Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
WAENDESHA pikipiki maarufu kama bodaboda, wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Tanzania na Kenya kupitia njia ya Holili mkoani Kilimanjaro, wamesimamisha shughuli za kibiashara baina ya Kenya na Tanzania kwa zaidi ya saa 10 baada ya kufunga geti la mpaka huo kwa mawe.
Wakielezea tukio hilo jana, mmoja wa madereva bodaboda hao, Severini Shirima, alisema walifikia uamuzi huo kutokana na madereva bodaboda wa Kenya kuwazuia kuingia nchini kwao.
Alisema madereva bodaboda wa Kenya wamekuwa wakiwazuia kuingia nchini kwao kwa kuwataka wanapofika mpakani hapo na abiri au mizigo kuwashusha na kurudi Tanzania na wao huwachukua na kuwaingiza Kenya.
Shirima alidai kuwa tatizo hilo lilianza kutokea juzi kabla ya kumalizwa jana saa saba mchana na kwamba baada ya kuona hivyo ndipo madereva bodaboda wa Tanzania wanaofanya kazi katika mpaka huo wa Holili walipoamua kuandamana na kufunga geti la kuingilia nchini kutoka Kenya wakishinikiza Wakenya kutoingia Tanzania.
"Sisi tumekuwa tukiwaachia wenzetu wa Kenya kuingia nchini kwetu na abiria wao pamoja na mizigo, lakini katika hali ya kushangaza wao wametuzuia tusiingie nchini kwao ndio maana na sisi leo tukaamua tufunge mpaka ili na wao wasiingie kwetu," alisema Shirima.
Akizungumzia tukio hilo mara baada ya kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Taveta nchini Kenya, Henry Wafula, Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Rombo ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Lembris Kipuyo, alisema kulitokea tatizo la kutoelewana kati ya madereva bodaboda wa Tanzania na Kenya.
Kipuyo alisema mara baada ya kutoelewana huko, vyombo vya usalama kutoka Kenya vilikutana na vya usalama kutoka Tanzania na kukubaliana kuwa Kamati za Ulinzi na Usalama za nchi hizo mbili kukutana na madereva bodaboda wa pande zote mbili ili kuwapatia elimu jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika mpaka wa nchi hizi mbili.
"Tumekutana kamati mbili za ulinzi za usalama ambazo ni ya Kenya na Tanzania, tumeongea na kuelewana hivyo tumeona ili kuhakikisha kuwa tatizo hili halijirudii tena ni vyema tukawapa elimu madereva bodaboda, hivyo elimu hiyo itatolewa Jumamosi wiki hii," alisema Kipuyo.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Rombo kuhakikisha kuwa hatawavumilia watu wanaojichukulia sheria mkono kama walivyofanya madereva bodaboda kwa kufunga mpaka.
Kwa upande DC Wafula wa Taveta, alisema wamekubaliana huduma hiyo ya bodaboda iendelee huku pia, wakiweka mikakati ya kukutana na madereva hao wa pande zote mbili na kuwaelimisha jinsi ya kufanya biashara kwa pamoja.
Chanzo: Nipashe