Chama Chahitaji Mapinduzi....

Dr Lizzy

Platinum Member
May 25, 2009
30,799
59,262
Chama Chahitaji Mapinduzi.

Sote tunajua kinachojiita “Chama cha Mapinduzi” hakijawahi kufanya mapinduzi yoyote. Neno mapinduzi kwa kadiri ninavyoelewa linaashiria “mabadiliko ya haraka ya kisiasa” wakati mwingine hata kumwagika damu au vurugu kama tulivyoona kule Misri na Tunisia. Katika nchi yetu mabadiliko ya aina hiyo yalitokea Zanzibar lakini hadi hivi sasa mjadala bado upo juu ya nani hasa walihusika. TANU tunajua haikuhusika (japo kwa wazi) na ASP kwa kadiri ninavyosoma humu inaonekana walidandia tu mbele ya safari.

Sasa kwanini CCM inajiita “Chama cha Mapinduzi” kama hakijawahi kushiriki mapinduzi yoyote? Ninaamini kuwa badala ya kukiita “Chama cha Mapinduzi” kana kwamba kina mapinduzi yoyote ni vizuri kukiita “Chama Chahitaji Mapinduzi” kwani jinsi kilivyo sasa hakiwezi kuendelea mbele bila mabadiliko makubwa ya ndani.

Kauli za Nape na zile za Katibu Mkuu wa CCM kuwa kumbe yale maneno ya “kujivua gamba” yalikuwa ni maneno tu na yasiyo na maana iliyotarajiwa zimenifanya niamini kuwa CCM inahitaji mapinduzi zaidi na labda ni mapinduzi ya kuvua magamba! Mapinduzi kwa kawaida ni kitu kigumu kama ilivyo kwenye kujivua magamba na wakati mwingine yanakuja na maumivu sana kama ilivyo kujivua magamba hivyo haiwezi kujivua magamba kiukweli kama haiko tayari kupitia hatua zote stahiki na kuleta mapinduzi wanayoyataja kila siku kwenye jina la chama chao.

Mimi ninavyoangalia hadi hivi sasa sioni ni nani ndani ya CCM anayeweza kuleta mapinduzi? Kule Misri na Tunisia walioleta Mapinduzi yaliyosababisha mabadiliko ya utawala ni vijana. Tatizo hapa kwetu vijana wenyewe wa CCM ndio wanaonekana kama sehemu ya magamba yenyewe!Vijana wa CCM ndio wa kwanza kutokea na magambaz yao ya kijani na njano kushangalia chama chao na hata wakianza kuzungumza maneno ya mabadiliko hawachelewi kuanza kupingana wenyewe kwa wenyewe.

Je, yawezekana watakaoleta mapinduzi ndani ya CCM watakuwa ni wazee waliochoshwa na siyo vijana? Ja yawezekana wazee ndio wanaona hasa mahitaji ya mabadiliko makubwa ndani ya CCM na siyo vijana? Je vijana walioko CCM ambao hawaoni haja ya mapinduzi ndani ya chama chao wanaweza kuwa tumaini la CCM huko mbeleni hasa katika siasa zetu zinazoonekana kubadilika kwa haraka kila siku?

Je bila Mapinduzi CCM inaweza kusurvive huko mbeleni? Au wameridhika kwa kujiita tu “Chama cha Mapinduzi” bila kuwa na “Mapinduzi” yoyote zaidi ya jina? Au wanafikiria “mapinduzi” ni jina la heshima tu bila kuwa na maana? Kama “mapinduzi“ ya kweli na yenye manufaa hawajawahi kushiriki na wala hawana mpango wa kujipindua angalau wabadili tu hata jina liendane na wanayofanya.Nadhani wakati umefika CCM ibadili jina kabisa; isiwe kitu chochote “mapinduzi” na kiwe CCM -Chama cha Matanuzi!
 
HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP



Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa tarehe 5 Februari, 1977 kutokana na kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).

Tendo hilo la kihistoria lilikuwa ni la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko nyuma wa kuunganisha nguvu kwa lengo la kujiimarisha katika mapambano. Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar ilitokana na kuungana kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA), tendo ambalo liliunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza. Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilitokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.
Kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, kulifanya TANU na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni mkongwe na usultani. Hata hivyo, vyama vya siasa hivi viliendelea kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru kiuchumi na kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, Katika mazingira ya ubeberu duniani wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua kuungana tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa Tanzania. Chini ya Muungano huo, Tanzania iliendelea kuwa na vyama vya siasa viwili, yaani TANU na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa. Vyama hivi vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi ulifanywa rasmi wa kuvunja TANU na ASP na kuundwa kwa Chama Cha Mapinduzi tarehe 5 Februari, 1977. Katiba ya CCM, katika Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP tarehe 21 January, 1977, inaeleza kuwa, (uk. 2-3), “...kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African Union(TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari, 1977 na wakati huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.” Muungano wa TANU na ASP ndio uliowezesha CCM kuwa Chama chenye nguvu, imara na madhubuti, hivyo kuwa Chama cha siasa pekee chenye uwezo wa hali ya juu wa kuwaunganisha Watanzania. Aidha, CCM kimeweza kuwaongoza wananchi katika mapambano ya kitaifa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi.CCM kimeendelea kupewa dhamana na wananchi ya kuunda serikali na kukamata dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hadi sasa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi yaliyoidhinishwa na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania Juni 1992.



Umuhimu wa kuielewa historia ya CCM na Vyama vilivyokitangulia


Historia ya CCM tangu TANU na ASP ina umuhimu wa pekee katika Taifa letu katika kuelewa tulikotoka, tulipo hivi sasa na tunakoelekea. Historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila ya historia ya vyama hivi vya ukombozi. Historia hutoa mafunzo na ni mwelekezaji pia, kwa hiyo ni wajibu wa Watanzania, hasa wanachama wa CCM kujifunza kutokana na historia yetu. Kazi kubwa na ya msingi inayofanyika katika kujifunza historia hiyo, ni kurithisha dhamira ya kujituma na kudumisha uhuru wa nchi yetu. Hivyo, ili kuendelea kukijenga Chama, na kuimarisha uwezo wa kuendelea kukamata dola barabara kwa namna endelevu, hapana budi ihakikishwe kuwa historia ya CCM inabeba pia jukumu la msingi la kusaidia:-

· Kujua Chama kilikotoka, mahali kilipo na kinakoelekea katika misingi ya sera, itikadi, malengo na wanachama.
· Kuunganisha wanachama na kuwaweka pamoja kiimani, kiitikadi na kiutendaji.
· Wanachama kujitambua, kutambua wajibu na majukumu yao na kujenga moyo wa kujiamini na kujithamini.
· Kuinua kiwango cha ushiriki wa wanachama wa CCM na wananchi katika kubuni na kutekeleza mkakati na mbinu sahihi za kutetea na kuendeleza Chama na taifa kufuatana na hali ya wakati na mahali.
· Kuweka misingi ya kufanya tathmini na hivyo kuwa na uhakika katika kufanya maamuzi.
· Kupanda mbegu bora za upendo, uzalendo na uchungu wa kweli kwa uhai wa CCM na taifa kwa ujumla.
· Kuwa na majibu sahihi wakati wote kwa hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu Chama Cha Mapinduzi na taifa kwa ujumla.
· Kuweka msingi wa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maadili ya msingi wa uhai wa CCM.
· Kuhifadhi kuweka na kueneza kumbukumbu sahihi ya historia ya Chama, nchi, mchango wa Waasisi na wanachama na kuhakikisha wapotoshaji hawapati fursa ya kueneza uongo.

Chimbuko la Historia ya CCM
Pamoja na kwamba Chama Cha Mapinduzi kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari, 1977, chimbuko lake linaanzia miaka mingi kabla, sambamba na historia ya uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya historia ya CCM imo ndani ya harakati za kukataa ukoloni na usultani, zilizofanywa na wananchi wa Tanzania. Wahenga wetu kwa pamoja tangu enzi, walionyesha wazi kukataa kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa mifano mingi ya harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na ujirani, katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya TANU na ASP.

Wananchi hao waliotutangulia walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na uhuru wao ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi ya udhalimu huo. Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni Vita ya Majimaji huko Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare, Waluguru, Wameru, Wahehe na mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa na katika jamii za wafugaji. Ari, utashi, uzalendo na dhamira ya kweli ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha katika harakati hizo, viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na ASP.
CHAMA CHA MAPINDUZI


Kuzaliwa kwa CCM


Katika Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP uliofanyika tarehe 22 Septemba, 1975 Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Tanzania ni nchi yenye Chama kimoja;

“Lakini kwa sababu kuna vyama viwili TANU na ASP, Katiba inazungumza juu ya Chama kimoja, hicho Chama kimoja kwa kweli ni vyama viwili … Siasa ya TANU na ASP ni moja yaani Ujamaa na Kujitegemea. Midhali Katiba ya Tanzania ni ya Chama kimoja, Katiba hiyo inataka hicho Chama chenye Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kishike hatamu na uongozi wa nchi”. (Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, uk. 3-4).

Kwa msisitizo huo, Mwalimu alipendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP na kuundwa kwa chama kipya. Pendekezo hilo liliwasilishwa kwa wanachama wa TANU na ASP ili kujadili na kutoa maoni yao. Matokeo ya maoni ya wanachama ni kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanachama walikubaliana na pendekezo la Mwalimu Nyerere. Baada ya kupokea matokeo ya maoni ya wanachama wao, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU na ile ya ASP, zilikutana na kufanya kikao cha pamoja Oktoba, 1976. Katika mkutano huo iliteuliwa Tume ya Watu 20 iliyopewa jukumu la kutayarisha Katiba ya Chama kipya. Mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Sheikh Thabit Kombo na Katibu wake alikuwa Ndugu Pius Msekwa.
 
Dhana ya mapinduzi ccm hawaiwezi na ni kujichanganya tu kwa chama kama hiki. Wakati huu tunahitaji mapinduzi kutoka kwa wananchi wenyewe mimi na wewe na wala si viongozi wa chama wala serikali
 
Lizzy ahsante sana kwa thread nzuri sana, lakini mimi kwa maoni yangu naomba tu CCM ife. Nasema naomba ife kwa sababu wamepata opportunities chungu nzima za kukisafisha chama chao ili kirudi kuwa ni Chama cha Wakulima na Wafanyakazi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla ya kuvamiwa na mafisadi.

Wameonyesha juhudi finyu mno za kukisafisha chama chao nahisi hii inasababishwa na Viongozi wote wa juu ndani ya CCM kutokuwa wasafi na uchafu wao unajulikana na kila mtu na hii ndio sababu kubwa hakuna ambaye anaweza kusimamia kikamilifu kuisafisha CCM. Hivyo kutokana na kushindwa kwao kujisafisha mimi naomba ni bora tu ife labda hii itasaidia nchi yetu kwa namna moja au nyingine kupata maendeleo ya kweli ambayo tumeshindwa kuyapata chini ya CCM pamoja na kuwa na utajiri wa rasilimali mkubwa sana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom