Chadema kujadili mauaji ya Mwangosi

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
Sunday, 09 September 2012 09:22

YAKUTANA LEO DAR, MTEI AMTAKA KIKWETE ATOE TAMKO KUHUSU MAUAJI HAYO
Fidelis Butahe
KAMATI Kuu (CC) Chadema inakutana leo katika kikao chake cha dharura, kujadili hali ya siasa nchini na mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi katika mikutano yake, yakiwamo ya mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.

Kikao hicho kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kitatoa uamuzi wake juu ya vitendo vinavyofanywa na polisi na Serikali, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutoa tamko lolote hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho jana ilieleza kuwa vitendo vinavyofanywa na polisi ni kinyume na Katiba ya nchi na kudai kwamba, lengo la Serikali ya CCM ni kuzima Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), inayofanywa na chama hicho.

Kikao hicho kinafanyika ikiwa wiki moja imepita, tangu polisi walipodaiwa kumuua Mwangosi aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni, Channel Ten mkoani Iringa.

Mwangosi aliuawa na mlipuko unaoaminika kuwa ni wa bomu, ambao ulisambaratisha vibaya viungo mbalimbali vya mwili wake Septemba 2 mwaka huu, katika eneo la Nyololo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wakati akiripoti tukio la Chadema kufungua matawi yake.

Inadaiwa kuwa bomu hilo lilipigwa na polisi waliokuwa wakijaribu kuusambaratisha mkutano wa Chadema.

Mwangosi alizikwa siku moja baadaye katika Kijiji cha Kasoka kilichoko wilayani Rungwe, Mbeya.

Hadi sasa askari watano wa Jeshi la Polisi akiwamo anayetuhumiwa kumlipua Mwangosi kwa bomu, wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo mkoani Iringa.

Kukamatwa kwa askari hao kulifanyika siku moja baada ya kubainika kuwa askari kadhaa walioendesha operesheni dhidi ya wafuasi wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha Mwangosi, walitoka mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro.

Taarifa hiyo ya Chadema ilieleza kuwa mbali na Mwangosi, pia hivi karibuni mjini Morogoro polisi walisababisha mauaji ya mfuasi wa chama hicho, Ali Singano (Zona) baada ya kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wao waliokuwa wakijiandaa kuwapokea viongozi wa kitaifa waliokuwa na ratiba ya kufanya mkutano wa hadhara mjini humo.
“Baada ya tukio hilo chama kilitoa kauli kumtaka Rais Jakaya Kikwete aagize kutumika kwa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) ili kubaini chanzo na kuondoa utata wa kifo cha kijana huyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Hivi karibuni yametokea mauaji ya Mwangosi, chama kilimtaka Rais Kikwete aagize kufanyika uchunguzi huru kupitia tume ya kimahakama kwa kuwa katika tukio hilo, hakukuwa na utata kuwa mwandishi huyo aliuawa na polisi.”

Ilieleza kuwa ilitakiwa ufanyike uchunguzi katika matukio hayo, ili kubaini vitu vya ziada, kama vile ukiukwaji mkubwa wa Katiba, haki za binadamu na sheria za nchi na aliyetoa amri za mauaji hayo.

Ilieleza kuwa chama hicho kilipinga kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa sababu iliundwa kinyume cha sheria ya tume za uchunguzi.

“Lengo la kuundwa kwa kamati hii ni kufunika mambo na kurejesha uhusiano wa Serikali na vyombo vya habari, badala ya kutafuta ukweli. Kwa mara nyingine tena chama kilimtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria ili kweli ujulikane,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza:

“Chadema kiliahirisha Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mjini Iringa, kikisisitiza kauli yake ya kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati, kuhakikisha analinda Katiba ya nchi inayotambua haki ya kuishi.”

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kutokana na Rais Kikwete kuwa kimya hadi sasa kuhusu matukio ya mauaji yanayofanywa na polisi, Chadema kimeamua kuitisha mkutano wa dharura, kujadili hali hiyo na kutoa uamuzi dhidi ya polisi.

“Tutatoa uamuzi wa hatua zaidi za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi na Serikali inayoongozwa na CCM, kwa manufaa ya taifa letu na Watanzania wote kwa ujumla,” ilieleza taarifa hiyo.

Mtei
Naye Moses Mashalla kutoka Arusha, anaripoti kuwa mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Rais Kikwete ashtuke na kusema jambo kuhusu mauaji ya Mwangosi.

Akizungumza akiwa nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha, Mtei alishangaa ukimya wa Rais Kikwete baada ya mauaji hayo, akisisitiza kwamba ukimya wake utaifanya nchi isitawalike.

“Ni lazima Rais Kikwete aseme jambo. Ni lazima kama mkuu wa nchi ashtuke, mimi nashangaa ukimya wake juu ya mauaji haya, nchi hii haitaweza kutawalika,” alisema Mtei.

Hata hivyo, alibainisha kuwa taifa haliwezi kuwa na polisi wanaolenga vichwa vya watu na kuwaua badala ya kuwalinda wao na mali zao.

Alitoa wito kwa Serikali kuwanyang’anya polisi wote nchini silaha za moto na kuwakabidhi silaha za plastiki, maji ya kuwasha, virungu pamoja na pingu pekee kwa kuwa wameshindwa kudhibiti matumizi ya silaha za moto.

Mtei, aliyewahi kuwa gavana wa Benki Kuu nchini, alitoa wito kwa askari wote waliohusika na mauaji ya mwandishi huyo sanjari na vigogo wa Jeshi la Polisi waliotoa amri ya kutekeleza mauaji hayo kujiuzulu mara moja kwa kuwa taifa linakoelekea ni kubaya.

“Hatuwezi kuwa na polisi wanaolenga vichwa vya watu, taifa linaelekea kubaya. Polisi hawa wanyang’anywe silaha za moto kwa kuwa hawajui matumizi yake,” alisisitiza Mtei.
 
Back
Top Bottom