CUF Habari: Habari zilizobamba wiki hii

Dunia yakoo

Senior Member
Nov 23, 2019
122
250
CUFHABARI NA HABARI ZILIZOBAMBA WIKI HII

Ndugu msomaji wetu karibu tena kwenye Ukurasa wetu huu wa CufHabari ambapo Leo tunakumbushana habari muhimu zilizochukua umuhimu Mkubwa kwenye wiki inayoishia jumamosi Januari 30, 2021.


A. HABARI ZA KITAIFA
(i ) Siku ya Mashujaa wa CUF- Chama Cha Wananchi:
na Mapambano ya Kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi:

CUF- Chama Cha Wananchi Jumatano Januari 27, 2021 kimefanya Dua na Maombi kwa ajili ya Kuwakumbuka Mashujaa wa Chama hicho waliouawa kinyama Januari 26 na 27, 2001 huko Zanzibar wakiwa kwenye Maandamano ya Amani ya kupinga wizi wa Kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2000 na kudai Katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi.

Akiongea kwenye Kumbukizi hizo, Mwenyekiti wa Chama Prof. Ibrahim Lipumba alitoa wito kwa Rais Magufuli kufufua Mchakato wa Katiba Mpya kuanzia kwenye Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ili kupata Katiba yenye Maridhiano na inayotokana na Maoni ya Wananchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu Bara Mheshimiwa Magdalena Sakaya alisisitiza Umoja na Mshikamano baina ya Wananchi wote na taasisi mbalimbali katika Mapambano ya Kudai Katiba mpya yenye Tume huru ya Uchaguzi.

Nao UKUKAMTA waliendeleza Mapambano ambapo mwanzoni mwa wiki hii walimualika Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF-Chama Cha Wananchi, Mhandisi Mohamed Ngulangwa kuelimisha juu ya Umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya kwa watanzania.

Kipindi hicho kilichofanyika Jumatatu Januari 25 kuanzia saa 03:00 kiliibua ari na hamasa kubwa kwa walioshiriki. Mhandisi Ngulangwa amekuwa ni mgeni wa Pili kualikwa UKUKAMTA baada ya Mheshimiwa John Pambalu wa BAVICHA kutangulia wiki moja iliyopita.

UKUKAMTA ni Umoja wa Kudai Katiba Mpya Tanzania unaoundwa na wanachama wa vyama mbalimbali, wanazuoni wa fani mbalimbali, Viongozi wa Taasisi na Asasi mbalimbali pamoja na Wananchi wa kawaida walijumuika kwa nia ya kushiriki kwa pamoja Mapambano kudai Katiba Mpya na Tume huru ya Uchaguzi nchini.

Vyama vya CUF- Chama Cha Wananchi, NCCR- Mageuzi, CHADEMA na Viongozi wa Dini kama Sheikh Mussa Kundecha na Askofu Mwamakula wameshajitokeza hadharani kuonesha utayari wao wa Kuipambania Demokrasia nchini kwa kuanzia kudai Katiba mpya yenye Tume huru ya Uchaguzi.

Kwa Upande mwingine CCM na maswahiba wao katika Kuunda Serikali wanadaiwa kupanga mbinu mbalimbali za kukwamisha Mapambano hayo, moja ya mbinu hizo ikiwa ni kutumia waandishi wa Habari wasio waaminifu kuwatoa Wananchi kwenye agenda hii muhimu kwa kuwachomekea mambo mbalimbali ya Uzushi. Kilichofanywa na Mwandishi wa gazeti la mwananchi Toleo Na. 7480 la Januari 28, 2021 dhidi ya Prof. Lipumba ni katika mikakati hiyo ya CCM na washirika.wake. Watanzania wameaswa kuwapuuzia waandishi wote wababaishaji katika kipindi hiki cha Mapambano mazito.


(iii) Mapambano dhidi ya CORONA: Rais Magufuli akizindua Shamba la miti huko Chato amekiri kuwepo kwa CORONA na akasisitiza juu ya kufuata njia za kupambana na maradhi hayo ikiwa ni pamoja na kujifukiza.

CUF- Chama Cha Wananchi wakiongea kupitia DW habari za mchana Ijumaa Januari 29 pamoja na kuunga mkono maamuzi ya kutoifungia nchi ( Lockdown), kilitoa wito kwa Serikali kuangalia upya msimamo wake wa kukataa chanjo za CORONA kwa hofu ya chanjo hizo kutumika kuwadhuru waafrika kwa makusudi. Badala yake Chama hicho kimeitaka Serikali kuwahusisha wataalamu na kutathmini chanjo yenye ubora inayoweza kutumika nchini dhidi ya virusi vya CORONA.

"...Tunashauri wataalam wetu wajipange kutathmini ubora wa chanjo tunazoweza kutumia Tanzania dhidi ya CORONA, badala ya kuzikataa kienyeji. Aidha Serikali iweke Utaratibu mwepesi na usio ghali wa kupima CORONA...", alisema Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF-Chama Cha Wananchi katika sehemu ya Taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Shirika la Afya Duniani ( WHO) limeitaka Tanzania kutoa takwimu za mwenendo wa CORONA ili iwe rahisi katika kupambana na kuzuia maambukizi mapya.

"...Moja ya makubaliano ya Wanachama wa WHO ni kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa, nimewakumbusha Serikali ya Tanzania na ninayo kumbukumbu kwa maandishi kuwa wao ni sehemu ya Wanachama hivyo wanatakiwa kuitikia wito huu. Tuna imani kuwa Mawasiliano yetu kuhusu chanjo yatazingatiwa ili kukabili maambukizi ya virusi...", alisema Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshdiso Moeti kwenye Mkutano na waandishi wa Habari kwa njia ya Mtandao, siku moja baada ya Rais Magufuli kusikika akizitilia Shaka Chanjo za CORONA.

Mwanzoni mwa wiki Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ( TEC), Askofu Gervas Nyaisonga alipaza sauti kwa maaskofu wenzake kwa kuwahimiza wawaongoze Waumini wao katika Mapambano dhidi ya maradhi hatari ya CORONA kwa kuzingatia njia za Kisayansi pamoja na sala.


B. HABARI ZA KIMATAIFA
(i) Museven awa mbogo: Pamoja na kudaiwa kuongoza udanganyifu katika Mchakato wa Uchaguzi uliomrudisha madarakani, Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekataa katakata kuongea na wapinzani na kufikia Maridhiano kwa Maslahi mapana ya Uganda na Amani yake.

Wiki iliyopita Uganda ilifanya Uchaguzi ulioambatana na umwagaji wa damu na vitendo vya Ukandamizaji wa Haki za Binadamu.C. MICHEZO NA BURUDANI
(i ) Mashindano ya CHAN:
Timu ya Taifa ya Tanzania imepambana kiume na kutoka Sare 2- 2 na timu ya Taifa ya Guinea Januari 27, 2021.

Hata hivyo Tanzania imeshindwa kufuzu kucheza hatua ya Robo Fainali, ambapo timu za Guinea na Zambia zimefanikiwa kufuzu kutoka kundi hilo. Wadau wengi wa Soka wameisifu Taifa Stars kwa mchezo mzuri na kuutaja mchezo wa kwanza ambapo Tanzania ilipoteza kwa kufungwa 2-0 na Zambia kwamba ndio mchezo walioharibu kwa kucheza chini ya kiwango walichokidhihirisha kwenye mechi mbili zilizofuata.

(ii) Simba Super Cup 2021:
Mashindano ya Mabingwa yanayodhaminiwa na Mabingwa wa Soka nchini Simba Sports Club yanatarajiwa kufikia Tamati Jumapili Januari 31 kwa mechi ngumu kati ya Mnyama Simba na TP Mazembe ya DRC.

Katika mechi ya Ufunguzi Januari 27, Simba ikicheza kwa mara ya kwanza chini ya Kocha wake mpya Gomes, raia wa Ufaransa, liirarua El- Hilal ya Sudan kwa mabao 4-1 huku ' mzee wa Kukera' Benard Morrison akifunga magoli mawili ndani ya dakika tatu.

Baada ya kufunga goli la kwanza, Morrison alifanya " UKERAJI" kwa kukimbia nje ya Uwanja na Kuchukua mpira na kuutumbukiza kwenye bukta, kumithilisha ' busha' ambalo alizushiwa kupachikwa na timu yake ya zamani.

Magoli mengine ya Simba yalifungwa na Bwalya na Chikwende.

Katika mchezo wa Pili uliochezwa Januari 29, El Hilal ilijiuliza vyema na kuifunga TP Mazembe kwa magoli 2-1.


NB:
Usikose kutembelea ukurasa wa Cufhabari kila siku kwa habari za Kisiasa na kila jumamosi kuanzia saa 02: 00 usiku kwa Muhtasari wa Habari za wiki nzima.

Imeandaliwa na:

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Januari 30, 2021
 

Mnyanyembe wa Mboka

JF-Expert Member
Feb 10, 2017
1,853
2,000
Mh!!? Hapa nnamashaka kuwa hao mashujaa wa CUF wanaoongelewa hapa itakuwa roho zao huko kuzimu zilihamia ACT maana sidhani kama waliendelea kuwa CUF mpaka sasa huko walipo
 

antimatter

JF-Expert Member
Feb 26, 2017
5,110
2,000
Mh!!? Hapa nnamashaka kuwa hao mashujaa wa CUF wanaoongelewa hapa itakuwa roho zao huko kuzimu zilihamia ACT maana sidhani kama waliendelea kuwa CUF mpaka sasa huko walipo
Juzi tu niliona picha ya m/kiti wa cuf na maalim seif mahali, caption yake inasema:
Li-pumba amwangukia Maalim..
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom