CCM kushirikiana na CUF Zbar ni uamuzi wa wananchi

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
Tuesday, 01 March 2011 21:19
bbbseif.jpg
Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Seif Sharif Hamad

Joyce Mmasi
HAKUNA shaka kwamba Watanzania ni watu wenye uwezo wa kuona na kutambua mbivu na mbichi. Uzuri ni kuwa hawaishii kuona na kutambua, bali pia husema panapokuwa na haja ya kufanya hivyo.

Ni dhahiri kwamba mambo kadhaa ambayo yamejitokeza katika medani ya siasa ya nchi yetu kwa siku za karibuni ni ushahidi wa mambo kwamba Watanzania si watu wa kudanganyika.

Wanasiasa wetu, mashabiki au wapenzi wao, wanatambua kwamba hali ya mambo inayoendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba, hasa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inaipa siha siasa ya sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kwa miaka michache iliyopita ilikuwa katika majaribu makubwa.

Lakini, si wote wanaokubaliana na msimamo wa vyama viwili vikuu kule kisiwani, CCM na CUF kuwa na ushirikiano.

Kwa mfano, kitendo cha viongozi wa Chadema kuwakebehi CUF kufuatia ushirikiano wao na CCM katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kule kisiwani Zanzibar siyo cha kupongezwa.

Msimamo huo, kwa mtazamo wangu ni dharau au kejeli kwa Wazanzibari. Lakini, zaidi naweza kusema ni wivu wa mafanikio wa wazi unaoonyeshwa na chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania Bara dhidi ya wenzao wa CUF ambao wanaonekana kufanikiwa katika suala zima lililosababisha maafikiano ambayo pia yamewezesha kufanyika mabadiliko makubwa yakiwamo ya katiba yaliyowezesha kufikiwa maamuzi ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Ni dharau na kejeli kwa kuwa CUF haikukaa na kuomba kushirikiana na CCM isipokuwa ni mchakato wa wazi na wa muda mrefu uliofuatiwa na mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliyofanyika baada ya asilimia zaidi ya 60 ya Wazanzibari kuridhia mabadiliko hayo.

Kimsingi yale hayakuwa maamuzi ya CUF au ya Maalim Seif Shariff Hamad, Amani Abeid Karume au Rais Jakaya Kikwete kama ambavyo Chadema wanataka kuwaaminisha wafuasi wao.

Hivyo, kuishutumu CUF ni kupuuza nafasi ya wananchi wa Zanzibar walioamua kufanya mabadiliko na kutaka dunia iamini kuwa vyama vya CUF na CCM ndivyo vilivyoamua suala hilo kubwa bila kuwashirikisha wananchi.

Unaweza kuitwa wivu wa mafanikio kwa kuwa ushirikiano ule wa CCM na CUF katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa umeonyesha mafanikio makubwa yaliyoisababisha Zanzibar kuwa shwari, jambo ambalo sina shaka kwamba litaipa nafasi ya kupiga hatua kimaendeleo.

Ni ukweli usiopingika kwamba mwafaka uliosababisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar umeibadili Zanzibar kisiasa, kijamii na hali itakwenda mbali zaidi katika mabadiliko ya kiuchumi.

Kabla ya CCM na CUF kufikia muafaka uliozaa serikali ya umoja wa kitaifa, nchi hiyo naweza kusema ilikuwa na machafuko, uhasama ambao ni vigumu kuusahau.

Watu walichukiana na hawakushirikiana kabisa, iwe katika shida au raha. Ilikuwa ni nadra kwa CCM au CUF kushirikiana na mtu yeyote hata kama ni mwandishi wa habari endapo ataonekana kuwa na ukaribu wa aina yoyote na upande mmoja katika vyama hivyo.

Kilichokuwa kikifanyika Zanzibar kabla ya mwafaka, hakikuwa siasa, ilikuwa ni chuki, uhasama, visasi, na kila aina ya ubaya dhidi ya upande mwingine.

Haikuonekana ajabu kwa upande wowote uwe wa viongozi au wafuasi wa vyama hivyo kufurahia mateso au hata maumivu yanapoufika upande mmoja.

Kwa ufupi ni kuwa hali ilikuwa mbaya sana na ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndiyo iliyorejesha mshikamano, amani, upendo na ushirikiano baina ya watu wa visiwa hivyo.

Kufuatia hali iliyopo sasa katika visiwa vya Unguja na Pemba, nilidhani mtu yeyote, awe kiongozi au mwananchi wa kawaida na anayependa amani na utulivu ataifurahia.

Niliamini viongozi wetu wasingeishia kufurahia na kupongeza pekee, bali wangeenda mbali zaidi kwa kuiga jambo lile jema na kuungana pamoja kudai au kushawishi kile kilichofanyika Zanzibar kiweze kufanyika pia na hata hapa bara.

Siyo katika kushirikisha pekee, bali kuungana kudai katiba mpya itakayotoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uchaguzi katika hali ya uhuru na uwazi, na kwamba chama kitakachopata idadi ya kura au ya wawakilishi kiweze kuwa na uwezo wa kushiriki kuunda serikali kama ilivyo Zanzibar.

Baada ya hayo kushindwa kufanyika Chadema inasimama kifua mbele kujaribu kubeza juhudi za CUF na CCM za kuleta amani Zanzibar.

Ninadhani kuwa badala ya Chadema kuendelea kuwakebehi wenzao wa CUF, wangepaswa kuwapa heshima yao stahiki kwa mchango wao wa kuleta mageuzi ya kisiasa nchini.

Kadhalika Chadema wanapaswa kufahamu kuwa wabunge wa CUF kutoka Zanzibar si sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Wanapaswa wafahamu kuwa umoja kama huo uko katika nchi mbalimbali duniani, kwa mfano Ujerumani, chama tawala kinaweza kushirikiana na chama cha upinzani katika jimbo fulani na kushirikiana na chama kingine katika jimbo jingine kwa kutegemea ni chama gani kilichokubaliwa na wananchi. Hizo ndizo serikali za umoja wa kitaifa zilivyo.

Kitendo cha Chadema binafsi naweza kukiita kuwa ni uchanga wa kisiasa, wanapaswa wasome kwa wengine, mbona mifano iko mingi?

Joyce Mmasi ni mwandishi wa Makala wa gazeti la Mwananchi.
0714 233929
 

Attachments

  • asset.jpg
    asset.jpg
    3.5 KB · Views: 35
Hawa CUF wanajisahau sana. CCM watatumia vizuri sana mwanya huu kuhakikisha wanarejesha imani ya wananchi wa pemba kwao, then 2015 ndo inakuwa mwisho wa serikali ya umoja wa kitaifa.
 
Hawa CUF wanajisahau sana. CCM watatumia vizuri sana mwanya huu kuhakikisha wanarejesha imani ya wananchi wa pemba kwao, then 2015 ndo inakuwa mwisho wa serikali ya umoja wa kitaifa.

unawasemea wazanzibar?
 
Back
Top Bottom