Barua Ya Wazi Kwa Wale Waliofukuzwa Kazi, Kutumbuliwa Au Kukutwa Na Sakata La Vyeti Feki.

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,420
Habari za leo rafiki?
Karibu kwenye barua hii ya wazi kwa wale wote ambao wamekutana na changamoto ya ajira yao kuisha ghafla. Hapa kuna wale ambao wamefukuzwa kazi, wametumbuliwa na waliokutwa na sakata la vyeti feki.

Hata kama kazi yako imekatishwa haraka bila ya maandalizi yako binafsi, pia barua hii inakuhusu na yapo mambo unayoweza kwenda kufanyia kazi kuboresha zaidi maisha yako.

Naelewa namna ulivyo wakati mgumu kwako katika kipindi kama hichi, ambapo tayari ulikuwa na kazi ambayo uliitegemea na ndiyo ilikuwezesha kuendesha maisha yako. Lakini ghafla, kinyume na matarajio yako, kazi hiyo imeisha na unajikuta mikono mitupu, ukiwa huna fedha za akiba za kukutosha, na huenda pia uko kwenye madeni.

Watu wanaweza kusema mengi, lakini wewe hasa ndiye unayejua wakati gani unapitia sasa, hivyo pole sana kwa kila ambacho unapitia kwa wakati huu umeondolewa kwenye kazi yako.

Natumia nafasi hii kukushirikisha mambo machache muhimu kufanya na kuzingatia kwenye kipindi hichi kigumu cha maisha yako.

1. Kubali hali uliyonayo na panga kusonga mbele.
Jambo lolote baya linapomtokea mtu, iwe ni kufiwa au kupoteza kitu, huwa anapitia kwenye hatua za kisaikolojia ambazo ni kukataa, kukasirika, kukubali, kuomboleza na maisha kuendelea. Sasa wapo wengi ambao wamekuwa wanatumia muda mrefu kwenye hizo hatua nyingine na hii kuwafanya wachukue muda mrefu kabla ya kuanza kuchukua hatua.

Kwako rafiki yangu, nakusihi utumie muda mfupi kwenye kila hatua, lengo ni kwenda kwenye kuchukua hatua, kutoka hapo ulipo sasa na kusonga mbele zaidi. Kwa sababu hata kama kufukuzwa ua kutumbuliwa kwako kumekuumiza kiasi gani, bado upo hai na maisha lazima yaendelee.

Pia kubali maisha yatabadilika, mwanzo ulikuwa na kipato ambacho unakitegemea kwa sasa hakipo tena, hivyo utahitaji kubadili mfumo wako wa maisha ili kuweze kuvuka salama kipindi hichi cha mpito.

2. Kama utachukua hatua za kisheria, usizitegemee kama njia ya kukutoa hapo ulipo. Huenda kufukuzwa au kutumbuliwa kwako kumefanywa kimakosa, huenda kweli huna kosa au huenda kosa unalo ila hatua zilizochukuliwa siyo sahihi kwako. Huenda una maslahi zaidi unapaswa kupewa kwa kufukuzwa kwako kazi. Na hivyo sehemu muhimu ya kwenda kudai haki yako ni mahakamani.

Watu wengi wamekuwa wanakwenda kufungua kesi zao wakiwa na matumaini makubwa na kusimamisha kila kitu wakitegemea watashinda kesi na mambo yao yatakwenda vizuri. Lakini huangushwa pale kesi inapochukua muda mrefu huku maisha yao yakizidi kuwa magumu.

Hivyo unapoamua kuchukua hatua za kisheria, chukua lakini usisimamishe kila kitu kwa sababu hiyo. Jua kwamba itakuchukua muda mpaka kuja kupata hiyo haki yako, kulingana na mifumo yetu ilivyo. Hivyo dai haki yako, lakini lisiwe ndilo tegemeo lako kuu, hasa kwa wakati huu ambapo huna kazi ya kufanya.

3. Kaa chini na jitathmini kipi unaweza kufanya sasa.
Chukua muda huu kukaa chini na kujifanyia tathmini wewe binafsi. Angalia katika kazi zako ambazo umekuwa unafanya, angalia mambo ambayo umekuwa unafuatilia na hapa utaona kitu gani unaweza kufanya kwa sasa.

Kama hujafukuzwa kwa sababu za kukosa sifa za kuajiriwa, kama cheti na mengine, unaweza kuona ni namna gani ya kutafuta ajira nyingine, hata kwa muda ili maisha yaweze kwenda. Lakini sikushauri sana urudi tena kwenye mfumo wa ajira, huu ni wakati muafaka kwako kushika hatamu ya maisha yako.

Kama huna tena sifa za kuajiriwa, basi hapo umebaki na hatua gani muhimu unayoweza kuchukua, na huna cha kukuzuia tena bali kuanza kuchukua hatua.

4. Tumia nafasi hii kama fursa ya kununua uhuru wa maisha yako.
Kwa watu wengi sana, ajira zimekuwa kama kifungo kwao. Wanalazimika kuishi maisha fulani ambayo siyo halisi kwao, bali tu kwa kuwa watu wanaofanya kazi kama wao wana maisha ya aina hiyo. Hivyo watu wanafanya manunuzi ya vitu visivyokuwa muhimu kwao bali tu kwa sababu kila aliye kwenye kazi anafanya hivyo.

Kingine ni mategemeo ya familia, ndugu na jamii kwa ujumla. Unapokuwa na kazi kila mtu anajua na hivyo unategemewa na wengi. Hata mambo ambayo wengine wangeweza kutafuta njia mbadala, hawafanyi kwa sababu labda wewe upo. Sasa huna tena kazi, hivyo hata wale waliokuwa wanakutegemea, matarajio yao yanakuwa siyo makubwa tena. Hili linaweza kukupa uhuru mkubwa wa kuanzia chini kabisa bila ya kutaka kuonekana na wengine kwamba na wewe upo.

5. Angalia wapi unapoweza kuanzia kwa sasa.
Kwa tathmini uliyoifanya, kwa uzoefu ambao umeupata kwenye kazi uliyokuwa unafanya, na mambo mengine ambayo unapenda kufanya na kufuatilia, angalia wapi unapoweza kuanzia. Anza kwa kutoa huduma yoyote ambayo inaweza kuongeza thamani kwa wengine. Angalia ni matatizo gani watu wanayo na unaweza kuyatatua na wakakulipa kwa kipindi hichi.

Huu siyo wakati wa wewe kuchagua utafanya nini, huu ni wakati wako wa kujenga msingi mpya wa mapato kutokana na msingi uliokuwa nao kuwa umeanguka.

Kama tayari ulikuwa na shughuli ya pembeni unaifanya wakati bado upo kwenye ajira, sasa ndiyo wakati wa kwenda kuweka nguvu zako zote kwenye shughuli hiyo ili kuikuza zaidi.

Kama ulijisahau kabisa na ukawa unategemea tu ajira, sasa unahitaji kuchukua hatua na anza na huduma unazoweza kutoa kwa sasa, maana hapo patakuwa rahisi kwako kuanzia.

Angalia fursa za kibiashara unazoweza kuanza nazo hapo ulipo sasa, kwa kiasi chochote cha fedha ulichonacho, na kama huna kabisa, basi angalia zile unazoweza kuanza nazo kutokea chini kabisa.

Muhimu ni fursa iweze kukutengenezea kipato cha kuhakikisha maisha yanaenda huku ukitengeneza msingi mpya.

6. Tengeneza msingi mpya, uliosahau kutengeneza ulipokuwa kwenye ajira.
Kama kilichotokea kimekukuta mweupe, yaani huna kitu kabisa, basi ulifanya makosa, hukujenga msingi kwenye maisha yako. Na hapa msingi ninaozungumzia ni vyanzo mbalimbali vya kipato pamoja na uwekezaji ambao unaweza kukuzalishia zaidi baadaye.

Ukishapata kitu ambacho kinakuwezesha maisha kwenda, sasa hapo unahitaji kujenga msingi wako mpya. Hata kama utapata ajira nyingine au kazi ya muda, huu ni wakati wa kuanza kujenga msingi wako upya.

Hakikisha unatengeneza vyanzo vingi na tofauti vya kipato na pia unawekeza maeneo ambayo baadaye yatakuzalishia.

Haya ndiyo mambo ambayo nakusihi sana wewe rafiki yangu uyafanye, na hutabaki hapo ulipo sasa. Muhimu sana ni kufungua akili yako, kutoka kwenye mtazamo kwamba sina la kufanya na sina pa kuanzia na kuanza kufikiri nianzie wapi au nifanye nini. Huo ni mtazamo sahihi ambao utakufanya uzione fursa nyingi zinazokuzunguka, ambazo hukuwa unaziona awali.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom