mimi ni mwanamke mwenye mtoto kabla ya ndoa. Nakushauri umuache huyo dada. Ushasema analia sana, hataki kutengana na mtoto wake kutokana na uzoefu wake. Nakuomba sana umuache, alie na Mungu wake kama hajiri alivyolia na Mungu wake jangwani huku amemshikilia ismail wake. Kama umeona huyo dada alishaachana na mzazi mwenzie, na wewe umeona mzazi mwenzie anamkomoa kwa kutaka kumnyang'anya mtoto akae nae au aende boarding ulitakiwa uwe upande wa huyu dada, lakini badala yake unaungana na mwanaume mwenzio kumkandamiza. Huyu dada alishakata mawasiliano na mzazi mwenzie pengine kwa kuhofia maumivu; wewe ukamtuma ampeleke mzazi mwenzie ustawi wa jamii. Jamaa amekubali kulea mtoto ila kwa masharti yake ambayo yanamuumiza mama na mtoto.
Kama huwezi kulea mtoto ambaye baba yake yuko hai, na huyo dada hayuko tayari kuwa mbali na mwanae kwa kuwa anaogopa atanyanyaswa na mama wa kambo, basi suluhisho ni kumuacha aishi single mpaka afe au mpaka akutane na mwanaume atakayekuwa-comfortable na hali yake.
Watu wengi waliongia kwenye ndoa za aina hii kwa kusitasita wana mahangaiko, ila walioingia wakijua wana changamoto gani na wakajipanga kukabiliana nazo wana furaha kwenye ndoa zao. Kwa kuwa unasita muache huyo dada. Kilio atakacholia kwa kuachwa na kidogo kuliko atakacholia kwa kutengwa na mwanae. Halafu hata sijui utakuwa na raha gani kwa kuishi na mke mwenye huzuni. Kwa ufupi hiyo ndoa bila huyo mtoto itakosa furaha kutokana na huzuni ya mke, na ikiwa na huyo mtoto bila ridhaa yako ya moyo mkunjufu itakosa furaha kwa gubu la mume. Kwa hiyo bwaga manyanga kama unampenda huyo dada.