Anna Henga - LHRC : Ukeketaji umepungua lakini jitihada bado zinahitajika

Anna Henga - LHRC : Ukeketaji umepungua lakini jitihada bado zinahitajika

News Tz1

Member
Joined
Nov 28, 2025
Posts
25
Reaction score
30
Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya – Tanzania (TDHS 2022), kiwango cha ukeketaji kimepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2015/16 hadi asilimia 8 mwaka 2022 miongoni mwa wanawake wenye umri wa miaka 15–49.

Utafiti huo unaonesha kuwa asilimia 34 ya waliokeketwa walifanyiwa vitendo hivyo wakiwa chini ya umri wa miaka 5, mara nyingi kwa kisingizio cha kutibu lawalawa au madudu, hasa katika Kanda ya Kati. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 28 walikeketwa wakiwa na umri wa miaka 10–14.

Zaidi ya hayo, taarifa inaeleza kuwa asilimia 55 ya ukeketaji hufanywa na wakunga wa jadi, huku asilimia 26 ikifanywa na mangariba.

Mikoa inayoongoza kwa viwango vya ukeketaji ni Arusha (43%), Manyara (43%), Mara (28%), Singida (20%), Tanga (19%) na Dodoma (18%).

Akizungumza leo, Februari 6, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, akisoma tamko la pamoja la mashirika takribani 30 yanayopinga ukeketaji nchini Tanzania, amesema kuwa licha ya hatua zilizopigwa, bado zinahitajika jitihada zaidi ili kupunguza kwa kasi vitendo vya ukeketaji.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni kutungwa kwa sheria maalum ya kupinga ukeketaji itakayolinda pia wanawake watu wazima.

Amesema kuwa Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa sasa inazuia ukeketaji na kulitambua tendo hilo kuwa ni kinyume cha sheria linapofanyika kwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18.

Ameongeza kuwa maboresho ya sheria hiyo yatasaidia kupanua wigo wa ulinzi na kuwalinda wanawake wote, tofauti na ilivyo kwa sasa.

Sambamba na hilo, mashirika hayo yameshauri kuwekwa kwa uwajibikaji wa wazazi, walezi na viongozi wa mila wanaohusika au kuruhusu vitendo vya ukeketaji.

Ikumbukwe kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji huadhimishwa kila mwaka tarehe 6 Februari, tangu ilipotambuliwa rasmi mwaka 2003 kufuatia azimio maalum la Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo lilitokana na tathmini ya kina iliyoonesha kuwepo kwa madhara makubwa ya kimwili, kisaikolojia na kijamii yanayotokana na vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike.
 
Back
Top Bottom