Mphamvu
JF-Expert Member
- Jan 28, 2011
- 10,702
- 3,356
Makala hii ilichapishwa katika Mwananchi, Jumatatu 2 Juni 2014...
Michezo ya Jumuia ya Madola inatarajia kuanza mwezi Julai mwaka huu huko Glasgow, Uskochi. Tanzania nasi tutashiriki michuano hii yenye sura ya kikoloni bila shaka, kama ambavyo tumekuwa tukishiriki miaka yote huku rekodi yetu ikiwa si ya kuvutia sana.
Kinachofanya ushiriki wa nchi yetu mwaka huu uwe wa pekee ni maandalizi makubwa yaliyofanyika na vyama vya michezo husika kwa ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Nje. Timu tofauti, kwa vipindi tofauti zilikwenda nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya madola, tangu Mei 4 mwaka huu.
Jambo hili sio tu linaongeza ufanisi wa kiufundi mchezoni, lakini pia linaamsha hamasa ya wachezaji pamoja na kurudisha imani ya washabiki kuwa Serikali ingali inajali michezo na mustakabali wake kitaifa.
Tukiacha timu zingine tano za ngumi, kuogelea, judo, kunyanyua vitu vizito na mpira wa meza ambazo zilikwenda kupiga kambi nchini China na Uturuki , makubwa yalizuka kwa upande wa timu ya riadha.
Timu hii ambayo husimamiwa na chama cha riadha nchini (RT) ilikumbwa na kashfa ya kupeleka majina ya wanariadha ambao hawakuwepo katika kambi hiyo iliyowekwa nchini New Zealand na Ethiopia. Majibu ya tuhuma hizi kutoka uongozi wa RT hayakuwa ya kuridhisha, ama tunaweza sema kuwa yalikuwa ya funika kombe mwanaharamu...
Walioweka wazi tuhuma hizo walitekeleza wajibu wao wa jicho la tatu, vyombo mbalimbali vya habari vikafanya kinachostahili, yaani kuutafuta ukweli. Kilichoonekana baada ya kupata ukweli kutoka pandez zote, nia ina ya ubabaishaji ule ule ambao umekuwa ukifanywa siku zote na vyama vya michezo vya kitaifa.
Tuhuma za kupeleka majina hewa ni kitu kimoja, lakini siku chache zilizopita RT wakashangaza tena taifa. Rais wake, ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mvomero, bwana Anthony Mtaka akizungumza na kituo kimoja cha redio, alisema kuwa Watanzania wasitarajie makubwa sana katika michezo ya Jumuia ya Madola kwani kuna washindani ambao walifanya maandalizi mapema na kwa ufanisi mkubwa, huku akiwataja Ethiopia kama mfano.
Kauli yake inaweza kuwa kweli katika mazingira fulani, lakini inashangaza kwanini RT waliridhia timu yao kuwekwa kambi nje ya nchi wakati wakijua fika kuwa maandalizi hayo yasingefaa kitu.
Kwa miaka mingi kisingizio cha kushindwa katika mashindano ya kimataifa kimekuwa ni maandalizi duni ya timu husika. Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya nje ikawezesha kuwa na maandalizi ya mapema, tena nje ya nchi ambako inaaminika kuna miundombinu bora kuliko hapa.
Timu zilizopelekwa kambini zimetumia fedha za Serikali, ambazo tunaweza kusema kuwa ni za walipa kodi, kwa jambo ambalo rais wa RT anadhani kuwa halina msaada mkubwa katika ushiriki wetu katika michuano ya Jumuia ya Madola.
Rais huyo na jopo lake la uongozi, pengine wangetumia busara kutoipeleka timu nje ya nchi kwa kazi isiyo na faida. Kama kweli RT walidhani kuwa maandalizi haya si kitu, walikuwa na uhuru wa kukataa pendekezo la wizara la kupeleka timu nje, na badala yake ikaenda timu nyingine ambayo inashiriki michuano hii kwani si timu zetu zote zilipata fursa ya kwenda kufanya maandalizi nje ya nchi.
Rais wa RT alidai pia si lazima maandalizi yatufae kwa michuano hii, bado kuna michuano mingine mikubwa ya All Africa Games itakayofanyika mwakani na tunaweza kutumia maandalizi ya sasa katika michuano hiyo.
Haihitaji kuwa mtaalamu wa masuala ya kiufundi kubaini kuwa hizi ni porojo, itawezekana vipi kwa maandalizi ambayo hayajakufaa kwa michuano ya karibuni yaje yakuweke fiti kwa michezo ambayo itafanyika mwakani na hata tarehe bado haijatangazwa. Vilevile huku ni kwenda kinyume na malengo ya wizara ambao walilenga kufanya maandalizi kwa ajili ya michuano ya Jumuia ya Madola na si vinginevyo.
Rais wa RT ana maono kuwa maandalizi haya ya wiki chache yanaweza kuwa na manufaa katika michezo ya All Africa Games, ni kama anataka kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kila mmoja anajua kuwa kuwa fiti kimchezo si sawa na fedha ambazo unaweza kuweka akiba ili zikufae baadae.
Haya ndiyo yanayotokea pale hoja za kiufundi zinapotolewa na mtu ambaye si mtaalamu wa mchezo husika. Hoja za 'kitaalamu' zilizotolewa na Mtaka zinashangaza na sijui kama kocha wa timu ya taifa ya riadha, amabye pia ni katibu mkuu wa RT alikuwa na usemi wake katika visingizio hivi.
Hivi ni kati ya visa vichache tu vya uongozi uliopo madarakani wa RT, ambao baadhi ya wanaharakati wanadai kuwa uliingizwa madarakani kinyume na katiba ya RT ukiwa unaongozwa na mwanasiasa.
mphamvudaniel@gmail.com
+255713049852