Buriani simu feki, siku zako zinahesabika

Buriani simu feki, siku zako zinahesabika

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,086
ZIMEBAKI siku nne kabla ya simu feki kufungiwa. Iwapo hufahamu kama simu yako ni feki au orijino, unachotakiwa kufanya ni ni kubonyeza *#06# ili upate namba ya IMEI. Kisha hiyo IMEI namba uitume kwenda namba 15090 na utapokea ujumbe utakaokufahamisha kama simu yako ni feki au orijino.

Kumbuka kutuma ujumbe huo ni bure kabisa. Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imeshatamka Juni 16 mwaka huu, ndipo simu hizo feki zitafungiwa. Imesisitiza haitasogeza muda. Kwa hiyo ukiona tarehe hiyo hunipati kwa kupiga simu, kutuma meseji au kuchati kwenye mitandao ya kijamii, basi ujue ‘simu yangu imekatwa’. Wale wenye simu feki, uamuzi huo wa TCRA utatufanya tubaki tukisimulia , hapo zamani za kale, kulikuwa na simu feki ambazo zilisheheni madukani, zikiuzwa bila kificho.

Tutasimulia ilivyotuwia vigumu kutambua simu feki kutokana na kutotofautiana na zile halali. Ingawa baadhi ya watu walidhani simu feki ni lazima ziwe zinazouzwa bei ya chini, bado nyingine ziliuzwa ghali kwa madai kuwa ni orijino. Wapo walioamini kwamba, maduka yaliyoko maeneo fulani ndiyo maalumu kwa uuzaji wa simu feki na mengine ndiyo yenye bidhaa halisi; lakini bado ilikuwa dhana potofu. Hakika simu feki ilikuwa janga.

Wananchi wengine waliingia mkenge kwa maana ya kununua simu feki bila kujua na wapo waliozinunua kwa utashi wao kutokana na bei kuwa ndogo. Baada ya TCRA kuelimisha umma kwa kutoa kanuni ya kugundua simu feki, ndipo wengi waligundua simu zao ni feki.

Wakati wapo watu ambao wameshanunua simu mbadala kabla ya Juni 16, wapo ambao hadi sasa hawajanunua ama kutokana na ukosefu wa fedha au bado wanasikilizia kuona kama TCRA itafanya kweli.

Kwa muktadha huo, siku ya TCRA kuzima simu feki, zitashuhudiwa kauli zenye maswali, shutuma na hata kulaani kitendo hicho. Upo uwezekano mkubwa wa hasira ya kukosa mawasiliano, kuwaelekeza baadhi ya watu kuishutumu TCRA kuwa imewashtukiza.

Hawatakosekana watakaodai kuwa hawakupewa taarifa mapema na hivyo kuomba muda wa kuwazimia usogezwe ili wajiandae. Hata hivyo, katika hili la elimu na taarifa, naitetea TCRA kwani imefanya kazi yake vyema kufahamisha umma.

Katika kudhihirisha hilo, ndiyo maana hivi karibuni, baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya simu jijini Dar es Salaam, walikaririwa wakisema idadi ya wateja imepungua kutokana na wengi kusubiri muda ufike, wawe na uhakika wa simu bora za kununua. Wafanyabiashara walidai wateja wengi hawanunui simu wakihofu kununua feki na zisizo na viwango ambazo zitazimwa ndani ya muda mfupi ujao.

Inadaiwa wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao walishaingiza simu hizo feki, wameanza kuzisafirisha kwenda kuziuza nchi jirani ambako hazina kizuizi. Ikiachwa watakaodai kwamba hawakupewa taarifa na elimu ya kutosha, wapo watakaolalamikia hatua ya wafanyabiashara kuachwa wakaingiza bidhaa zisizokidhi viwango na hatimaye kuingiza wananchi kwenye usumbufu wa kuzimiwa simu zao.

Watahoji serikali ilikuwa wapi hata ikashindwa kudhibiti uingizaji wa simu hizo? Watataka kujua ilikuwaje simu hizo hatari kwa matumizi ya binadamu zikapitishwa kwenye mipaka, bandari na viwanja vya ndege na kusababisha walaji kupata bidhaa feki?

Watahoji Shirika la Viwango (TBS) lilikuwa wapi kiasi cha bidhaa feki kutawala soko la nchini? Watalalamikia hasara ambayo wananchi wameingia na kulazimika kununua simu nyingine.

Siyo tu hasara ya kifedha, bali pia hasara ya kukosa mawasiliano kwa wale ambao hawatakuwa na fedha za kununua simu mara moja. Watatamani serikali ifidie wananchi walioathirika. Hakuna ubishi, wenye malalamiko hayo wako sahihi ingawa naamini mamlaka zinazohusika, zinaweza kujieleza kwa namna moja au nyingine kwa lengo la kujivua lawama. Lakini lazima ukweli ubaki kwamba, upo uzembe uliosababisha simu feki kutawala soko la ndani.

Pamoja na ukweli huo, lazima tukubali ‘muarobaini’ wa simu feki nchini upatikane japo ni mchungu. Umma wa Watanzania hauna budi kukubaliana na uamuzi huu wa kudhibiti simu feki licha ya kwamba unauma. Lazima Watanzania wakubali uamuzi huu kwani ndiyo tiba ya kudumu ya uingizaji, usambazaji na uuzaji wa simu feki zinazohatarisha usalama wa wananchi.

Laiti kama kungekuwa na teknolojia au mfumo mwingine wa kufungia bidhaa zote feki zilizoko kwenye masoko! Ingawa wapo wengi watajikuta wakipoteza mawasiliano kutokana na simu zao kuwa feki, tuiunge mkono TCRA na kukubali ukweli kwamba kufungia simu feki ndiyo suluhu la kudumu ya tatizo.

Ushauri wangu kwa TCRA ni kuwa macho dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza siku hiyo ikiwemo kufungia simu ambazo siyo feki na hivyo kuzua malalamiko mengi.
 
Back
Top Bottom