Bunge la Katiba moto

Bunge la Katiba moto

nngu007

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2010
Posts
15,860
Reaction score
5,803
010812.jpg




JUMAPILI, FEBRUARI 09, 2014 08:54 NA WAANDISHI WETU

KUTANGAZWA kwa orodha ya majina ya wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, kunakotoa fursa ya kuitishwa kwa Bunge hilo wiki ijayo, sasa ni dhahiri kumeibua joto lingine jipya.

Tayari yapo mambo kadhaa yaliyobainika ambayo baadhi ya watu wanasema kuwa ama yanaweza kupandisha joto, au kuvuruga kabisa Bunge hilo la Katiba, lililopangwa kuanza kuketi Februari 18, mwaka huu.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwemo kwa majina ya baadhi ya wajumbe walioteuliwa kwenye Bunge hilo ambao wanatajwa kuwa ni mawakala wa watu wanaousaka urais mwaka 2015.

Muundo wa serikali tatu ambao umeendelea kusisitizwa kwenye Rasimu ya Pili iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge hilo, ni jambo lingine linalotazamwa kuibua moto mkali ndani ya Bunge.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wakati akikabidhi Rasimu ya pili ya Katiba, alisema kuwa muundo wa serikali tatu umezingatia maoni ya watu wengi, jambo lililoonekana kuvifurahisha vyama vya upinzani, hususan Chadema na CUF, huku likiikera CCM, ambayo imekuwa iking’ang’ania kubaki na muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Ni kwa msingi huo huo wa aina ya muundo wa Muungano, baadhi ya wagombea wanaotajwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wanadaiwa kufanikiwa kupenyeza mawakala wao ndani ya Bunge hilo, kwa kazi ya kujenga makundi yatakayopigania maslahi yao.

Gazeti hili limebaini kuwa miongoni mwa hao wanaotajwa kuwa ni mawakala wa wagombea urais ambao wamefanikiwa kuteuliwa ndani ya Bunge hilo la Katiba, wamo wale ambao hivi karibuni wamesikika wakilumbana hadharani kuhusu hofu ya kuwako kwa harakati za Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwania urais mwaka 2015.

Baadhi ya wanasiasa wanaousaka urais wanaamini kwamba chini ya mfumo wa serikali tatu, Rais wa Tanzania hatakuwa na nguvu kama alizonazo sasa Rais Jakaya Kikwete.

Wakati hilo likielezwa hivyo, jambo lingine ambalo linaweza kuibua moto mkali ndani ya Bunge hilo la Katiba ni hoja ya Tanganyika huru, hasa ukichukulia kwamba muasisi wa hoja hiyo naye, Mchungaji Christopher Mtikila, amejumuishwa ndani ya Bunge hilo.

Tayari, Mtikila ameweka bayana msimamo wake juu la suala la Tanganyika, na ameapa kwenda Mahakamani endapo hoja aliyopanga kuitoa wiki ya kwanza ya Bunge hilo itabezwa.

Mchungaji Mtikila, ambaye amekuwa na msimamo wa kudai serikali ya Tanganyika kwa miongo na miongo, alisema mara atakapofika Bungeni katika kikao cha kwanza, atatoa hoja ya kutaka iundwe kwanza Katiba ya Watanganyika na endapo hatasikilizwa, itampa urahisi wa kufungua kesi ya kudai Tanganyika huru.

Wakati hayo yakitokea kwa upande wa nyuma, kwa upande wake, Chama Kikuu cha Upinzani nchini, Chadema, kimeahidi kuzungumzia uteuzi wa wajumbe hao wanaounda Bunge hilo leo au kesho, baada ya kufanya uchambuzi wake wa kina.

“Kwa sasa ni mapema kama chama kutoa msimamo wetu, sasa hivi wataalamu wetu wanachambua jina kwa jina, nani katoka wapi na mwisho kabisa tutatoa tamko letu juu ya uteuzi huo, tunaweza kutoa kesho (leo) au kesho kutwa,” alisema Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.

Kwa upande wao wasomi, licha ya kupongeza uteuzi huo kwa kuzingatia usawa, wamelitaja suala la aina ya muundo wa Muungano kuwa ni hoja kubwa ambayo itasumbua ndani ya Bunge hilo la Katiba, huku pia wakiwa na hofu ya wanasiasa kuingiza matakwa yao.

Dk Bana

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema wazi kuwa suala la muundo wa Muungano itakuwa ni hoja itakayolisumbua Bunge la Katiba na hiyo inatokana na kile alichoeleza kuwa ni misingi ya dhambi ya uasili ambapo Zanzibar tayari wana Katiba yao inayowatambulisha kama nchi kamili.

Kutokana na hilo, alisema suala la serikali mbili au tatu litasababisha mjadala mrefu ndani ya Bunge na pengine kulivuruga kabisa, kwa sababu tayari Zanzibar wametia mtego katika suala la Muungano na hivyo kushauri wajumbe wa Bunge hilo kutokwepa maoni ya Tume ya Jaji Warioba.

Akizungumzia uteuzi wa wajumbe wa Bunge hilo, alisema umezingatia usawa kwa makundi yote ya wanasiasa, wasomi pamoja na wanajamii.

“Tena ningefurahi kama Dk. Slaa naye angejumuishwa, naamini kabisa Bunge la Katiba linaweza kuja na kitu chenye kueleweka kwa Watanzania na kufanya mchakato kuendelea vizuri.”

Dk. Bana alitahadharisha kuwa jambo muhimu linalofuata ni uteuzi wa Spika, kwa kusema kuwa inatakiwa ateuliwe Spika mwenye uwezo na busara nyingi za kuongoza watu kwa kusimamia misingi ya maridhiano.

Pia ametoa wito kwa wajumbe wote waende kwa mawazo ya kujitegemea, ili kuepusha ushabiki wa itikadi za vyama vya siasa.

Profesa Baregu

Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema suala la muundo wa muungano litawatikisa wajumbe wa Bunge hilo kama wakiamua kuanza nalo na hivyo kupendekeza kuanza na mambo mengine, ili wakifikia hatua ya kulijadili, watakuwa tayari wamejenga hali ya kuaminiana na kusikilizana.

Akizungumzia orodha hiyo inayounda Bunge la Katiba, alisema imeelekea kwenye usawa.

“Naona wajumbe hawa wanaelekea kwenye usawa, kwa kuwa baadhi yao siwafahamu walikotoka, tofauti na tume yetu ambayo iliundwa na watu wengi kutoka Dar es Salaam na Mjini Magharibi, lakini ushauri wangu ni kwamba wajumbe hawa walioteuliwa waende kwa fikra ya marekebisho ya maoni ya rasimu ya Tume na pia wafuate sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama tulivyofanya sisi,” alisema Profesa Baregu.

Profesa Safari

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari, alisema amefurahi kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba.

Sanjari na furaha hiyo, Profesa Safari alisema kuwa anakwenda kwenye Bunge la Katiba akiwa na hoja yake ya msingi, ambayo ni kuhakikisha suala la uchaguzi huru linapewa nguvu kubwa kwenye Katiba Mpya.

“Imezoeleka watu wenye shughuli nyingi ndio wale wale wanaopewa nafasi kama hizi, binafsi nashukuru nami kujumuishwa katika majina haya, lakini ninachokiona cha msingi katika Bunge la Katiba ni kusimamia hoja ya uchaguzi Uhuru…nitakuwa mjinga sana nikiacha hoja hii ikifumbiwa macho, halafu mambo ya kihuni yakaendelea kufanyika katika chaguzi mbalimbali za kisiasa hapa nchini,” alisema Profesa Safari.

Profesa Lipumba

Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kufurahishwa na uteuzi huo, kwa kusema umejumuisha watu kutoka maeneo mbalimbali.

“Ninachowaomba tu wanasiasa wenzangu waliobahatika kuchaguliwa, wajitahidi kutetea na kuwawakilishia wananchi kile wanachokitaka na si kwa maslahi yao ya kisiasa, kwani lengo ni kujenga taifa letu,” alisema Profesa Lipumba.

Abdallah Bulembo

Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdalah Bulembo, alishauri kuwa wajumbe wa Bunge wa katiba waende Dodoma kama wamoja na warudi wamoja.

“Tuweke kando maslahi yetu ya kisiasa, tukiwa Dodoma tujue tuko kwa ajili ya maslahi ya Watanzania, tusiende kwa ushabiki wa vyama vyetu, nikisema hivyo haimaaniishi napingana na msimamo wa chama changu kuhusiana na serikali mbili, lakini niwaombe wenzangu wakati tukiwa na dhamira yetu ya serikali mbili, twende tukaitetee kwa hoja na si kwa kuweka ushabiki utakaoleta malumbano,” alisema Bulembo.

Julius Mtatiro

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, amesema kuwa uteuzi huo wa Rais ni zawadi kwa Watanzania na kuahidi kwenda kutunga katiba ya Watanzania na siyo ya chama chake.

Juzi, Ikulu ilitangaza majina ya wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, likiwajumuisha wanasiasa wakongwe, kama Kingunge Ngombale Mwiru na Paul Kimiti.

Wanasiasa wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Ibrahimu Lipumba, Profesa Abdallah Safari, anayeiwakilisha Chadema, Mwenyekiti wa Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, Dk. Emanuel Makaidi (NLD) na James Mapalala wa Chausta.


IMG_0037.jpg


 
Back
Top Bottom