Nilifikiri ningekuta uzi wenye updates humu, lakini matarajio yangu yamekuwa sivyo. Pamoja na vyombo vya habari kujitahidi kutangaza kwa usawa michuano hii inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ndani ya bara la Afrika, bado mwitiko wa washabiki umekuwa mdogo ukilinganisha na uzito wa mashindano yenyewe.
Tatizo halipo hapa tu, kwani hata mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya michuano hii inayofanyika nchini Afrika Kusini, Sipho Sithole alikiri kuwa walikuwa na muda mchache wa kuitangaza vya kutosha, kama miezi tisa hivi baada ya kumalizika kwa michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 ambayo ilifanyika hapo hapo Afrika Kusini.
Si mara ya kwanza kwa CAF kufeli katika kuitangaza na kuleta hamasa katika mashindano yanayoandaliwa nao, kwani takwimu zinaonesha kuwa kadiri muda unavyosonga, ndivyo mashindano ya soka ya ndani ya Afrika yanavyopungua umaarufu, kuanzia Afcon, Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho na sasa CHAN.
Lipo jukumu kubwa mbele yao, pamoja na kuendeleza soka katika ngazi ya bara, lakini pia kuhakikisha kuwa msisimko wa mashindano ya ndani unarudi kabla haujamezwa kabisha na soka la kigeni ambalo licha ya kuwatoa watu kwenye soka lao, limekuwa chanzo kingine cha mapato kwa vilabu vya Ulaya kutoka kwetu Afrika.