Bila kuficha kuonesha hisia zangu za kisiasa, ni ukweli usiopingika kuwa CDM kwa sasa ina nguvu kubwa sana hapa nchini. Endapo chaguzi zitafanyika kwa mazingira ya haki na usawa sioni chama chochote kitakachothubutu kushindana nacho hasa upande wa Tanzania Bara. Kwa maoni yangu ipo haja kuheshimu matakwa ya wananchi hasa kuhusu kile wanachoamini kuwa Chama kitakachowavusha kuelekea ngazi nyingine ya Maendeleo. Yalitokea Zambia, Malawi, Kenya, Afrika Kusini, na kwingineko kwa hiyo si ajabu yakatokea hapa Tanzania. Mabavu sio suluhu, ila nguvu ya wenye nchi (Wananchi) ndio jibu. Changamoto waliyonayo CDM ni kututoa Watanzania hofu ya haya yafuatayo; 1: Ina Mipango gani ya kuivusha nchi kuelekea uchumi imara unaogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania ambaye siku zote amekuwa mhanga wa harakati za uchumi wa kibeberu? 2. Ina Mkakati gani wa kushughulikia tatizo linalokuwa kila siku la ukosefu wa ajira kwa nguvu kazi ya taifa yaani VIJANA? Nini msimamo wa Chama katika kushughulikia Raslimali za Taifa (Gesi na Madini mengineyo?) na mwisho, ni vema tukajua mikakati iliyopo katika kuboresha huduma za kijamii mfano Afya, Elimu na Maji. Kama uchaguzi ungefanyika leo, nisingeona tabu kuwapa CDM kura yangu.