ccm ijivue gamba mapema | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

ccm ijivue gamba mapema

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mujumba, Mar 15, 2011.

 1. Mujumba

  Mujumba JF-Expert Member

  #1
  Mar 15, 2011
  Joined: Jan 20, 2011
  Messages: 854
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  HEKIMA itumike katika uamuzi wa mawaziri, mambo nyeti yazungumzwe katika Baraza la Mawaziri na wajiwekee utaratibu wa kufuatilia uamuzi wao … Serikali inapoonekana kuyumba, wanaotaka nchi isitawalike, watapata fursa ya kufanikisha malengo yao.”

  Hiyo ni kauli ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kwa waandishi wa habari hivi karibuni Dar es Salaam, alipokuwa akizungumzia hali ya nchi inavyokwenda kisiasa.

  Lakini siku chache baadaye, Jumuiya ya Vijana wa CCM Mkoa wa Pwani, haikutafuna maneno pale ilipowanyooshea kidole mawaziri, ikiwapasulia kuwa hawamsaidii Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho.

  Wakasema mawaziri hao wamekuwa wakijiweka pembeni na kushindwa kutetea mambo yanayokosolewa, ukiwamo mfumuko wa bei, huku wakiwa na maelezo juu ya suala hilo.

  “Viongozi hao wakiwamo mawaziri, wamekuwa kimya hata pale wanapoona yapo mambo wanayoweza kuyatolea ufafanuzi kabla ya Rais … hawafanyi hivyo na kumwachia Rais aeleze na kutetea kila jambo.” Ni kauli ya vijana hao.

  Lakini hawakuishia hapo, wakawavaa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, kwamba wanaikosoa CCM na Serikali yake bila kufuata utaratibu na kwamba hatua hiyo inachochea machafuko nchini.

  Inaonekana hapa UVCCM na Lipumba, wanasafiria chombo kimoja, kwa sababu fikra zao zinaoana kwa kiasi kikubwa.

  Wote wanataka taratibu zifuatwe katika kujadili masuala nyeti yanayohusu Serikali, kwamba yajadiliwe katika vikao rasmi na kufikia uamuzi ambao watausimamia kikamilifu.

  Lipumba hapa anaisaidia CCM kuweka sawa mambo yake, hasa wakati huu ambao inajiandaa kujivua gamba na kuzaliwa upya kama afanyavyo nyoka; kuwang’oa wasiostahili na kuingiza ambao wanakubalika na jamii ya vijana ambao ndio wanaotawala siasa za leo

  Mimi nakubaliana kabisa na hoja hizi za UVCCM na Lipumba, kuwa ni vyema kujadiliana masuala muhimu katika vikao, hasa inapoonekana kuwa kuyaweka hadharani ni kujivua nguo na kila mtu kuona na kujua ukurutu au kovu ulilonalo.

  Lakini pia si yote yanayopaswa kujadiliwa kwa faragha vikaoni, hasa wanaofikishiwa ujumbe wanapokuwa wazito au wagumu kuelewa na kukubali wanayoshauriwa. Na kama hali ndivyo ilivyo, sioni tatizo la akina Sumaye na Lowassa.

  Hata Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa nje ya madaraka, alipokuwa anaona mambo hayaendi sawa ndani ya CCM na Serikali yake, hakusita kuita wanahabari na kuzungumza na Taifa kupitia kwao na hivyo ujumbe kufika.

  Sikupata kusikia hata mara moja si CCM au vijana, kuibuka na kushutumu kauli za Mwalimu kuwa anaikosoa CCM na Serikali yake bila kufuata vikao rasmi vinavyokubalika; pengine ni kwa sababu Nyerere aliheshimiwa sana au kuogopwa.

  CCM ina kazi kubwa na nzito katika kujivua gamba hivi sasa, kwa sababu baadhi ya magamba yanaweza kuwa muhimu kwake na hata kuondoka kwao kukaiathiri na kuunufaisha upinzani.

  Pia yapo magamba ambayo ni muhimu lakini kuwapo kwao kukaendelea kuigharimu CCM hivyo inapaswa imeze kidonge kichungu ili ipone na kwa kuwa wapo viongozi ndani ya CCM wanadhani ni bora na wakiondoka wataitikisa, pengine ndiyo sababu ya kuwapo chokochoko hizo.

  Kinachotakiwa ni CCM kutafuna jongoo kwa meno na kupuuza makunyanzi na kuwaacha watakaohamia kwingine wafanye hivyo kungali mapema, ili ijipange sawasawa, kwa sababu si siri kuwa ni kweli wapo wasioisaidia bali kuikandamiza kwa maslahi binafsi.

  Na hao wasiomsaidia Rais ni bora nao wakaenguliwa mapema, ili wanaobaki na wanaoingia wajipange pia mapema, kwani kufanya hivyo ni bora kwa mustakabali wa CCM kuliko kuendelea kubaki na watu ambao hawaisaidii zaidi ya kuididimiza.

  Wahenga walisema mchelea mwana kulia hulia yeye, kwa sababu inaonekana kuna watu wanaoamini na kudhani kuwa hata iweje CCM haiwezi kuwaondoa kwa sababu kufanya hivyo ni kwa hasara yake, na wamejijengea usugu wa kutojali wayafanyayo kwa hasara ya CCM.

  Hivyo kama CCM itawachelea wao kulia italia yenyewe na ijue kuwa wapinzani wako pembeni wanaangalia kama kunguru anavyoshuhudia vita ya panzi.

  CCM bado ina nafasi ya kujibadilisha na kuwa mpya, hata kama gamba hilo litavuliwa na kuacha vidonda, ijue vitapona.
   
Loading...