Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wilaya ya Arusha kimetoa ubani wa shilingi 200,000 kwa jeshi la polisi mkoani Arusha kwa ajili ya rambirambi ya kifo cha Askari polisi wa kitengo cha upelelezi, Kijanda Mwadu aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mtu anayetuhumiwa kuwa jambazi sugu wakati polisi walioongozwa na Mkuu wa upelelezi wilaya ya Arusha, Fautine Mafwele walipokuwa katika harakati za kumtia mbaroni eneo la kijiji cha Shangarai wilayani Arumeru.
KKatika tukio hilo, OC-CID pia alijeruhiwa kwa kupigwa risasi begani na kulazwa katika hospitali ya Seliani kwa matibabu.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro aliyeongoza viongozi wa Chadema katika hafla fupi ya kukabidhi ubani huo kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alisema chama chake kimetoa kiasi hicho kutokana na kuthamini mchango wa askari polisi katika harakati za ulinzi na usalama wa raia na mali zao kama alivyofanya marehemu Kijanda aliyekuwa tayari kukabiliana na wahalifu hadi kwa gharama ya maisha yake.
Kwa upande wake, RPC Andengenye alikishukuru chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kuelezea kitendo hicho kama kufungua njia mpya ya ushirikiano kati ya jeshi lake na Chadema na kuonyesha jamii kuwa pande hizo mbili hazina uhasama kama baadhi ya watu wanavyofiri.
Picha ya tukio hilo hapa chini
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye (katikati) akiwa katika picha ya pomoja na viongozi wa Chadema wilaya ya Arusha mara baada ya kupokea ubani wa shilingi 200,000 zilizochangwa na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika Januari 5, mwaka huu katika viwanja vya NMC, Unga Ltd Manispaa ya Arusha kuadhimisha mwaka mmoja wa mauaji yalitokea baada ya jeshi la polisi kuwafuatulia risasi wananchi katika harakati za kuzuia amaandamano hayo ambayo awali yaliruhusiwa kabla ya kupigwa marufuku Saa chache kabla ya kufanyika. Wemgine pichani kutoka kushoto ni Diwani wa kata ya Nagarenaro, Isaya Doita, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro, mjumbe wa kamati tendaji wilaya, Sarah Fundikira na mwenyekiti wa Bawacha wilaya ya Arusha, Gloria hio.
RPC Andengenye akipokea kitita cha shilingi 200,000 kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha), wilaya ya Arusha, Gloria Shio ikiwa ni ubani kutoka Chadema kufuatia kifo cha askari polisi, Kijanda Mwadu aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mtu anayedaiwa kuwa jambazi sugu katika tukio lililotokea kijiji cha Shangarai wilayani Arumeru. Anayeshuhudia kushoto ni mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro ambaye pia ni diwani wa kata ya Levolosi