Bagamoyo iliyosahaulika inavyolikosesha taifa mapato

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
ngome-kongwe-bagamoyo-2.jpg
Na Florence Majani
Unapoingia katika mji wa Bagamoyo unalakiwa na taswira ya mji nyamavu, usio na purukushani wala shughuli nyingi.Hii ni tofauti sana na hapo zamani. Kwani hata Mjerumani Franz Ferdinand Mueller, mnamo mwaka 1888 aliusifia mji huu kwa mapana na kusema:

“ Bagamoyo ni mji wenye bandari kuu katika upwa wa Tanganyika, mji wenye mitaa myembamba, mawe ya ajabu, nyumba za waafrika, soko lenye purukushani, na vito vya thamani”

Maneno ya Franz yanahakiki ukweli kuwa, hapo zamani Bagamoyo lilikuwa ni jiji katika nchi ya Tanganyika.
Lakini Bagamoyo hii, hivi sasa imepwaya, haina wafanyabiashara zaidi ya hoteli chache, wasanii wa vinyago wanaofanya kazi katika mazingira duni na wafanyakazi wa idara ya maliasili katika majengo ya makumbusho.

Pamoja na kubeba kumbukumbu adhimu na yenye kusisimua, Bagamoyo haina umaarufu kama ule wa makumbusho ya visiwa vya Zanzibar, Olduvai Gorge au mbuga za wanyama za Ngorongoro. Na hilo linathibitishwa na idadi ndogo ya watalii wanaoingia hapo kwa mwaka.

Na kwa hilo Bagamoyo, mji wa kale ambao ni maarufu sana duniani kutokana na kutambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni – UNESCO kama moja ya urithi wa dunia unashindwa kupata pato la kutosha kupitia sekta ya utalii.

Ndani ya mji wa Bagamoyo zipo mali kale chekwa ambazo ni vivutio tosha vya utalii kuliko makumbusho mengine yoyote hapa Tanzania. Ni sehemu inayobeba historia ya Tanganyika na uhusiano wake na nchi nyingine duniani.
Kwa nini Bagamoyo imesahaulika?

Mkurugenzi wa Maliasili,Utalii na Mazingira Donatious Kamamba anasema, kubwa linaloyafanya makumbusho ya Bagamoyo yasivume kama mengine, ni kukosekana kwa matangazo. “Hayatangazwi vya kutosha na ndiyo maana unaona hata wageni wanaofika hapa ni wachache iwe wa ndani hata nje. “

Hata Waziri wa Maliasili, Ezekiel Maige naye alipasua lake na kudai kuwa, Wizara ya Maliasili ina bajeti finyu isiyotosheleza mahitaji na pia, hatua ya hazina kuitaka TANAPA kuchangia asilimia 10 ya mapato nayo imepunguza uwezo wa wizara wa kutangaza vivutio kwa nguvu kubwa zaidi.

Ukweli ni kwamba, Bagamoyo ilitakiwa iwe na umaarufu kama ule wa zamani, enzi za biashara ya utumwa, na pembe za ndovu. Bagamoyo ilikuwa ni kituo kikuu cha biashara na hapa kuna historia kubwa.
Umaarufu wa Bagamoyo uliofikia upeo na kama makao makuu ya serikali ya kwanza ya mkoloni wa Kijerumani aliyeitawala Tanganyika haupaswi kupotelea upotelee hewani mithili ya moshi wa moto wa kuni au nyasi kuni, bali unatakiwa kuenziwa na kutukuzwa.

Jambo jema ambalo serikali na watanzania wanalopaswa kufahamu kuhusu Bagamoyo kuwa ni moja ya miji michache sana duniani ambayo imeteuliwa na UNESCO kuwa urithi wa duniani. Hii inatokana na mji kuwa na historia iliyotukuka na inayotakiwa kuhifadhiwa kwa faida ya dunia. Bagamoyo, kwa hiyo ni mji wa kimataifa.

Makumbusho ya Bagamoyo yalianzishwa mwaka 1957 na hata sheria ya maliasili ya mwaka 1994 ilisisitiza zaidi kuwa, vitu vyovyote vilivyotengenezwa kabla ya mwaka 1863 vinatakiwa kuwa kumbukumbu za utamaduni. Sheria inampa madaraka waziri kutangaza chochote kinachoweza kuwa kumbukumbu ya taifa.

Kwa nini Bagamoyo ni kivutio kikubwa?
Bagamoyo kuna historia kubwa mno kwa watanzania na dunia kwa ujumla. Inasadikiwa kuwa hapa ndipo dini zote mbili kuu yaani Uislamu na Ukristo zilipoingilia kwenda bara na ushahidi upo wa kanisa la kwanza katika mji huo pamoja na msikiti wa zamani sana unaokadiriwa kuwa na miaka 800.

Caravan Serai: hoteli ya misafara ya watumwa
Unapofika Bagamoyo kilomita 70 kutoka Dar es Salaam aghalabu utakutana na jengo hili ambalo lilijengwa mwaka 1860 na mhindi mashuhuri, Magram Awadh.

Hili ni eneo ambalo misafara ya watumwa ilikuwa ikikutana. Hapa ilikuwa ni sehemu ya makutano kwa ajili ya biashara zote. Ni eneo la kumbukumbu ya biashara ya pembe za ndovu na watumwa katika karne ya 19.
Ndani ya Caravan Serai utakuta picha za misafara ya watumwa, mali ambazo wafanyabiashara wa Kiarabu na Kihindi walibadilishana kwa watumwa na hali kadhalika zawadi ambazo machifu wa Kiafrika walipewa na wakoloni kwa kubadilishana na pembe za ndovu, shanga na dhahabu. Machifu wa kiafrika walipewa nguo za pamba, bakuli za udongo na vioo.

Ngome Kongwe
Mbali ya Caravan Serai, lipo jengo linalotambulika kama Ngome Kongwe, hii lilijengwa na Abdallah Selemani Marhab na mtu huyu alilitumia kama makazi yake.
Kutokana n uzuri na ukubwa wake, jengo hili baadaye lilitumiwa na Sultani wa Zanzibar kama makazi yake mnamo mwaka 1884 hadi 1919.

Kadri dunia ilivyokuwa ikibadilika ndivyo matumizi ya jengo hili la Ngome Kongwe yalivyobadilika, baadaye jengo lilitumika kama ngome ya jeshi la Wajerumani. Hata hivyo mwaka 1919 lilitumika kama gereza hadi mwaka 1974. Na mwaka 1974 hadi 1992 lilitumika kama makao makuu ya polisi ya wilaya ya Bagamoyo na sasa linamilikiwa na idara ya mambo ya kale.

Kibanda cha Kinyamkela
Lakini pia, kipo kibanda cha Kinyamkela. Hiki ni kibanda cha ajabu ambacho wakazi wa Bagamoyo walikitumia kufanya matambiko mbalimbali yakiwemo kuomba kuondokewa na balaa, kuponywa maradhi na kuomba heri katika kibiashara au jamii.

Bagamoyo ulikusanya watu na wafanyabiashara kutoka nchi nyingi zikiwemo bara Hindi, Uarabuni, Uajemi na hata Ulaya. Ni eneo ambalo limemeza siri nyingi ambazo pengine nyingine zinawagusa mababu wa babu zetu na kugusa kwa undani kabisa juu ya historia yetu.
Hivyo basi makumbusho haya kama anavyosema mbunge wa Kahama, James Lembeli kuwa ni urithi wa dunia- ni dhahabu isiyokwisha - ni tunu dhabiti kwa kizazi cha sasa na kijacho- hivyo hayana budi kutunzwa na kutangazwa.
 
Ahhh nyumbani ni nyumbani hata kama kukiwa ni juu ya mlima ni nyumbani tu....................






 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom