Anayetafutwa na CAG Oman kitendawili
UAMUZI wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutuma wawakilishi kwenda nchini Oman kuzungumza na mmiliki wa kampuni ya PiperLink, ambaye bado uwepo wake una utata, unazidi kuzua hali ya wasiwasi.
Mmiliki huyo amefahamika kwa jina la Issa Mohamed na uchunguzi wa gazeti hili umeshindwa kupata anuani yake, picha yake wala taarifa za kampuni hiyo kupitia tovuti au mitandao yoyote ya kijamii.
Hata hivyo, vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili kutoka ndani ya serikali vimeeleza kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba ‘mmiliki' huyo anaweza kuwa hayupo isipokuwa jina hilo lilitumika tu kwenye kufanikisha uuzaji tata wa kampuni ya Independent Power (IPTL).
Septemba 9, mwaka 2010, PiperLink ilidai kununua hisa za kampuni ya Mechmar iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya IPTL kwa gharama ya shilingi milioni sita za Tanzania na baadaye ikaja kuziuza hisa hizo hizo kwa Kampuni ya Pan African Power (PAP), kwa gharama ya shilingi milioni 500.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na Kaimu CAG, Francis Mwakapalila, wiki iliyopita ilieleza tu kwamba uchunguzi wa suala hilo la fedha za IPTL bado unaendelea na unaweza kuchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ndiye aliyefichua kwamba wachunguzi wa CAG wanakwenda Oman ingawa hakufahamu wanakwenda kumuhoji nani.
Duru za kiuchunguzi za gazeti hili zimeeleza kwamba ofisi ya CAG inashindwa kutoa muda wa mwisho wa kukamilisha uchunguzi kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa hiyo ya kumpata mmiliki huyo wa PiperLink.
"Kuna mambo mawili yanachanganya kidogo kuhusu huyu bwana ambaye anatafutwa Oman. Mosi, alinunua hisa za Mechmar katika kipindi ambacho ilikuwa imetangazwa mufilisi.
"Duniani kote, sheria iko wazi kwamba mtu hawezi kuuza hisa za kampuni ambayo iko chini ya mufilisi. Sasa tunajiuliza ni kwa vipi PiperLink walinunua hisa za Mechmar katika mazingira haya?
"Pili, kampuni zote mbili, Mechmar na PiperLink zililipa kodi ya ongezeko la mtaji siku hiyo hiyo katika tawi la CRDB la Azikiwe Desemba 5, mwaka 2013, siku moja baada ya Benki Kuu kuachia fedha za akaunti ya Escrow kwa PAP," kilisema chanzo hicho.
Gazeti hili limeambiwa kwamba ukweli kwamba PiperLink na Mechmar walilipa kodi hiyo siku moja unaibua shaka kuwa huenda mtu aliyefanya ‘mchezo' huo ni mmoja ila anatumia majina tofauti.
Ingawa ofisi ya CAG imekataa kutoa taarifa zozote kuhusiana na kinachoendelea kwa maelezo kwamba inaweza kuingilia kazi inayofanyika, Raia Mwema limeelezwa kwamba wachunguzi wana shaka kwamba inakuwaje kampuni mbili tofauti zilipe kodi kwa siku moja na katika benki moja kwa wakati mmoja, wakati zina wamiliki tofauti.
Pamoja na mambo mengine, ofisi ya CAG inataka kufahamu kwa kina kuhusu mauzo yaliyofanywa na kama yalifuata taratibu zote za kihasibu na kiserikali.
Jina la Issa Mohamed halionekani kuwa na uhusiano wowote na PiperLink katika utafutaji uliofanywa na gazeti hili, ingawa wakati wa ununuzi huo ilihifadhi hisa zake hizo za Mechmar katika Visiwa vya British Virgin Islands (BVI).
Ziara hii ya wachunguzi wa CAG imeibua hofu miongoni mwa wabunge na mawaziri kwa vile ndiyo inaonekana kuwa hatua ya mwisho katika kukamilisha uchunguzi huo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati timu ya CAG ikijipanga kwenda Oman, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe, nao wako Oman kwa ziara wakiongoza msafara wa wabunge wa Tanzania.
Haijafahamika hasa lengo la ziara hiyo ni nini lakini mmoja wa wabunge waliowasiliana na gazeti wakiwa huko, wameeleza pia kwamba suala la IPTL limetawala mazungumzo hayo.
Ikumbukwe kwamba Makinda aliwahi kutamka hadharani kuwa endapo Ripoti ya Uchunguzi wa Fedha za IPTL ingewasilishwa bungeni, baadhi ya vigogo wa serikali wangepoteza nyadhifa zao.
Akizungumza katika hafla ya kumuaga aliyekuwa CAG, Ludovick Utouh, mjini Dodoma mwezi uliopita, Makinda hakuingia kwa undani kwenye suala hilo ingawa ilitafsiriwa kwamba kuna makosa yamegundulika miongoni mwa watumishi wa serikali kwenye suala hilo.
"Asikudanganye mtu bwana, hili suala la IPTL linazungumzwa sana na wabunge. Kuna viongozi wa serikali wanaonekana kabisa kuanza kupoteza amani. Wengine wamekonda au kuwa kimya kuliko kawaida yao.
"Siwezi kubashiri kitu kitakachotokea maana mimi si marehemu Sheikh Yahya (mmoja wa waliokuwa watabiri maarufu hapa nchini) lakini ukitazama picha tu unaona hali ya hofu imetanda," alisema mmoja wa wabunge hao aliyeko Oman aliyewasiliana na gazeti hili kwa njia ya mtandao juzi jioni.
Katika sakata hilo la IPTL, kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 200 kimelipwa kwa wafanyabiashara wawili; James Rugemalira, aliyekuwa na asilimia 30 ya hisa katika kampuni hiyo na Harbinder Sethi Singh ambaye kampuni yake ya PAP ndiyo iliyonunua asilimia 70 ya hisa za Mechmar kutoka kampuni hiyo yenye utata ya PiperLink.
Fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Tegeta Escrow ya BoT baada ya kutokea kwa mgogoro baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL kutokana na gharama halisi za uendeshaji ambazo shirika hilo la serikali lilidai zilizidishwa na wawekezaji hao.
Utata uliosababisha hatimaye fedha hizo kutolewa BoT na kisha kupewa PAP na Rugemalira kupitia kampuni yake ya VIPEM ndiyo ambao sasa unachunguzwa na taasisi za serikali kama ofisi ya CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Chanzo: Raia Mwema
- Huenda ni ‘mtu hewa'
- Ni aliyeuza IPTL kwa Singh
- Makinda naye atua, hofu yatanda kwa vigogo