"Asiyekubaliana na hilo akae pembeni tu ili waliobaki waendelee" Rais Magufuli

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
RAIS John Magufuli amewataka makatibu na manaibu makatibu wakuu walioapishwa kukubali ahadi ya uadilifu wa viongozi na asiyetaka akae pembeni.

Akizungumza baada ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema hakuna aliyelazimishwa kula kiapo cha ahadi za uadilifu wa uongozi wa umma, hivyo asiyetaka akae pembeni.

“Tusije tukawa tunazungumza hapa kwa ‘generalization’ (kwa ujumla), lakini kumbe si wote wanakubali hayo masharti kama vile rushwa na kadhalika, kutoa vitu kwa upendeleo. Kwa hiyo mimi niwaombe makatibu wakuu pamoja na kwamba mmeshaapa kwangu; ambaye hakubaliani na hilo asimame pembeni tu ili waliobaki waendelee,” alisema Rais Magufuli.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alirudia kauli hiyo kwa kusema: “Mheshimiwa Rais na mimi nauliza, kuna ambaye masharti haya yanamkwaza hataki kubanwa nayo? Kama hakuna naomba tusimame kila mtu asome akitaja jina lake,” alisema Balozi Sefue.

Hata hivyo, hakuna Katibu wa Naibu Katibu Mkuu aliyejitoa kwa kukataa masharti hayo bali wengine walionekana wakitabasamu kwa tamko hilo.

Awali akisoma ahadi hizo, Kaimu Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, alisema ahadi hizo zimezingatia maadili yaliyoainishwa katika ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1995.

Alizitaja ahadi hizo kuwa ni pamoja na; kuwa mzalendo kwa nchi na kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa mwadilifu na mfano kwa watumishi wa umma na watu wengine katika kusimamia maadili, kutotumia cheo na wadhifa kwa masilahi binafsi, kwa familia na marafiki bali kwa masilahi ya umma.

Nyingine ni kulinda na kutumia rasilimali kwa masilahi ya umma, kutekeleza majukumu na uamuzi kwa kutumia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa masilahi ya umma.

“Sitaomba, kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa, sitaomba, kutoa wala kupokea zawadi au fadhila za kiuchumi, kisiasa za au za kijamii zisizoruhusiwa na sheria.
“Sitatoa shinikizo kinyume cha sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji wa kazi za umma. Nitatenda kazi kwa kuepusha migongano ya masilahi ya aina yoyote na endapo utatokea, uamuzi wangu utazingatia masilahi ya umma,” alisema Kipacha.

Aliendelea kusoma: “Nitatoa huduma bora kwa watu wote bila kujali misingi ya dini, siasa, ukabila undugu, ukanda, jinsia au hali ya mtu. Nitaepuka tabia ambayo inavunja heshima ya uongozi wa umma hata nitakapokuwa nje ya mahali pa kazi au nitakapoacha kazi.”
 
Safi sana Magufuli, mwenyezi Mungu azidi kukupa afya njema na kukulinda dhidi ya wanaokuombea mabaya
 
Back
Top Bottom