CCM Haiwezi Kukwepa Lawama Katika Ujambazi wa Utoroshaji Madini Yetu

Mzalendo_Mwandamizi

JF-Expert Member
Dec 12, 2007
1,117
4,772
New-Doc-2017-05-25_17.jpg


Juzi tumesikia ripoti kuhusu mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya Tanzania yetu (well, kuna jina la kitaalamu lakini sio la muhimu kulinganisha na athari kubwa za usafirishwaji wa mchanga huo).

Kwa baadhi ya wenzetu, taarifa hiyo imewashtua mno, na kuwapandisha hasira kubwa. Ndio Tanzania yetu hiyo, wengi wa raia wake hawana habari kuhusu yanayoisibu nchi yetu. Ukiwauliza watu, "hivi mustakabali wa Tanzania mwakani utakuwaje?" nina hakika watu kadhaa watajiumauma kutoa jibu la kueleweka. Ukiwauliza kuhusu miaka 10 (au zaidi) ijayo, watakuona kama una matatizo ya akili. Ukiwauliza kwanini leo JK ni shujaa ilhali sote tunajua alivyoitenda Tanzania yetu 2005-2015, hutopata jibu la kueleweka. Tupo tupo tu!

Watanzania wengi aidha hawaelewi au wamesahau nchi yetu ilivyochukua mwelekeo mpya - na usiopendeza - baada ya kung'atuka kwa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Hatua ya kwanza kabisa ya kubadili mwelekeo ilikuwa kitu kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar. Hili lilifanyika katika utawala wa Mzee Ruksa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Kimsingi, Azimio la Zanzibar liliua Azimio la Arusha, na sio kuliua tu bali kuliua na kulizika mubashara. Ukitafuta nyaraka kuhusu Azimio hilo la Zanzibar hutozipata kirahisi kwa sababu lilifanyika katika mkusanyiko uliokuwa kama "mkutano haramu."



Mzee wetu Mwinyi hakuitwa Mzee Ruksa kama utani. Utawala wake ulitawaliwa na kile Waingereza wanaita 'laissez faire', labda kwa Kiswahili chepesi tuseme 'bora liende' au 'liwalo na liwe.'

Lakini kumtendea haki 'Mzee Ruksa,' asili hasa ya ufisadi haikuanza katika utawala wake bali ilianza katika utawala uliomtangulia, wa Baba wa Taifa.

Tofauti kati ya tawala hizo mbili ilikuwa bayana: Wakati baadhi ya waliomzunguka Baba wa Taifa walikuwa 'mafisadi wa chinichini' au 'waliokuwa wakisubiri atokea madarakani ili waanze kutafuna keki ya taifa,' katika utawala wa Rais Mwinyi, ilikuwa ni mwanzo wa 'kula kadri unavyoweza,' Waingereza wanaita 'open season.' Na ulaji huo ulifanyika with full knowledge of Mzee Ruksa.

Kwamba labda Baba wa Taifa alifahamu watu hao au walikuwa mahiri kuficha tabia zao, sina jibu la hakika. Lakini huhitaji kuwa mchambuzi mahiri wa siasa kubaini kwamba mara baada ya Nyerere kung'atuka na hatimaye kufariki, ghafla watu walewale waliokuwa wakiimba kuhusu Ujamaa na kulaani Ubepari wakageuka matajiri wa kupindukia, mabepari. Ninachofahamu ni kwamba kulikuwa na idadi kubwa tu ya wanasiasa waliomhadaa Baba wa Taifa kuwa ni waumini wa Ujamaa lakini walimudu kuhifadhi fedha huku nje wakisubiri 'Nyerere aondoke.'


Kwahiyo, Awamu ya Pili ya Mzee Ruksa ni kama iliyotoa ruksa kwa walafi waliokuwa wakimendea keki ya taifa, lakini walishindwa kuitafuna wakati wa utawala wa Nyerere. Kwa kifupi, utawala wa Mzee Ruksa ulitoa rasmi ruksa kulifisadi taifa letu, hasa kupitia Azimio la Zanzibar.

Ni muhimu kukumbuka Utawala wa Mzee Ruksa ulikuwa wa Chama Cha Mapenduzi, CCM.

Kuingia kwa Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995 kuliingiza zama mpya kuhusiana na ufisadi. Miaka 10 ya Mzee wa Uwazi na Ukweli ilitawaliwa na Watanzania kuhadaiwa kuwa ufumbuzi wa matatizo yao upo mikononi mwa wawekezaji, ilhali wengi wa hao walioitwa wawekezaji walikuwa in fact majambazi waliokuwa wakiwinda raslimali zetu.

Miaka 10 ya Mkapa ilileta matumaini ya kitakwimu, tukiambiwa kuwa sijui GDP, sijui Pato la Taifa, sijui vipimo gnai vya kiuchumi, kuwa vyote vilionyesha uchumi wa Tanzania ukifanya vizuri. Kama kuna kitu kinanichukiza mno kuhusu hizi takwimu za uchumi ni kuwaangalia watu kama bidhaa au namba na sio binadamu. Haiingii akilini kusema uchumi unakua ilhali watu wanazidi kuwa masikini. Uchumi unakua kimazingaombwe?

Tofauti kati ya utawala wa Mwinyi na Mkapa ni ya wazi: nimeshaeleza kuwa katika zama za Mwinyi ilikuwa 'ruksa' kufanya lolote lile. Zama za Mkapa zilituaminisha kuwa kila kitu kinafanyika kwa uwazi na ukweli, na kwenye uwazi na ukweli hakupaswi kuwa na ufisadi.

Yaliyojiri katika utawala wa Mwinyi yalikuwa yakionekana mubashara. Hiki kilikuwa kipindi cha mtu tu kuamua kuwa tajiri kwa njia halali au zisizo halali, maana ilikuwa ruksa. Lakini katika zama za 'uwazi na ukweli,' watu pekee walioonekana kuwa na ruksa ya kufanya wapendayo ni wawekezaji.Mkapa aliwathamini wawekezaji kuliko Watanzania wenzake.


Lakini ni baada ya Mkapa kutoka madarakani ndio tukafahamu kilichokuwa kikijiri 'behind the scene.' Kumbe wakati anatuhubiria kuhusu uwazi na ukweli, yeye akaigeuza Ikulu kuwa soko la Kariakoo, akawa anafanya biashara.

Na Mkapa, mwanafunzi mtiifu wa Mwalimu Nyerere, ni mfano sahihi wa watu ambao Nyerere aliwaamini sana lakini alipoondoka nao wakapuuza misingi aliyoijenga Mwalimu.

Zama za Mkapa ndio haswa zilizowavutia wawekezaji kujazana nchini mwetu. Wengi wao walikuja na brifukesi tupu, wakaondoka na mamilioni ya dola. Baadhi ya wawekezaji hao, walipoona bado wanahitaji kuchuma wasichopanda, walibadili majina na kuongezewa likizo ya kulipa kodi.



Ni muhimu kukumbuka kuwa Mkapa alikuwa Rais kwa tiketi ya CCM.

Baada ya Mkapa akaingia Kikwete. Ili kuorodhesha madudu yote yaliyofanywa katika utawala wa Kikwete inahitaji kitabu kizima. Wakati mwingine unaweza kupatwa na kizunguzungu kuona sasa Watanzania wengi wanamlilia JK, mwanasiasa ambaye hakuwa makini kabisa kuhusu mustakabali wa Tanzania yetu.

Ni hivi, kuna mengi hayawekwi wazi kuhusu yaliyojiri kati ya 2005 na 2015, na siku yakiwekwa hadharani itakuwa balaa. Bwana Magufuli aliposema 'tusifukue makaburi' alitumia busara tu ili kuepusha aibu ambayo kimsingi isingekuwa kuhusu utawala wa JK tu bali mwendelezo wa CCM kuwa janga kwa taifa letu.

Kutoka EPA hadi Kagoda hadi Richmond hadi Escrow, utawala wa JK ulitawaliwa na skandali mfululizo. Pengine JK hakuwa mwanasiasa mwenye mapungufu lakini kosa lake kubwa lilikuwa maandalizi yake kuwania urais from 1995 to 2005, ambapo alikusanya sapoti ya kila kundi, ikiwa ni pamoja na mafisadi. lipopata urais, JK alikuwa na deni kubwa kwa watu hawa, na hii ilipeleka awaruhusu kutafuna keki ya taifa kama asante yake kwao.



Sihitaji kukumbusha kuwa JK alikuwa Rais kwa tiketi ya CCM.

Magufuli pia ni Rais kwa tiketi ya CCM, lakini wakati tunapongeza jitihada zake binafsi ni muhimu kutambua kuwa chama chake kina mchango mkubwa katika matatizo mengi yanayotukabili leo, ikiwa ni pamoja na hilo la utoroshaji wa mchanga wa dhahabu.

Lakini Magufuli hawezi kukwepa lawama kwa uamuzi wake kumteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyolazimika kujiuzulu katika utawala wa JK kutokana na kashfa ya Escrow. Hivi Magufuli alikuwa anategemea miujiza kutoka kwa Prof Muhongo?

Kwa waliosoma kitabu changu cha 'Dokta John Magufuli: Safari ya Urais, Mafanikio na Changamoto Katika Urais Wake' watakumbuka nilichoandika ukurasa wa 74 kuhusu uamuzi wa Magufuli kumteua Profesa Muhongo.

5188-dokta-john-magufuli.jpg



Niliandika

20170524_150544.png



Hata hivyo, angalau Magufuli amejitahidi kufanya jitihada binafsi kukabiliana na majambazi wanaobaka uchumi wetu. Ile tu kuchukua hatua inapaswa kupongezwa hasa ikizingatiwa kuwa watangulizi wake watatu -Mwinyi,Mkapa na JK - waliishia kutupatia matumaini hewa huku ufisadi ukizidi kushamiri.



Jana nilimwangalia Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Poplepole akitoa maneno mazito kuhusiana na suala la mchanga wa dhahabu. Nikaandika tweet kwamba Bwana Polepole anaongea kana kwamba CCM haihusiki na kuwezesha ujambazi uliopelekea mchanga wa madini kusafirisha. Akaleta uzushi kuwa sijui mie nipo ughaibuni, sijui sina uhalali. Baadhi ya watu wakamshutumu kuwa ni mbaguzi (kuwa ughaibuni hakuninyimi uhuru wa kuzungumzia mustakabali wa taifa letu) lakini mie siamini kabisa kuwa huyu Polepole ni mbaguzi. Ni siasa tu.

Mwisho, makala hii haitokamilika ipasavyo bila kuwatupia neno ndugu zangu wa "kitengo." Hebu fanyeni kuona aibu japo kidogo. Hivi inawezekanaje taifa kuibiwa zaidi ya shilingi trilioni moja ilhali ninyi mkifaidi mishahara minono na posho nzuri inayotakana na jasho la Watanzania masikini lakini mnawaangusha kiasi hicho? Tatizo la kitengo ni vipaumbele fyongo, kuandama watu wasiohusika badala ya kukwekeza nguvu dhidi ya wahalifu halisi/matishio halisi kwa usalama wa taifa letu.

Hata hivyo, kwa vile lawama hazijengi, ni matumaini yangu makubwa kuwa suala hilo la mchanga wa dhahabu litatufungua mcho kama taifa na kukabiliana na ujambazi wa aina hii. Sina uhakika sana kuhusu mbinu mwafaka, lakini pengine kwa kuanzia, CCM hata kama inaona aibu kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwa kichaka cha ufisadi, hali iliyowezesha ujambazi wa mchanga huo wenye madini, basi angalau imuunge mkono mwenyekiti wao, si kwa porojo za kina Polepole bali kwa vitendo halisi. Wingi wa wabunge wa chama hicho tawala uwe na faida kwa wananchi na taifa na sio mhuri wa kupitisha kila kitu kama ilivyokuwa kwa miswada iliyopeleka sheria za madini zinazowapa fursa wawekezaji wasio waaminifu kutorosha kila wanachotaka ilhali sie tukizidi kuwa masikini.

Mungu ibariki Tanzania
 
Back
Top Bottom