka msimamo wa chama ktk kufikia maazimio walokusudia japokuwa amekuwa na upinzani mkubwa toka ndani..Upinzani ambao hautazami mwelekeo wa chama na agenda zake bali - ULAJI kwa sababu maskini siku zote hutaka shibe kwanza kabla ya kuangalia maswala mengine.
Hizi ndizo siasa za Bongo, nchi maskini ambayo wanajaribu kugawana umaskini kwa kutumia mbinu za matajiri na nchi za Ulaya. Tajiri huwekeza
FEDHA zake akitegemea faida kwa kipindi fulani lakini maskini akiwekeza
MUDA wake (maana hana mtaji) ndio kaondoa sahani ya chakula mezani.
Vyama vya Upinzani vyote vimejaa opportunist ambao kwa umaskini wao fikra za kuongoza chama ni kupata Ajira, Uheshimiwa na kupendeza ktk kumudu maisha ya nchi ilijaa Maskini, wajinga na wenye maradhi.
Na amini maneno yangu kwamba watu tunaikubali Chadema kwa sababu hakuna chama kinachotumia udhaifu wa CCM kama mtaji wao isipokuwa Chadema lakini haina maana tunakubaliana na bandiko lako. Umezusha mengi kwa fikra zako na kujipa matumaini makubwa lakini Chadema ni chama bado kabisa dhaifu na kinahitaji kujipanua kama chama chenye itikadi na sio kutumia umaarufu wa Dr.Slaa, Mbowe na Zitto kuwa mtaji mkubwa wa chama.