Ni jambo jema la kisiasa kupita maeneo mbalimbali ya nchi kueneza chama na kusema chama husika kina nini kipya kwa watanzania. Kuonesha jinsi gani CHADEMA ni mbadala wa CCM-kama chama tawala ili ifikapo chaguzi za 2014 na 2015 CHADEMA ikabidhiwe uongozi wa nchi.
Kulikuwa na Operesheni Sangara hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mwanza,Shinyanga,Mara na Kagera). Kimsingi,Operesheni hii iliwaamsha wengi na kuimarisha chama katika sehemu husika. Ukweli wa hili ulithibitika hapo 2010 ambapo CHADEMA ilipata viti vingi vya Ubunge katika Kanda hiyo ukilinganisha na Kanda nyingine za nchi hii.
Baadaye,ikaja Operesheni ya: Vua Gamba,Vaa Gwanda. Hii ilitembea karibu Tanzania nzima. Na bado inaendelea. Ni Operesheni iliyosheheni ushawishi na kuhamisha wanachama wa vyama pinzani kwa CHADEMA na kuhamia humo (CHADEMA). Kuna mafanikio katika hili pia. Na sasa kuna Operesheni za Kikanda. Kanda zinazinduliwa na kuanza kazi. Ni jambo jema. Ni ubunifu uliotukuka na wenye kupigiwa mfano.Kisiasa,kukosolewa kwa jambo lolote ni sifa kuu ya siasa. Operesheni itakosolewa lakini pia itapongezwa.Cha muhimu ni kusonga nayo mbele kwa malengo yaliyowekwa.
Hata chama chetu cha CCM kinafanya siasa bunifu. CHADEMA,kama chama kikuu cha upinzani nchini, kinaimarika na kueneaTanzania. Ingawa mimi ni m-CCM,napenda siasa safi na za ushindani. Siku yaja ambapo watanzania watachagua wagombea kwa sera,uwezo na malengo yao.Si kwa kuangalia chama atokacho,rangi za bendera za chama,viongozi wake wala historia ya chama husika. Watachagua maendeleo. Na vyama vitasimamisha wanamaendeleo.Tanzania itapiga hatua kubwa kimaendeleo. Siku yaja upesi!
Lakini,CHADEMA msiishie kupita tu kila mkoa,wilaya,tarafa,kata,kitongoji/kijiji,mtaa,nyumba nahata kitanda kwa kitanda. Mnakopita,acheni alama ya uwepo wenu. Jengeni Ofisi.Ofisi,pamoja na kuwa kielelezo cha uwepo wenu hapo,itahamasisha wanachama,kukusanya wanachama wapya na kadhalika.Ofisi ndiyo kila kitu. Ujenzi wa matawi tu hautoshi. Mnaweza kuanza na ngazi za kimkoa,kiwilaya na kitarafa.Taratibu ndiyo mwendo.
Sijui kwanini leo ninawashauri na kuwasisitiza jambo hili ambalo chama changu hupatia ushindi wa kihoja kupitia humo.Hatahivyo, ni siasa kuimarisha siasa.
Mzee Tupatupa wa Lumumba,Dar es Salaam.