Barua ya Saleh Ally kwa mwamuzi wa Simba vs Yanga

madeinmusoma

JF-Expert Member
Jan 7, 2014
324
387
Kwako sister Jonesia Rukiyaa,

Najua wewe ndiye umepata nafasi nyingine muhimu ya kuchezesha mechi kubwa ya watani, yaani Yanga na Simba.
Mechi pekee ambayo inaweza kusimamisha au kuongeza kasi ya mapigo ya moyo ya wapenda soka nchini na hata nchi jirani.
Mechi maarufu zaidi ya watani katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kipindi kirefu sasa. Umepata nafasi nyingine ya kuwa mwamuzi.
Najua si kazi ndogo, lakini nianze na kukupongeza kwa kuwa nilijua watatu tu walikuwa na nafasi hiyo kulingana na hali halisi na utaratibu waliojiwekea TFF ambao unaweza ukawa sawa au vinginevyo. Ndiyo maana nimeamua kuandika barua jahara (ya wazi) kwako.
Nimeona, wamekuwa wakipanga waamuzi wa karibu kila mechi ya Ligi Kuu Bara, mapema kabisa. Lakini pale Yanga na Simba, wamekuwa wakiacha na sijajua hasa ni uamuzi wa kibiashara au utaratibu wa kitu fulani.
Kwa mfumo huo, maana yake ni Martin Saanya, Israel Nkongo na wewe, mmoja wao alikuwa ana nafasi hiyo. Hongera, unaipata nafasi hiyo tena.
Hii ni mara ya pili baada ya siku 402, ikiwa ni hesabu ya miaka mitatu tofauti kwa wale wenye kumbukumbu nzuri katika masuala ya soka hapa nyumbani.
Mara ya kwanza ulichezesha pambano la Simba na Yanga, ilikuwa ni Desemba 13, 2014, ulikuwa ni mchezo wa Nani Mtani Jembe. Siku 18 baadaye ukaingia mwaka 2015 uliokuwa na siku 365, halafu siku 19 za 2016, ile ya 20 utakuwa uwanjani ukizichezesha tena rimu hizo.
Ukijumlisha siku hizo za miaka hiyo mitatu, unapata 402. Unarudi kuzichezesha Yanga na Simba ambazo ziko katika presha kubwa, kila moja ikiwa katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa. Tena Simba wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mzunguko wa kwanza.
Naiangalia presha kubwa iliyo mbele yako, najaribu kukumbuka namna lile pambano ulivyoshirikiana na akina Josephat Bulali na Mohamed Mono, wote wa Tanga.
Lakini namna ulivyokuwa na hofu, ukimwaga kadi mfululizo, wakati mwingine katika sehemu hata ambayo haikuwa na sababu za kufanya hivyo.
Nakumbumba mahojiano yako baada ya mechi ile ulivyolalamika baadhi ya wachezaji kukuonyesha hali ya kukudharau, pia ukawataja majina kwamba hawakukufurahisha kabisa. Angalau Emmanuel Okwi hayupo tena Simba, anaweza kuwa salama huko aliko. Vipi wale wa Yanga na Simba ambao Jumamosi unakutana nao uso kwa uso?
Hivi kweli utakuwa uliisha wasamehe? Au utaingia na wewe kwenda kulipa kisasi kama ambavyo Simba imepania kufanya kwa Yanga. Au utataka kuwaonyesha au kuwakomoa kama ambavyo Yanga imepania kuifanya Simba?
Safari ni umepewa waamuzi wasaidizi wa Tanga, nao ni Josephat Bulali uliyekuwa naye katika mechi ya mwanzo, ila umebadilishiwa Mohamed Mono na kupewa Samwel Mtenzu. Ninaamini wataungana na wewe na kukusaidia.
Sijui yaliyo ndani ya moyo wako, niko mbali sana na wewe Sister Jonesia, Bukoba na Dar es Salaam ni hatua. Lakini moyo wa maendeleo ya soka nchini, kama unao basi mimi ninao pia.
Ndiyo maana nimeamua kuandika barua hii kwa upendo kukumbusha, kwamba ninaamini sasa umekomaa zaidi kwa kuwa wakati ulipochezesha mechi ya Simba na Yanga kwenye Mtani Jembe, mechi pekee kubwa kwako kabla ya hapo ilikuwa ni Simba dhidi ya Mtibwa Sugar.
Sasa una uzoefu, hivyo onyesha ukomavu, tulia na tuliza akili. Achana kabisa na mawazo ya kisasi au kutaka kuwaonyesha kina fulani.
Lakini ile kauli yako: “wananidharau kwa kuwa mimi mwanamke.” Ifute kabisa, kama wako walifanya hivyo ukaamini wasamehe ili uifanye kazi yako vizuri.
Pia sioni kama itakuwa ni sahihi kumwaga kadi kama njugu kwa sababu ya kutaka kutengeneza hofu ili “wasimdharau mwanamke”. Badala yake angalia usahihi kwa kuwa ninakuamini katika kusimamia sheria 17.
Nikukumbushe usajili kabla ya kuingia uwanjani, pia endelea kujiamini na nikipata muda, nitawaambia wachezaji wanaoonyesha kukudharau, “wakuache”.
Salamu kwa wazazi, usimsahau yule jirani mpenda soka. Nikutakie kila la kheri katika kazi yako Jumamosi.
Wako msemakweli.


Saleh Ally “Jembe”
 
Back
Top Bottom