Angalia Pumba za Polisi wa tz

Shiefl

Senior Member
Oct 31, 2010
145
32
Mauaji ya Arusha: Polisi inawadanganya raia
ban.blank.jpg


Barnabas Maro​

amka2.gif
BAADA ya ghasia za Arusha zilizosababisha vifo vya watu watatu akiwamo raia wa Kenya na wengine kadhaa kujeruhiwa kwa risasi za moto, sasa Jeshi la Polisi linajaribu kujikosha kwa kutoa taarifa yenye utata.
Jeshi la Polisi linasema tarehe 31 Desemba, 2010 lilipokea barua ya CHADEMA yenye Kumb. Namba CDM/AR/W/20/10 kulitaarifu Jeshi hilo dhamira ya kufanya maandamano na mkutano wa hadhara tarehe 5 Januari, 2011.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini, aliijibu barua ya CHADEMA kwa Kumb. Namba AR/B.5/Vol II/63 ya tarehe 4 Januari, 2011 akiruhusu maandamano na mkutano siku iliyofuata, yaani tarehe 5 Januari, 2011 kama ilivyoombwa na CHADEMA.
Polisi inadai kuwa taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa katika kipindi cha wiki moja kuishia tarehe 4 Januari, 2011, “zilionesha kwamba kuna matishio makubwa ya kiusalama na kwamba yalilenga kuharibu sura ya mji wa Arusha katika uso wa dunia (ukizingatia Arusha ni mji wa kitalii).”
Polisi inasema “taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa katika kipindi cha wiki moja kuishia tarehe 4 Januari, 2011 zilionesha matishio makubwa ya kiusalama”. Wiki moja ina siku saba. Kama taarifa za kiintelijensia zilikusanywa kwa wiki moja iliyoishia Januari 4, 2011, basi ina maana taarifa hizo zilikusanywa hata kabla ya CHADEMA kuliandikia Jeshi hilo barua ya tarehe 31 Desemba, 2010.
Fikiri barua ya CHADEMA kwenda Polisi ilikuwa ya tarehe 31 Desemba, 2010 na Polisi iliijibu CHADEMA Januari, 4 2011.
Tangu Desemba 31, 2010 mpaka Januari 4, 2011 ni siku tano ambazo hazikamilishi wiki moja yenye siku saba. Kama taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa kati ya Desemba 31, 2010 na Januari 4, 2011 zilibainisha uvunjifu wa amani, ilikuwaje mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha aijibu CHADEMA tarehe 4 Januari, 2011 kuiruhusu kuandamana kwa amani na kufanya mkutano wakati tayari kulikuwa na taarifa za kiintelijensia za uvunjifu wa amani?
Wakati naandaa makala haya, Polisi ilitumia vituo vya runinga kuonesha baadhi ya picha za matukio ya Arusha. Picha hizo zinaonesha kuwa wafuasi wa CHADEMA ndio waliofanya fujo. Wasichoelewa wananchi ni kwamba picha zile zilihaririwa kitaalamu kwa kuondoa maeneo yaliyohusu askari kupiga waandamanaji. Badala yake walionesha picha za raia waliokuwa wakijihami kwa kujibu mapigo!
Ikumbukwe kuwa wananchi kujumuika pamoja, kuandamana na kujieleza ni miongoni mwa haki ya kikatiba kwa wananchi. Hivyo, Polisi haitakiwi kuombwa kibali wala kuzuia maandamano na mikutano.
Kinachotakiwa ni kuliarifu tu Jeshi hilo ili lipange askari watakaohakikisha amani na usalama wa wananchi na mali zao. Hili la Polisi kutoa kibali ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Suala la Polisi kuzuia maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani si geni. Karibu nchi nzima vyama vya upinzani vinapotaka kufanya maandamano na mikutano, huzuiwa na Polisi kwa madai ya kutokuwa na askari wa kutosha. Linapokuja suala la kuwasambaratisha wanachama na wapenzi wa upinzani, askari huwapo, tena wengi wakiwa na silaha za moto.
Polisi inajikanganya kwa kutoa sababu tatu kuu za kuzuia maandamano kule Arusha kuwa ni: i) uharibifu wa mali binafsi na za serikali; ii) mipango ya utekaji wa vituo vya polisi na kambi za makazi ya askari wa Jeshi la Polisi na iii) kuvuruga mfumo wa utawala wa sheria.
Sababu zote tatu zilizotolewa na intelijensia ya Polisi haziingii akilini. Kama kazi kuu ya Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, ilikuwaje watu wauawe, wejeruhiwe na baadhi ya mali zao kuharibiwa wakati wa maandamano?
Kama Polisi inajua dhahiri kuwa mpinzani mkubwa wa CCM ni CHADEMA kwa nini isiweke ulinzi kwenye ofisi za CCM na maeneo ambayo ilidhani yalikuwa hatarini kushambuliwa?
Polisi inadai eti kulikuwa na mpango wa utekaji wa vituo vya Polisi na kambi za makazi ya askari wake. Kweli raia wasiokuwa na silaha wanaweza kuthubutu kuteka vituo vya Polisi, penye silaha za moto, na kuingia kwenye kambi za makazi ya askari mikono mitupu? Hawajipendi?
Kwa waliobahatika kuona picha halisi za matukio yale kupitia vituo vya runinga walishangazwa kwa jinsi askari walivyokuwa wakiwashambulia wananchi kwenye mkutano pale NMC. Walipigwa virungu, mateke, kukatwa mtama na kurushiwa risasi za moto. Kudhihirisha askari walikuwa na dukuduku fulani dhidi ya CHADEMA, walionekana wakilishambulia gari jekundu la mbunge wa viti maalumu kwa kuvunja vioo na kuwalazimisha waliokuwa ndani washuke ili wapate mkong’oto! Gari lile lilikosa nini kama si wivu na chuki?
Tunajua askari akiamriwa kufanya jambo hufanya ili kutii amri ya mkubwa. Hata hivyo wanafundishwa sheria za kumkamata mtuhumiwa na kumfungulia mashitaka bila kumhukumu kwa kumpiga au kumtoa roho! Nguvu hutumika pale tu mtuhumiwa anapokataa kutii amri ya kukamatwa/kuwa chini ya ulinzi.
Askari wanapaswa kutumia hekima wanapotenda kazi zao. Wakiambiwa kufanya jambo wanaloona ni kinyume cha utaratibu/sheria, wana kila sababu ya kukataa.
Kwani hawausomi msahafu (PGO) wao kujua mema na mabaya? Wale waliowashambulia kwa virungu na silaha za moto wangekuwa ndugu zao wangefanya hivyo?
Mashuhuda wanasema maandamano yalianza kwa amani kutoka hoteli ya kitalii ya Mount Meru lakini yalipofika katikati ya safari, askari wakaanza kuwashambulia watu na kuwapiga.
Hapo ndipo vurumai zilipoanza kwa waandamanaji kujihami kwa kurusha mawe huku askari wakitumia risasi za moto. Kwa nini askari hawakufuatana na waandamanaji mpaka kwenye uwanja wa mkutano na yeyote aliyeonekana kuhatarisha amani akamatwe?
Katika purukushani hizo, watu watatu waliuawa, mmoja wao akiwa raia wa Kenya aliyekuwa katika shughuli zake. Raia wa Kenya aliyeuawa katika vurugu hizo alitajwa na Polisi kuwa George Mwita Waitara wa Tanzania kumbe jina halisi ni Paul Njuguna Kayele, raia wa Kenya! Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliwaonyesha waandishi wa habari kitambulisho cha raia huyo wa Kenya.
Je, Polisi walipata wapi jina la George Mwita Waitara na kwa nini walitumia jina la uongo? Walitaka kumficha nani na kwa madhumuni gani? Tangazo la ukurasa mmoja unusu lililotolewa na Polisi kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 15, Januari, 2011 ukurasa wa 14 na 15 halikueleza ni kwa nini Polisi walitangaza jina la uongo la raia wa Kenya aliyeuawa!
Tukio zima la Arusha ni kama lilipangwa kwani mpaka naandika makala haya, si Rais, Waziri Mkuu wala kiongozi yeyote wa serikali aliyetoa salamu za rambirambi kwa wafiwa. Kinachoshangaza ni kwamba Rais Kikwete alipoongea na mabalozi wa nchi za n-nje walio nchini alisema “tukio lile ni la bahati mbaya!” Itakuwaje bahati mbaya wakati askari waliwaua kwa makusudi raia wasio na silaha?
Kioja kingine ni wakati wa kuaga miili ya marehemu kutoka chumba cha maiti kwenye Hospitali ya mkoa wa Arusha mpaka viwanja vya NMC Unga Limited. Hakuna askari yeyote aliyejishughulisha ingawa walionekana askari wa usalama barabarani waliorundikana kando ya barabara kama watazamaji! Tangu mwanzo mpaka mwisho wa shughuli hiyo hakukuwa na uvunjifu wa sheria.
Kama ni vurugu, basi zingetokea siku ya kuaga kwani ilikumbusha machungu na majonzi ya kujeruhiwa/kufiwa na raia wasiokuwa na hatia.
Bila shaka serikali iliwaamuru askari kutojishughulisha kwa lolote ili kutokee vurumai, ipate sababu za kuhalalisha mauaji ya raia wale wawili wa Tanzania na mmoja wa Kenya.
Mambo hayakwenda kama walivyotarajia, ndipo sasa wanatumia fedha za umma kutoa matangazo magazetini kutetea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Ingawa Polisi imetaja watu wanaochunguza tukio lile kuwa ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha na Mwanasheria Mkuu wa serikali, ni vigumu ukweli kuwekwa wazi. Kama walificha jina la raia wa Kenya aliyeuawa watashindwa kudanganya kuwa chanzo cha vurugu ni waandamanaji wa CHADEMA? Maana kesi ya nyani akipelekewa ngedere haki haitapatikana.
Nikumbushe jambo hili: Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana, mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM kule Maswa, alimkata mtama askari aliyekuwa Mkuu wa kituo cha Polisi akishinikiza mpinzani wake akamatwe. Mpaka leo hatujasikia hatua alizochukuliwa mgombea yule ambaye hata hivyo alishindwa uchaguzi.
Ili umma wa Watanzania uridhike kwenye uchunguzi huo, wawepo wanasheria wa CHADEMA, Serikali, taasisi za Haki za Binadamu, viongozi wa dini na watu walioshuhudia tukio lile. Ole serikali; mwanzo wa ngoma ni lele!
Source: Tanzania daima
 
Hizi aibu za Police ni hadi lini? Au hadi tuwe kama Tunisia ndio watatuheshimu?
 
Watanzania, naona kabisa 'Tunisia' haizuiliki kutokomesha kabisa hizi hila zote za CCM, ufisadi, dharau na utapeli mwingi ili watu tukaanze upya kwenye ukurasa mwingine kabisa.

Kansa ya CCM katika jamii yetu haivumiliki.
 
Back
Top Bottom