Birika la kahawa na propaganda dhidi ya ACT-Wazalendo

Birika la kahawa na propaganda dhidi ya ACT-Wazalendo

Jemedal_bin_chichi

JF-Expert Member
Joined
Feb 17, 2016
Posts
542
Reaction score
585
Jumamosi tarehe 09 Septemba 2017 nilikuwa Jimbo la Kasulu Mjini kuhudhuria Mkutano wa Kidemokrasia wa Jimbo ulioandaliwa na Uongozi wa ACT Wazalendo wa Mkoa wa Kigoma.

Kwa kuwa kikao kilikuwa kesho yake nilimuomba Mwenyekiti wa Mkoa anipeleke sehemu ya mji wanakokutana viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa kujadiliana.

Mwenyekiti akanipeleka kwenye kijiwe maarufu cha kahawa cha Sheikh Upupu. Baada ya kutambulishwa na kubadilishana mawazo mawili matatu mtu mmoja akaniuliza "Je ni kweli nyinyi ACT ni CCM B"?

Mimi nikawageukia wajumbe na kuwapa changamoto kuwa mtu yeyote atayetoa mfano wa kuonesha kuwa ACT ni CCM B na wote tukaridhika nitanunua birika zima la kahawa ambalo linauzwa elfu tano.

Kwa kila mfano utaotolewa ambao nitashindwa kuujibu na wao wakaridhika niliwaahidi kununua birika moja. Hata mifano ikiwa kumi niliwaahidi kuwa nipo tayari kununua birika kumi za kahawa. Washiriki wa mjadala wakachangamka kwelikweli na kuanza kuimimina mifano nami nikatoa majibu.

Swali: Zitto alitoa maneno makali sana dhidi ya Dk. Shein kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar. Rais alipokuja kuhutubia Bunge wenzake walitoka Bungeni kumsusia Shein ambaye naye alikuwepo. Zitto alibaki. Huoni kuwa huo ni mfano unaostahili birika zima la kahawa?

Jibu: Ninashukuru kwa kutambua Zitto alitoa maneno makali dhidi ya Shein. Kwetu suala la Zanzibar ni sual a la principle. Demokrasia imebakwa Zanzibar.

Haiitaji nguvu kufahamu hilo. Kwa kweli sisi tumekuwa *bold* sana kwa jambo la Zanzibar. Upo mstari Zitto amewahi kuuvuka kuhusu Zanzibar wenzake hawajawahi. Yeye amewahi kufananisha kilichofanyika na uhaini na kutaka Shein achukuliwe hatua. Nitoe mfano mwingine.

Ndani ya chama chetu tulilazimika kumchukulia hatua Makamu Mwenyekiti Zanzibar kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama kuhusu Zanzibar. Kwa hiyo, suala la zanzibar ni nyeti sana kwetu. Zitto hakutoka Bungeni kwa sababu aliyekuwa anahutubia ni Rais Magufuli na ilikuwa hotuba yake ya kwanza.

Hatukuona umuhimu wa kufanya hivyo. Kila tulipoona sababu ya kuwaunga mkono wenzetu kutoka nje iwapo kuna ulazima wa kufanya hivyo tumefanya na nyinyi ni mashahidi. Hata wewe mwenyewe utakubaliana na mimi kuwa mfano huu haustahili birika

Swali: Akiwa hapa Kasulu Zitto aliambatana na Rais Magufuli. Kisha akawa naye Kigoma. Humo mote, Zitto alimsifia Magufuli kuhusu masuala fulani. Lakini Zitto amekuwa kinara wa kusema Magufuli anabana Demokrasia na kwamba ni dikteta. Mbona anageuka?

Jibu: Watu wanaotaka Zitto atumie jukwaa lile la uzinduzi wa miradi ya maendeleo kusema Magufuli ni dikteta hawawatendei haki wana Kasulu, wanakigoma na watanzania.

Viongozi wa Chadema na CUF wanahudhuria hadhara za Rais licha ya kwamba wanapambana naye kuhusu demokrasia. Nani kati yao ametumia jukwaa la maendeleo kusema udikteta wa Magufuli?

Mfano pekee ninaoukumbuka ni wa Mama Mwakagenda. Yeye licha ya kumpongeza RC Makala kuwa mchapakazi alimwomba Waziri Mkuu kukemea amri ya mkurugenzi wa wilaya kuamuru bendera za chadema kushushwa. Sijaona mwingine.

Si kaka yangu Meya Boniface Jacob. Si Mbunge Nassari. Si Mbunge Lwakatare nk Hakuna anayefanya hivyo. Kila jambo lina sehemu yake. Wasaa wa kudai maendeleo tutadai maendeleo, kwenye majukwaa muafaka tutakabiliana na Rais kuhusu demokrasia.

Hatutarudi nyuma. Hivi sasa wanasheria wetu wanachambua kwa umakini namna ya kutengua amri yake batili ya kuzuia mikutano kwa kwenda kuipinga mahakamani.

Mngenishawishi kuwa kwenye mkutano ule kwamba Ndugu Zitto alibadilisha maneno na kusema kwamba Magufuli sasa ni mwanademokrasia ningetoa birika. Hivi si mwenyekiti mbowe aliyesema kuwa Rais akifanya vyema asifiwe na akikosea akosolewe?

Swali: Zitto ni mwiba kwa Rais Magufuli. Kwa nini hakamatwi?
Jibu: Zitto amekwishaitwa mara mbili na kuhojiwa polisi. Pia, "Kwa ufundi wake" amewatoroka polisi Kahama. Ni kweli wafuasi wengi zaidi wa chadema wamekabiliwa na polisi. Niwaulize swali. Wakati ule IGP Mahita akikabiliana na CUF kwa mkono wa Chuma alifanya hivyo kwa Chadema?. Aliwaweka ndani mara kwa mara na kuwapandikizia majambia akina Mzee Makani wa Chadema?

Hakufanya hivyo. Chadema haikukabiliwa kama CUF wakati huo kikiwa chama kikuu cha upinzani. Jibu ni wazi kabisa. Chadema haikuwa tishio kama CUF. Na sasa ni hivyohivyo. Dola inatuhofia kwa hoja zetu na inatutisha mara kadhaa kwa sababu tuna hoja nzito. Lakini kimapambano, wanachukua hatua zaidi kwa chadema.

Hatuwezi kuichokoza polisi ili tukamatwe zaidi ya wengine. Ni kanuni ya kawaida kabisa. Na sisi wakati wetu wa kukabiliwa zaidi kuliko chama chochote unakuja na kwa bahati nzuri hauko mbali kwa sababu chama chetu kitashika gurudumu la upinzani.

Swali: Rais amemteua Mama Mgwira kuwa Mkuu wa Mkoa na hivyo kuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM. Na prof kitila ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara. Huoni kama Rais anawapenda sana.

Jibu: Kwanza Katiba ya CCM haisemi kuwa Kila mkuu wa mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa. Kifungu husika kinasema "mkuu wa mkoa anayetokana na CCM". Mama Anna hatokani na CCM. Lakini yote kwa yote, sisi hatujakaa na Rais Magufuli kufanya teuzi hizi.

Anaamua mwenyewe. Anaweza kufanya kwa nia njema au kutupunguza makali. Sisi kama chama tumechukua tahadhari. Wote wawili wamelazimika kuachia nafasi zao kwa sababu nafasi wanazohudumu zinazalisha mgongano wa kimaslahi kati ya majukumu ya chama na yale ya serikali. Haikuwa rahisi. Kwa mfano, kama mnavyofahamu, Mama Mghwira aliweka msimamo wake kuwa angependa kuendelea kuwa mwenyekiti.

Sisi tukasema hapana. Kwa hiyo kama chama hatutamzuia mtu kuteuliwa. Kila mtu yupo huru kabisa. Kwa mfano mimi nilihojiwa na BBC wakati fulani "kijana ukiteuliwa wewe kuwa DC au RC utakubali"? Jibu likawa kwa mazingira ya nchi yetu na nature ya kazi hizo SITAKUBALI.

Na Ndugu Zitto ameweka bayana hivi karibuni kuwa hatakubali uteuzi wowote wa Rais Magufuli kutokana na matumaini ya Wana-ACT juu yake. Halafu ninapenda kuwapa swali: kwa jinsi Mama Anna na Prof. Kitila walivyokuwa nyeti ndani ya ACT mnadhani kweli uteuzi wao ni mahaba? Mahaba gani ya kukuchukulia wale walio bora kwako?

Moja kati ya magazeti ya Ndugu Kubenea liliandika kwamba Magufuli anafanya teuzi hizi kumshughulikia zitto. Kwa hiyo teuzi hizi sio jambo dogo. Ni jambo lenye mjadala na sura nyingi. Inawezekana ni kuwateua wahudumie taifa. Ikiwa hivyo sawa.

Lakini pia kama lionavyo gazeti la Kubenea, inawezekana ni kutupunguza nguvu. Ikiwa hivi pia ni sawa, kwa maana sisi haiwezi kuturudisha nyuma. Chama chetu kimeshinda hila nyingi na kina hazina ya wanachama wa kuchukua nafasi zao.

Swali: Tunaambiwa magari mliyotumia wakati wa kampeni ni ya serikali ya CCM. Ni kweli?

Jibu: Hizo ni porojo. Wakati mwingine wapishi wa porojo hizo hawana kumbukumbu kabisa. Leo watakuambia ulipewa mabilioni ya uchaguzi na CCM. Kesho magazeti yao yataandika na kutoa vielelezo kuonesha kuwa ACT kinadaiwa madeni makubwa yani yotokana na uchaguzi. Unajiuliza ushike lepi uache lipi! Ukweli ni kwamba uchaguzi ule ulitokana na michango ya watu wenye kuitakia mema ACT hasa viongozi na wanachama.

Swali: Kwa nini chama chenu hakikusimama na UKAWA kwenye uchaguzi uliopita?

Jibu: Sisi tuliwaandikia barua UKAWA kutaka kufahamu utaratibu wa kujiunga UKAWA. Lengo letu lilikuwa baada ya kujua utaratibu huo tupeleke jambo hilo kwenye vikao ili wanachama waamue kama wangependa kujiunga ama la. Wenye maamuzi ni wanachama wenyewe. Hatukujibiwa barua yetu. Tukasonga mbele na kushiriki uchaguzi kivyetu. Tumepata Mbunge, Manispaa na Madiwani 42.

Tutazitumia manispaa na kata kuonesha sera zetu kwa vitendo. Madiwani tumepata nchi nzima kuanzia Arusha(Ngorongoro), Manyara(Hanang na Mbulu), Tabora (Urambo na Kaliua), Mwanza(Misungwi), Pwani(Mkuranga na Kibaha) na Morogoro(Mvomero na Morogoro Kusini Mashariki).

Kwa sasa, kwa uchaguzi wa mwaka 2015 chama chetu kiliachwa na CCM, CHADEMA na CUF pekee. Tumeyapata mafanikio hayo kwa kipindi kifupi sana. Bila shaka 2020 tutafanya vizuri zaidi.

Swali: ACT ni chama kilichoundwa na CCM kudhoofisha upinzani?
Jibu: Hiyo ni propaganda tuu. Awali walisema kuwa Chama hiki ni cha Lowasa. Kumbukumbu zipo na magazeti yaliandika. Lowasa akaenda kwao wakageuza gia angani na kusema sisi ni CCM.

Ukiwauliza kwa hoja ipi hakuna wanachoeleza cha maana. ACT ni chama kilichoundwa na watu ambao wamechoshwa na mienendo mibovu ya demokrasia kwenye vyama vyao.

Kusema kimeundwa na CCM ni porojo. Niwape mfano, Mbowe alisema kuwa Zitto ni msaliti anayetumiwa na CCM. Lakini mara kadhaa akiwa Bungeni amefanya kazi na zitto pale Bungeni. Nyie wenyewe mmeona.

Sasa unadhani kwa nini Mbowe anaweza kukaa meza moja na zitto? Jibu ni jepesi.

Moyoni mwake anajua kilichowagombanisha kabla ni mnyukano wa kugombea cheo, hizo nyingine ni blah blah tu. La sivyo asingekaa naye meza moja.
......
Tuliendelea na mjadala huu tangu saa moja hadi saa nne. Hakuna muuliza swali aliyedai birika la kahawa kwa kutoridhika. Kuchangamsha baraza nilinunua birika moja. Mwishowe, bila kujali itikadi,Wanakasulu walinishukuru kwa kuwatembelea kwa kile wlichosema "sio jambo la kawaida kwa kiongozi wa kitaifa kuwatembelea kwenye vijiwe vya kahawa labda wakati wa uchaguzi". Wakaniahidi kuwa kwa vile nimewaonyesha uungwana kuwatembelea, nao watakuja kesho kwa wingi kwenye mkutano wetu. Kesho yake, ukumbi wa TTC Kasulu ukatapika watu.
10.9.2017
Ado Shaibu,
Katibu Mwenezi Taifa
ACT Wazalendo
11.09.2017
Kasulu
 
Mkuu, tunashukuru sana kwa taarifa yako ndefu. Lakini mbona unatumia muda mwingi kukanusha kama vile ACT wazalendo kuwa na partnership na CCM ni dhambi? Yes. aliyekuwa mgombea wa chama chenu ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro. Je anatekeleza sera za maagizo ya ACT huko? Kiongozi mwingine pia ni Katibu Mkuu wa Wizara moja nyeti. Unajua ni kwa nini CCM inateua kutoka kwenye chama chenu na si Chadema wala CUF? ukiweza kujibu swali hili nitakuongezea birika la kahawa.
 
Mkuu, tunashukuru sana kwa taarifa yako ndefu. Lakini mbona unatumia muda mwingi kukanusha kama vile ACT wazalendo kuwa na partnership na CCM ni dhambi? Yes. aliyekuwa mgombea wa chama chenu ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro. Je anatekeleza sera za maagizo ya ACT huko? Kiongozi mwingine pia ni Katibu Mkuu wa Wizara moja nyeti. Unajua ni kwa nini CCM inateua kutoka kwenye chama chenu na si Chadema wala CUF? ukiweza kujibu swali hili nitakuongezea birika la kahawa.
Majibu ya swali hilo yapo tayar ktk maelezo hapo juu, yalitoka maelezo mazur ndio sababu walishindwa kuuliza swali hilo kwa uona majibu yashatolewa,

Je wewe hauoni wenzako pia walifaham kuwa swali hilo lilisha wakosesha fursa ya kupata birika moja ya kahawa?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom