Bagamoyo sekondari yaelemewa, sasa yatembeza bakuli | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bagamoyo sekondari yaelemewa, sasa yatembeza bakuli

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by MziziMkavu, Mar 5, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 5, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,618
  Trophy Points: 280
  [​IMG] Vyoo pekee vinavyotumiwa na wanafunzi wa kiume zaidi ya 400 shuleni hapo.
  WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haiwezi kuwa kimbilio pekee la kila changamoto zinazozikabili shule mbalimbali hasa zile zinazomilikiwa na serikali.
  Huu ndio mtazamo wa viongozi wa shule ya sekondari ya Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani walioamua kuigeukia jamii na wafadhili kunusuru hali ya mambo shuleni hapo.
  Ni miaka 38 sasa tangu shule hiyo kongwe kwa wilaya ya Bagamoyo ilipojengwa, miundo mbinu na mazingira ya shule hayatamaniki.
  Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa shule, Sophia Kitembe, Aprili mwaka huu shule hiyo inatarajia kuendesha harambee ya kutafuta fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga upya majengo ya shule hiyo.
  “Serikali ina mambo mengi ya kufanya na imeelemewa. Ni jambo la kupongeza kuona walimu wenyewe wakiguswa na kulishupalia suala hili,’’ anasema Makamu Mkuu huyo katika mahojiano maalum na Mwananchi.
  Anasema kuja kwa Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na ule wa sekondari (MMES) iliyosababisha ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kumeleta changamoto kubwa shuleni hapo. Miundo mbinu muhimu ni michache na iliyopo ni chakavu.

  Kwa mfano hali ya vyoo ni ya kusikitisha. Takriban wanafunzi 400 wa kiume wanaoishi bwenini wanatumia matundu manane tu yaliyomo katika vyoo vinne vinavyotumika hivi sasa. Hakuna mabafu hali inayowafanya wanafunzi kuoga katika maeneo ya kufulia na yale ya wazi nyakati za usiku.
  “Eneo la vyoo na bafu limeharibika kabisa na havitumiki kwa sasa. Tatizo hilo ni kubwa na linahatarisha afya za wanafunzi wa shule hii,’’ anafafanua.
  Kwa upande wake, mwenyekiti wa harambee ya kukusanya fedha, Evodius Chilipweli anasema mazingira na miundombinu muhimu shuleni hapo hayawavutii wanafunzi hali anayodai pia ndiyo iliyochochea kwa kiwango fulani vurugu za wanafunzi miaka michache iliyopita.
  “Shule imekuwa ikifanya vizuri na hata zile fujo zilizokuwa zamani ni kwa sababu mazingira hayakuwa rafiki,’’ anabainisha Chilipweli ambaye pia ni Mwalimu Msaidizi wa Taaluma shuleni hapo.
  Ukitoa ukosefu wa vyoo vya kutosha, mabweni nayo yako hoi. Ni dhahiri kuwa miaka 38 tangu yalipojengwa hayakufanyiwa ukarabati wowote hali inayohatarisha usalama wa wakazi wake.
  “Mabweni yanaonekana kuwa ni mazuri kwa nje, hii inatokana na ujenzi makini na imara uliofanywa. Ndani ya mabweni hayo sura ni tofauti, kingo za ngazi zimechakaa na kubaki tupu na kuhatarisha usalama wa wanafunzi,’’ anaeleza.
  Wakati mabweni kwa wanafunzi wa kiume yakikabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu hali kwa wanafunzi wa kike si ya kuridhisha pia. Jengo lililojengwa kuchukua wanafunzi 54 hivi sasa lina wanafunzi zaidi ya 80.
  “Shule inahitaji bweni jipya la wasichana litakalochukua kiasi cha wanafunzi 320. Shule inalazimika kuongeza wasichana na kufikia 320,’’ anataja mahitaji halisi ya bweni kwa wanafunzi wa kike.
  Anasema uchakavu wa madarasa na kutokuwapo kwa uzio shuleni hapo ni masuala mengine yanayowapasua kichwa wadau wa shule hiyo. Baadhi ya madarasa mapaa yake yametitia na hata hali ya ulinzi si madhubuti kwa ukosefu wa uzio katika shule hiyo yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100.
  “Kwa kuwa hakuna uzio basi utoro ni mkubwa na pia upotevu wa mali za shule. Hata watu wameanza kuvamia maeneo yetu,’’ anabainisha.
  Kwa mujibu wa Chilipweli, kauli mbiu ya harambee hiyo ni ‘’Shiriki katika kujenga na kulea kizazi chenye kuwajibika na kujali kwa kuchangia katika kusaidia na kuboresha elimu na mazingira ya kujifunzia kwa watoto wetu,’’ kauli mbiu hiyo inalenga makundi kadhaa ya kjamii kama watu wote waliosoma shuleni hapo na wazazi wa wanafunzi.
  Makundi mengine ni wahisani wa ndani na nje, wafanyabiashara, wakazi wa Bagamoyo, taasisi na mashirika na wafanyakazi wa shule hiyo waliopita na wa sasa.
  Kwa pamoja walimu Kitembe na Chilipweli wanatoa wito kwa wadau wa elimu na jamii kwa jumla kujitokeza na kuwapa sapoti katika juhudi za kuipa sura mpya na ya kisasa shule hiyo iliyo mojawapo ya shule tegemeo kwa wakazi wa Bagamoyo na nje ya wilaya.
  Shule ya sekondari ya Bagamoyo ilijengwa na kuanza kutoa masomo ya sekondari mwaka 1972 ikiwa shule ya kutwa na bweni kwa wanafunzi wa sekondari ya kawaida.
  Kwa sasa shule hiyo imebaki kuwa ya bweni pekee huku ikiwa katika hatua za mwisho za kuwa shule ya sekondari ya juu. Imekuwa na matokeo ya wastani katika mitihani ya kitaifa kwa vidato vya nne na sita.
   
Loading...