Josephat Gwajima ni Askofu na mwanzilishi wa kanisa la 'Glory of Christ Tanzania Church' GCTC (Ufufuo na Uzima Ministries), kadhalika ni mwanasiasa ambaye mwaka 2020 alichaguliwa kuwa
mbunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
Askofu Gwajima amekua akifuatiliwa kwa karibu na watu wengi nchini Tanzania kutokana na kile alichokisema tarehe 24 Mei, 2025 alipofanya
mkutano na waandishi wa habari ambapo alieleza uwepo wa mlolongo wa matukio ya watu kutekwa pamoja na kupotea hivyo kutokana na hayo aliamua kuitisha mkutano na waandishi wa habari kuongelea kuhusu suala hilo na kisha kutoa ushauri wake.
Juni 12, 2025 ilitolewa
taarifa ya kulifutia usajili kanisa la Askofu Gwajima likidaiwa kuingilia masuala ya siasa kwa nia ya kuichonganisha Serikali na Wananchi na baadaye waumini wa kanisa hilo kuzuiliwa na jeshi la polisi kufanya ibaada katika kanisa hilo.
Ipo
video iliyochapishwa katika mtandao wa YouTube ikimuonesha Askofu Gwajima akiambatana na walinzi wake kwenda kuchukua fomu ya kutia nia ubunge jimbo la Kawe ikidaiwa kuwa ni ya mwezi Juni, 2025.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia Google Reverse Image Search umejiridhisha kuwa kipande cha video kinachomuonesha Askofu Josephat Gwajima akienda kuchukua fomu ya ubunge jimbo la Kawe si ya mwaka 2025.
Video hiyo ni ya tukio la
Julai 14, 2020 ambapo Gwajima alienda kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa jimbo la Kawe kupitia Chama cha mapinduzi (CCM)