Bajeti 2011/12 Serikali kitanzini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bajeti 2011/12 Serikali kitanzini

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, May 26, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  May 26, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  *Wasomi, wabunge waitaka kubadili mwelekeo wa bajeti
  *Yatakiwa iachane na tabia ya kunakili za miaka iliyopita
  *Wengi walilia bajeti itakayonusuru uchumi, kuondoa umaskini
  *Kisa ni kuyumba kwa uchumi duniani, tatizo la umeme
  Na Mwandishi Wetu
  [​IMG]


  SIKU chache kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2011/2012, sauti za kutaka bajeti hiyo ijipambanue kwa kujitofautisha na bajeti za miaka iliyopita kwa kuangalia matatizo yanayomkabili mwananchi wa kawaida, zimeanza kutikisa katika mijadala mbalimbali inayoendelea hapa nchini.


  Sababu kubwa zinazotolewa na watu wanaoibua hoja hiyo ni kwamba pamoja na takwimu kuonyesha uchumi wa nchi umekuwa ukikua kwa tarakimu zinazoridhisha, bado ukuaji huo haujajitafsiri katika maisha ya kila siku wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wakipambana kukabiliana na umasikini.


  Sababu nyingine inayotolewa kutaka bajeti ya mwaka huu ichukue mwelekeo tofauti na bajeti zilizopita ni kwamba tatizo la umeme ambalo limekuwa likiikabili nchi kwa takriban miaka mitatu mfululizo sasa, limezidi kudhoofisha uwezo wa kiuchumi wa nchi na hivyo kuwaathiri kimapato wananchi walio wengi na kuendelea kuathiri mapato ya Serikali yanayokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


  Kabwe Zitto na bajeti mbadala
  Tayari kambi rasmi ya Upinzani bungeni chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekwisha kuandaa bajeti yake mbadala ambayo mwelekeo wake uliwekwa hadharani na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi wa kambi hiyo, Kabwe Zubeir Zitto.

  Msukumo wa bajeti ya Kambi ya Upinzani bungeni hasa unatokana na dhana ile ile ya takwimu za ukuaji wa uchumi nchini zisivyokwenda sawia na ukuaji halisi wa pato la kila Mtanzania, huku bajeti hiyo ikijikita zaidi katika suala la mfumuko wa bei ambao chama hicho kinaamini pamoja na mambo mengine, kuwa unachangiwa sana na kupanda kwa bei ya bidhaa za mafuta ya petroli.

  Chanzo cha mfumuko wa bei

  Akizungumza na Rai siku chache zilizopita akiwa ziarani mkoani Mbeya, mara tu baada ya kuuweka hadharani mwelekeo wa bajeti mbadala, Zitto anasema kinachogomba katika bei ya mafuta ya petroli ni kodi na tozo nyingi ambazo walaji wanalazimika kuzitoa wanaponunua lita moja ya mafuta ya taa, dizeli au petroli, ambazo anaamini ndizo zinazochochea mfumuko wa bei.

  "Zipo kodi nyingi ambazo wananchi wanapaswa kuzijua, lakini Serikali haisemi waziwazi…kuna ile kodi ya ushuru wa barabara ambayo ni Sh 200 kwa kila lita moja ya petroli na dizeli. Hii ni kodi muhimu kwa sababu inakwenda moja kwa moja kwenye matengenezo ya barabara zetu, lakini pia wananchi wanalazimika kulipa kodi nyingine kama vile ushuru wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuna ushuru wa forodha na kodi nyingine nyingi wanapofika katika vituo vya mafuta," anasema Zitto na kuongeza:


  "Kwa ujumla kodi na tozo zote hizi huongeza bei ya lita moja ya mafuta ya petroli kwa karibu asilimia 48. Tunaweza kuziondoa kodi hizi na kutafuta maeneo mbadala ya kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu bei ya mafuta inapopungua, gharama za usafirishaji pia hupungua na hivyo kusababisha kupungua kwa bidhaa nyingine zote na hivyo kumpunguzia mzigo Mtanzania wa kawaida."


  Inawezekana mafuta kupungua kwa asilimia 50?
  Ndiyo maana katika bajeti mbadala, waziri huyo kivuli wa Fedha na Uchumi anapendekeza bei ya bidhaa za mafuta ya petroli ishushwe kwa asilimia 50, lengo kubwa likiwa ni kukabiliana na mfumuko wa bei ambao ndiyo umekuwa ukiathiri maisha ya mwananchi wa kawaida. Pia anataka misamaha ya kodi ipunguzwe kutoka asilimia 2.5 ya sasa hadi asilimia moja ili fedha zinazopatikana zisaidie kufidia pengo litakalotokana na kupunguzwa kwa kodi katika bidhaa za petroli.


  Mlengo wa bajeti hii ni kuondokana na utamaduni wa siku zote wa kutengeneza bajeti kwa kutegemea tu vyanzo vile vile, vikiwamo mishahara ya wafanyakazi serikalini, mashirika ya umma na sekta binafsi huku matajiri na wafanyabiashara wakubwa wakiachwa kuogelea kwenye ukwasi.

  Pamoja na kukiri kwamba pato la taifa limekua kwa asilimia 6.5, waziri huyo kivuli anasema sekta zinazokua kiuchumi ni zile ambazo hazimgusi moja kwa moja mwananchi wa kawaida, ambazo ni pamoja na madini, utalii na mawasiliano, ambazo zimekamatwa na zinawanufaisha zaidi wafanyabiashara wakubwa. Sekta ya kilimo ambayo inagusa asilimia 75 ya Watanzania wote, imekuwa ikikua kwa kasi ndogo mno.


  Waziri wa zamani aeleza wasiwasi wake
  Mbunge wa Magu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Festus Limbu, pia ni miongoni mwa Watanzania ambao wanauangalia mwelekeo wa uchumi wa Tanzania kwa jicho na fikra pana zaidi, akisema mwelekeo wake, ingawa kitakwimu unaonekana ni wa kuridhisha, hauwezi kuikomboa nchi na kuifanya iondokane na tatizo sugu la umasikini wa watu wake.


  Dk. Limbu aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Rais Benjamin Mkapa na kabla ya hapo alikuwa mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya kuamua kujiingiza kwenye siasa. Anasisitiza kuwa inahitajika bajeti ya kunusuru uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania.

  Kwa ufupi, Dk. Limbu anasema: "Takwimu zinazotolewa na Serikali zinaonyesha kuwa uchumi unakua, mfumuko wa bei ni wa tarakimu moja na akiba ya kigeni ipo ya kutosha kwa nchi kutumia katika kipindi cha miezi sita na nusu. Kwa kifupi uchumi mpana uko sawasawa, unapaa.

  "Lakini takwimu hizo za kiuchumi haziendani na hali halisi. Hali ya uchumi na maisha ya Watanzania walio wengi hivi sasa hakika si ya kujivunia wala kuridhisha. Bei ya bidhaa muhimu katika maisha ziko juu na wananchi walio wengi wanashindwa kuzimudu, kuna tishio la njaa kwa sababu ya upungufu mkubwa wa mvua, kuna ukosefu mkubwa wa ajira na fursa za kujiajiri. Watu hawana fedha, wanalia na umasikini, thamani ya shilingi inazidi kuporomoka kila kukicha, kitu ambacho kinazidi kuathiri uchumi na maisha ya wananchi," anasema Dk. Limbu na kuongeza:


  "Wakati nchi ikiwa inajitahidi kuondokana na athari za mtikisiko wa uchumi wa dunia, upungufu wa huduma nyeti ya umeme umeathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wetu. Uzalishaji viwandani umepungua na hivyo kodi inayokusanywa na Serikali pia itapungua. Uzalishaji wa mazao ya kilimo katika maeneo mengi utaathirika kwa sababu ya ukame.


  "Maisha yataendelea kuwa magumu. Deni la taifa katika kipindi cha mwaka mmoja tu limeongezeka kwa asilimia 18. Serikali imepunguza fedha zilizokuwa zitumike kwenye bajeti inayoendelea kwa kiasi cha Sh bilioni 510. Miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa imepangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha haitatekelezwa. Serikali pia imetumia fedha nyingi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambazo zimechangia kukuza mfumuko wa bei. Wakati huo huo, mikoa mipya mitatu na wilaya mpya 23 zinatarajia kuanzishwa katika mwaka ujao wa fedha," anasema Dk. Limbu.


  Limbu anataka nini kifanyike sasa?
  Dk. Limbu anasema kutokana na hali hiyo, halitakuwa jambo la busara kuiandaa bajeti ya mwaka ujao, yaani 2011/12 na hata ile inayofuatia, yaani bajeti ya 2012/13 kama vile hakuna kilichotokea na kinachoendelea hapa nchini na duniani kwa ujumla. Anapendekeza iandaliwe bajeti maalumu itakayorekebisha upungufu maalumu pamoja na kuandaa mazingira mwafaka ya kujenga uchumi wa taifa ulio imara na kuboresha misingi ya maisha bora kwa Watanzania.

  "Napendekeza Serikali ije na bajeti ya miaka miwili ya kunusuru uchumi na maisha ya Watanzania (A National Economic and Social Recovery Budget). Mpango wa miaka mitano uandaliwe kuanzia 2013/14. Serikali ije na bajeti itakayoachana na utaratibu uliozoeleka huko nyuma. Bajeti ya kunusuru uchumi na maisha isipandishe kodi, isimamishe matumizi yote yasiyokuwa ya lazima serikalini na kwenye vyombo vyake vyote, ujenzi wa majengo ya Serikali na idara zake mijini usimamishwe, ununuzi wa magari mapya, samani za Serikali kutoka nje ya nchi usimamishwe," anasema Dk. Limbu na kuongeza:


  "Mikoa na wilaya mpya visubiri bajeti ya 2013/14, fedha za semina zipunguzwe sana kwa kadri itakavyowezekana. Wigo wa kukusanya kodi upanuliwe zaidi, mianya ya ukwepaji wa kodi ipunguzwe na kubanwa kabisa na misamaha ya kodi ipunguzwe kwa kadri itakavyowezekana na mpango huu wa dharura utoe kipaumbele kwenye sekta chache muhimu katika uchumi."


  Atahadharisha asihukumiwe kisiasa
  Kwa kutoa maoni haya, Dk. Limbu anasisitiza kuwa hataki kujiingiza kabisa kwenye malumbano ya kisiasa, bali lengo lake kubwa ni kuhakikisha nchi inajengwa na kuimarika zaidi kiuchumi na hivyo kuboresha maisha ya Mtanzania hasa yule wa kawaida.


  Katika kuhakikisha kwamba anatoa mchango wake kwa taifa lake bila ya kujiingiza katika siasa, Dk. Limbu anapendekeza kuwa liitishwe kongamano la watalaamu wa uchumi hapa nchini ambako atakuwa tayari kutoa maelezo ya kina juu ya namna ya kutengeneza bajeti bora ambayo ana uhakika yatasaidia katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Tanzania.

  "Ni vema wataalamu wa uchumi tukaketi pamoja kuangalia mustakabali wa hali ya uchumi katika nchi yetu. Nipo tayari kutoa mwelekeo wangu utakaochambuliwa kwa kina na watalaamu wenzangu, lengo likiwa ni kunusuru uchumi wa nchi ambao naamini iwapo utaachwa kwenda kwa mwelekeo wa kawaida, utaifikisha nchi mahali ambako si kuzuri," anasema Dk. Limbu.


  Mkulo alisemaje kuhusu mwelekeo wa bajeti?
  Machi 17, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, aliwasilisha mwelekeo wa bajeti ya 2011/12, akisema Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh trilioni 11.9, huku akisema bajeti ya mwaka ujao wa fedha imezingatia zaidi nguzo kuu za kuendeleza utengamavu wa uchumi kwa ujumla, kuboresha huduma za jamii, uvunaji endelevu wa maliasili, kutumia fursa za kijiografia za Tanzania pamoja na kuendeleza teknolojia.

  Alivitaja vipaumbele vya taifa vitakavyoingia katika bajeti hiyo mpya kuwa ni pamoja na elimu, kilimo, mifugo na uvuvi, nishati, uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, afya, maji, maendeleo ya viwanda, ardhi, nyumba, makazi, maendeleo ya rasilimali watu na huduma za kifedha.


  Waziri Mkulo alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali inatarajia kuwa na matumizi ya kawaida ya Sh bilioni 7,376.3 huku miradi ya maendeleo ikitengewa Sh bilioni 4,594.0.


  Kwa mujibu wa mwongozo huo wa kutayarisha bajeti, kufikia Novemba 2010 deni la taifa lilikuwa limefikia dola za Marekani milioni 11,041.8 kutoka dola milioni 9,330.3 mwishoni mwa mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 18.


  Hata hivyo, mwongozo huo uliamsha hisia kali kutoka kwa wabunge huku wengi wao wakipinga na kusema hakuna kilichobadilika kwani vipaumbele vingi ni sawa na vya mwaka wa fedha wa 2010/2011.


  Wabunge wengi walionyesha kutoridhishwa sana na maelezo ya Waziri Mkulo, baadhi wakitaka waelezwe namna deni la taifa litakavyolipwa, huku wengine wakitaka ufafanuzi zaidi wa vipaumbele vilivyoanishwa katika mwelekeo huo wa bajeti.
   
 2. M

  Mdondoaji JF-Expert Member

  #2
  May 26, 2011
  Joined: Mar 17, 2009
  Messages: 5,106
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 145
  Ni vema waamke amasivyo Tanzania itaanguka kiuchumi mwaka huu. Hatuwezi kuvutia wawekezaji tu wakati wananchi hawana kitu mfukoni!!! Nani atanunua bidhaa za wawekezaji? Nguvu kazi ya wawekezaji itatoka wapi? Kodi ya tanzania itatoka wapi? Washauri wa rais mnajiuliza haya????
   
 3. VIKWAZO

  VIKWAZO JF-Expert Member

  #3
  May 26, 2011
  Joined: Apr 9, 2011
  Messages: 1,910
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 145
   
 4. chitambikwa

  chitambikwa JF-Expert Member

  #4
  May 26, 2011
  Joined: Nov 8, 2010
  Messages: 3,940
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 135
  Bajeti ya sigara, pombe na misamaha ya kodi
   
 5. m

  mndeme JF-Expert Member

  #5
  May 26, 2011
  Joined: Sep 2, 2008
  Messages: 322
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  kweli kabisa ni bajeti ya sigara, pombe na misamaha ya kodi.........pia chai na semina elekezi kama za ngurdoto na dodoma
   
Loading...