Bifu la Shigongo, Ruge na Babu Tale

moryda

JF-Expert Member
Sep 29, 2014
287
119
SHIGONGO: Mimi, Babu Tale na Ruge
NI kweli Shilawadu wameniomba msamaha na mimi ninawashukuru sana, huo ndiyo uungwana, unapomkosea mtu, omba samahani, YAMEKWISHA! Lakini siyo vibaya nikisimulia kidogo!

Ni saa 3:30 usiku, nimerejea nyumbani kutoka ofisini, nimechoka kupita kiasi, watoto wamekwishalala, jambo ambalo huwa sipendi kabisa litokee yaani watoto kuingia kitandani kulala kabla sijafika, kama binadamu wengine walivyo nimeudhika.

Babu Tale, Meneja wa Diamond ameniudhi, amenisingizia jambo ambalo sikufanya na amefanikiwa kuwaaminisha watu ya kwamba mimi na yeye tumeingia kwenye mvutano kwa sababu ya maslahi ya kibiashara, jambo ambalo si kweli, Tale mwenyewe anafahamu ukiachana na Mungu.

Mke wangu yuko macho, alikuwa ananisubiri nifike ili tule chakula pamoja, najaribu kadiri ya uwezo wangu wote kutomuonesha kilichokuwa kikiendelea kichwani mwangu, naufunika uso kwa tabasamu! Kabla sijaondoka ofisini mtu mmoja alinitaarifu mapema kwamba Tale alikuwa amepeleka sauti yangu Clouds TV, kwenye kipindi cha Da Weekend Chat Show maarufu kama Shilawadu ili anidhalilishe.

Mke wangu anaangalia Clouds TV, hewani kipo Kipindi cha Shilawadu, natamani nimwambie ahamishie stesheni nyingine ili asione kile ambacho vijana wa Shilawadu wangetangaza kwa niaba ya Babu Tale, Meneja wa Diamond Platnumz ili kunichafua, lengo la Tale kupeleka sauti ya maongezi yangu na yeye kwenye simu halikuwa jingine bali kutaka kuniharibia taswira yangu mbele ya jamii.
“Acha tu aangalie, alishasikia mangapi?” nilijisemea moyoni mwangu na kujiuliza kisha kunyanyuka na kuelekea bafuni.

Wakati nikiendelea kuoga nilisikia sauti ya mke wangu akisema:
“Baba Sam, njoo uone wanakutangaza!”
Sikutaka kuonesha kwamba nimeshtuka, baba yangu aliwahi kuniambia:
“Mwanamke ukimwonesha kwamba umeumia, umekasirika au umeshtuka, yeye hushtuka mara mbili!”
Hivyo nikaendelea na kazi niliyokuwa nayo; kuoga.

“Vipi?”
“Wametangaza kwamba wewe na mtu mmoja anaitwa Babu Tale eti mna ugomvi, ambao umetokana na biashara na sasa unamtishia maisha!”
“Mke wangu unanifahamu vizuri, kama naweza kufanya mambo hayo unatakiwa uwe mtu wa kwanza kuelewa, huu ni uleule mlolongo wa matendo ya kutaka kunichafua ambao kwa miaka mingi tangu nianze kazi ninayoifanya umekuwa ukifanyika!”

“Kwani kuna nini hasa?” aliuliza.
mwenza wangu alikuwa na haki ya kufahamu kile kinachoendelea katika maisha ya mume wake, hiyo ndiyo tabia yake kila ninaporejea kutoka kazini, wajibu wangu ukawa ni kumwelewesha juu ya nilichokiandika mtandaoni kama ushauri kwa Diamond, kwa upendo nilionao kwa kijana huyo, badala ya Tale kuchukulia ushauri wangu kwa mtazamo chanya, alikuwa ameamua kuingia katika vita ya kunichafua, eti kwa sababu ana ‘followers’ milioni moja kwenye Mtandao wa Instagram.

“Wamesema baadaye wataweka sauti yako ukimtishia Tale maisha!”
“Acha tusubiri, ila nataka nikuambie mapema kabla hawajarusha sauti yangu watasema maneno;

kama unataka kuposti posti Tale… unanitishia kuniposti tangu juzi… hutaki nifanye kazi yangu? Au unataka vita? Wakisema maneno tofauti na hayo, nidharau!”
Sote tulibaki kimya tukiangalia kipindi hicho, mke wangu alionekana kabisa kilichotokea kwenye luninga kwa namna moja au nyingine kilikuwa kimemgusa ila alichokifanya ni kunitia moyo! Kumbukumbu nyingi zikamiminika kichwani zikinirejesha miaka kadhaa nyuma;

Nikaikumbuka siku ambayo mtangazaji wa kipindi ambacho sikikumbuki hata jina cha Channel Ten alimweka msanii Dudubaya kwenye luninga kwa zaidi ya saa nzima akinitukana mimi kila aina ya matusi aliyoona yanafaa, kituo cha televisheni kiliamua kumpa Dudubaya muda wote huo kunitukana mimi bila kupewa nafasi ya kujieleza.

Baadaye nilikuja kugundua kwamba nyuma ya Dudubaya kunitukana kiasi hicho alikuwepo mtu mmoja aitwaye Ruge, sikufanya chochote, zaidi ya kumwambia mmiliki wa kituo hicho cha Televisheni wakati huo, Franco Tramontano kwamba walichonitendea hakikuwa kitu sahihi hata kidogo.

Kumbukumbu hizo zilinirejesha tena miaka mingi nyuma Jenerali Ulimwengu katika kipindi chake cha Jenerali on Monday alipowapa zaidi ya saa nzima marehemu Amina Chifupa na Sinta nao wakanitukana watakavyo pamoja na magazeti ninayoyachapisha bila mimi kupewa nafasi ya kujitetea, nayasema haya ili watu waelewe kuwa Shigongo si kazi rahisi, lazima uwe na ngozi ngumu.
Nikagundua pia kwamba nyuma ya Amina Chifupa na Sinta alikuwepo mtu aitwaye Ruge, uhusiano wangu na Ruge ukavurugika kabisa baada ya matukio hayo, si yeye tu bali pia Marehemu Amina Chifupa (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) na kundi zima lililojiita Alqaeda Network lililowajumuisha Maimartha, Mtandika, Violet Mzindakaya na Sinta ambao walikuwa wameapa (wakati huo) kupambana na mimi kwa gharama yoyote kuhakikisha eti na mimi nachafuka.
Niligundua pengine ilikuwa ni vita vya kugombea ushawishi, hata hivyo, baadaye tulikuja kuketi na kuona hapakuwa na sababu yoyote ya kuendelea kugombana sisi vijana wa taifa moja, bali tushirikiane kuchapa kazi kila mmoja asonge mbele!
Maneno haya yalikuwa ni ya Mkurugenzi wa Clouds FM, Joseph Kusaga ambaye siku zote huwa mimi naamini hakuna tatizo lolote kati yangu na yeye, labda kama mchana ni inzi, usiku ni mbu.

Kipindi hichohicho Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa wakati ule, akiongoza Baraza la Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mjini Dodoma walianzisha Kamati ya Kuthibiti Ukimwi Taifa iliyokuwa chini ya umoja huo, bila kuomba, bila kuwepo Dodoma, niliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo kwa kipindi cha miaka mitano, makamu mwenyekiti wa kamati yangu akiwa ni Ruge!

Ambacho umoja wa vijana hawakukifahamu ni kwamba mwenyekiti na makamu mwenyekiti wake walikuwa ni watu wasiopikika chungu kimoja, kazi ikaanza, nikakabidhiwa kamati yenye wajumbe kumi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela akiwa mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, bila fedha!

Kwa miaka mitano nilifanya kazi hiyo kwa kujituma, tukisafiri sehemu mbalimbali za nchi yetu kufanya matamasha makubwa kila siku ya Desemba Mosi ambayo ni Siku ya Ukimwi duniani, kwa msaada na ushawishi wa Mwenyekiti Nchimbi, tulipata baadhi ya mashirika ya kutufadhili, lakini mara zote hayakutoa fedha mapema hivyo kulazimika kutumia fedha zangu ili baadaye zikipatikana za wafadhili nirejeshewe!

Mhasibu sikuwa mimi, bali Marehemu Malinda, aliyekuwa mfanyakazi wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, hesabu zote zilitunzwa vizuri! Lakini mwaka wa tatu wa kamati hiyo, ikiwa ni siku moja kabla ya tamasha lililofanyika Viwanja vya Leaders, Kinondoni, nimemaliza kuongea na waandishi wa habari, nilipokea wito kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Vijana kwamba wajumbe wenzangu walikuwa wakinihitaji.

Nilikwenda kukutana nao, mtu mmoja alikuwa amefanikiwa kuwashawishi baadhi ya wajumbe kwamba ning’olewe uenyekiti wa kamati hiyo kwa sababu tu nilikuwa siwashirikishi wajumbe masuala ya fedha na makamu mwenyekiti ndiye alitakiwa kuchukua nafasi yangu.

Nilisikitika sana, lakini nikaelewa kilichokuwa kikiendelea ndani ya kamati, mtu mmoja alitaka isomeke kwenye magazeti siku iliyofuata “Shigongo ang’olewa uenyekiti wa kamati” na ingebaki kwenye historia yangu kwamba niliwahi kuondolewe kwenye kamati, bila Mwenyekiti Nchimbi na Katibu Mkuu wa UVCCM wakati huo, Amos Makala kuingilia kati, jambo hilo lingetokea na bila shaka leo hii ningekuwa natambulika kama mtu niliyewahi kung’olewa kwenye kamati.
Jambo hilo halikutokea, tamasha kubwa lenye mafanikio likafanyika, baada ya hapo nikataka kujiuzulu lakini mwenyekiti akanizuia, mwaka wa tano nikamaliza kazi yangu na kuondoka umoja wa vijana kwa heshima, mpaka ninavyoandika kumbukumbu hii tamasha hilo halijawahi kufanyika tena.

Yote haya yalinijia kichwani wakati nikisubiri vijana wa Shilawadu, Kipindi cha Televisheni cha Clouds waweke sauti yangu hewani, kituo cha televisheni ambayo wiki mbili tu kabla Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda alikivamia na mimi nikaandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook kumlaani Makonda kwa kitendo hicho, ikifuatiwa na vyombo vyote vya habari kugoma kuandika habari za mkuu huyo kama utetezi wa Uhuru wa Habari lakini pia Clouds TV na Redio.

Sitaki upendeleo, nikifanya kitu kibaya katika jamii ni vyema niandikwe au nikosolewe, lakini ilikuwa hainiingii akilini kabisa Clouds TV na kipindi chao cha Shilawadu katika kipindi ambacho mimi niliamua kutofautiana na Mheshimiwa Makonda kwa ajili yao, eti walikuwa wamefikia uamuzi wa kunichafua kiasi hicho kwenye televisheni yao kwa jambo la uongo, tena bila hata kuuliza upande wa pili.
“Hii ni dharau, hivi na mimi nikiamua kesho kuandika bila kuwapa haki ya kujieleza maneno yanayosemwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alivamia kituo chao kwa sababu alikuwa ameambiwa kwamba huwa wanaficha Cocaine kwenye studio zao na kwamba eti wanahusika na kifo cha Marehemu Mangwea kilichotokea Afrika Kusini, watafurahi?”

Nilijiuliza moyoni mwangu na nikahisi kuchukia. Mimi sikuandika mambo hayo kwani nilitumia hekima kwa sababu si kila kitu kinachosemwa ni cha kuandika lakini wao walishindwa kutumia hekima ili kunichafua. Uamuzi wa kuniweka kwenye televisheni yao kwa tuhuma za upande mmoja kwa sababu tu Babu Tale alikuwa ni rafiki yao, hakika zilikuwa zimenikasirisha kama binadamu, kuna wakati nilijiuliza “Hivi huyu Ruge sijui huwa ananitafuta nini?

Tumeshakwaruzana mara nyingi sana maishani lakini…” mwisho nikaamua kutulia na kusubiri sauti yangu irushwe, kama utani, kweli mwisho kabisa wa kipindi chao wakairusha. Nikajaribu kumpigia Ruge simu kama mara mbili hakupokea, nikapuuza na kuamua kuingia kitandani kulala, akili yangu ikiwa imevurugwa nikijieleza mwenyewe ule msemo wa Wachina

“Usifanye uamuzi wowote ukiwa umekasirika au kufurahi sana” hii ilinifanya nipuuze, haukupita muda mrefu sana nililala na kuamka siku iliyofuata, Aprili Mosi. Nikiwa ofisini nilipokea ujumbe kutoka kwa Ruge, akieleza kwamba hakuziona simu zangu kwa sababu alilala mapema, kwani alikuwa hajisikii vizuri, akaniuliza kama kulikuwa na jambo lolote ambalo angeweza kufanya, nilimjibu “Hakuna tatizo kaka, kipindi kilikuwa kizuri, mnafanya kazi nzuri sana, hongereni” nilijua lazima angeelewa nilichomaanisha katika ujumbe huo.

Baadaye nilifanya kikao na wafanyakazi wenzangu, karibu kila mtu alikuwa amekasirishwa na kilichokuwa kimetokea, nikachukua nafasi ya kuwaelezea jinsi suala zima lilipoanzia na mimi kutoa ushauri kwa Diamond kisha Tale baada ya kukasirishwa kuamua kuweka mtandaoni ujumbe kwamba ushauri nilioutoa ulitokana na mimi na yeye kutofautiana kimaslahi kwenye shoo ya Harmonize aliyotaka kuifanya Dar Live Siku ya Pasaka.

“Siyo kweli, niliposti kwanza ushauri mtandaoni, Tale akaniandikia ujumbe wa kulalamika, baadaye tukaongea kwa simu nikimwondoa wasiwasi, hapo ndipo akaingiza suala la shoo ya Harmonize, hivyo kuposti kulitangulia kwanza ndiyo suala la shoo likaja, hata hivyo nilimtuma kwa meneja mkuu maana mimi kama mjuavyo Dar Live huwa siendi.”

Vijana walikuwa tayari kuingia kazini na Ruge pamoja na Tale, lakini nikawasihi wasifanye chochote kwa sababu tu wamechukia, watulie, kwani hakuna tusi ambalo mimi nilikuwa sijatukanwa kwa miaka ishirini niliyofanya kazi ya uchapishaji! Wakakubaliana na mimi, hata hivyo, wakasema watakwenda mpaka kijijini kwao na Tale, huko Turiani, Morogoro, kujaribu kumchimba Tale ili wampe umaarufu aliokuwa akiutafuta.

“Mpigieni pia Zamaradi, mmuulize juu ya…!”
mmoja wa wahariri alisema, kazi hiyo ilifanyika, Zamaradi mwenyewe alifahamu alichoulizwa ambacho si muhimu kukiongea leo mpaka itakapohitajika. Huko Turiani, mwandishi wetu kutokea Mogorogo aliibuka na mambo mazito kuhusu Babu Tale, mtani wangu wa Kiluguru, ambayo hivi karibuni kama hataueleza umma ukweli juu ya uongo alionisingizia kwamba ugomvi wetu ulikuwa ni wa maslahi, yatachapishwa ili kijana huyu awe maarufu zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na hatakuwa na mtu wa kumlaumu, kwa sababu ameliamsha mwenyewe dude, msemo wa rafiki yangu, Askofu Gwajima.

Siku ya Jumapili nilipigiwa simu na mtu akinitaarifu kwamba Clouds FM walikuwa wanarusha sauti ya Tale kwenye redio yao nyingine iitwayo Choice FM, nikaelewa kweli jamaa wamedhamiria, siku ya Jumatatu mchana nilipigiwa simu tena na mtu kuwa walikuwa wakiendeleza mjadala kati yangu na Tale kwenye kipindi chao cha XXL! Duh! Vita ilikuwa imepamba moto, ya nini? Sielewi, nikahisi kulikuwa na jambo kubwa nyuma ambalo mimi nilikuwa silifahamu, kwani suala la Tale na mimi lilikuwa ni dogo mno kupewa dakika zote hizo kwenye vyombo vyao vya habari.
 
Shigongo ana credibility na moral authority gani katika jamii? Baba wa udaku na uvurugaji vijana Tanzania! Eti Dar Live mie siendi. Kwa vile mlokole ama? Kama mlokole mbona umeijenga hiyo Dar Live? Hata usipoenda uchafu unaofanyika huko haukufikii? Hivi na Opresheni Fichua Maovu (OFM) iliishia wapi? Au imepunguzwa makali na sheria ya makosa ya mtandao? Umedhalilisha sana dada na mama zetu. Umevuruga maisha ya watu wangapi kwa kuwaandika kidaku katika magazeti yako ya udaku? Leo nawe unaogopa kuandikwa na kusemwa kwenye vyombo vya habari. Pathetic! Siku moja utalipa - tena hapa hapa duniani!
 
Huko Turiani, mwandishi wetu kutokea Mogorogo aliibuka na mambo mazito kuhusu Babu Tale, mtani wangu wa Kiluguru, ambayo hivi karibuni kama hataueleza umma ukweli juu ya uongo alionisingizia kwamba ugomvi wetu ulikuwa ni wa maslahi, yatachapishwa ili kijana huyu awe maarufu zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na hatakuwa na mtu wa kumlaumu, kwa sababu ameliamsha mwenyewe dude, msemo wa rafiki yangu, Askofu Gwajima.

Blackmail, blackmail, blackmail.

Mkuki kwa binadamu, jamaa alivyowaandika watu bila aibu leo anaogopa kuandikwa? Kusemwa?
 
Shigongo ana credibility na moral authority gani katika jamii? Baba wa udaku na uvurugaji vijana Tanzania! Eti Dar Live mie siendi. Kwa vile mlokole ama? Kama mlokole mbona umeijenga hiyo Dar Live? Hata usipoenda uchafu unaofanyika huko haukufikii? Hivi na Opresheni Fichua Maovu (OFM) iliishia wapi? Au imepunguzwa makali na sheria ya makosa ya mtandao? Umedhalilisha sana dada na mama zetu. Umevuruga maisha ya watu wangapi kwa kuwaandika kidaku katika magazeti yako ya udaku? Leo nawe unaogopa kuandikwa na kusemwa kwenye vyombo vya habari. Pathetic! Siku moja utalipa - tena hapa hapa duniani!
Punguza ameshakusikia.
 
Back
Top Bottom