MEI 27, 2006, Naibu Katibu Mkuu UV-CCM Bara, Amos Makala aliupotosha umma kuhusu tathmini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ya siku 100 za Rais Jakaya Kikwete madarakani.
Makala katika hotuba aliyoitoa wilayani Temeke wakati wa ziara yake ya kuwashukuru vijana wa Chama Cha Mapinduzi, alisema Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitoa kauli kuwa Rais Kikwete amekuwa mtu wa kutoa ahadi, kuzunguka na kutokaa ofisini.
Makala alidai Kikwete anafanya hivyo kuonyesha anawajali wananchi na matatizo yao na ndiyo maana anazunguka ili ajue na kufanya utafiti kwa lengo la kuyashughulikia.
Nimeamua kumjibu Makala kwa masilahi ya Watanzania wakiwamo vijana wa CCM wenyewe ambao Makala amekuwa akizungukia katika wilaya kadhaa na kuwapotosha kwa kutumia ujumbe huu.
Makala hakulielewa tamko la CHADEMA la siku 100 za Kikwete.
Katika tamko la CHADEMA, kipengele cha pili sehemu ya mafanikio, Mbowe alisema serikali imerejesha matumaini ya kinadharia kwa wananchi.
Mbowe alimsifu Rais Kikwete kwa kuonyesha kuwa karibu na wananchi na kwamba amevunja uzio uliojengwa na awamu ya tatu wa kutenga kwenye tabaka moja, viongozi wa serikali na CCM, wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa katika upande mmoja, na wapinzani, waandishi wa habari, wakulima, wafanyakazi na wananchi maskini katika upande mwingine.
Hakumaanisha asiwe karibu na wananchi wala asiwatembelee kama Makala anavyotaka kuwasadikisha Watanzania.
Ieleweke kwamba, hoja ya Mbowe si Kikwete kutokuwa karibu na wananchi bali Kikwete kushughulikia matatizo ya wananchi kwa kuipatia nchi uelekeo.
Rais amekuwa akizunguka huku na kule, mara leo yupo gerezani, kesho sokoni na keshokutwa Muhimbili, lakini kote huko hakuna matokeo ya kutosha yanayoonekana, hakuna kinachobadilika na katika baadhi ya maeneo hali imezidi kuwa mbaya.
Kikwete anayafahamu vizuri matatizo ya Watanzania. Hii ndiyo hoja ambayo CCM ilikuwa ikiisema wakati wa kampeni na kujivunia kwamba tayari alishakuwapo katika utawala kwa muda mrefu, hivyo anafahamu hali halisi ya Watanzania.
Vipi leo Makala atake Kikwete apite kuyafahamu matatizo ya wananchi? Hoja ya Makala kuwa Rais anawatembelea wananchi ili kufanya utafiti haina msingi, kwani matatizo ya Watanzania yapo wazi. Na kama itabidi utafiti ufanyike, hauwezi kufanywa na Rais kwa kuzunguka sokoni na hospitalini.
Serikali inatumia mabilioni ya pesa kudhamini tafiti mbalimbali na kama Makala anasema Rais anapita sokoni ili kufanya utafiti, kuna sababu gani ya kutumia mabilioni ya walipa kodi maskini wanaokufa kwa njaa kugharimia tafiti za umaskini?
Katika mifumo ya utawala kuna mfumo wanaita Management by Walking Around' na kipimo ni namna kiongozi anavyoweza kuzungukia na kukagua, na pili kuna Management by Results or Objectives ambapo matokeo na malengo ndiyo kigezo cha kupima mafanikio ya utawala.
Sasa Rais ameamua kutumia staili ipi? Na je, Watanzania wanataka staili ipi? Wanataka kutembelewa pekee au matokeo ya ufumbuzi wa matatizo yao ?
Kimsingi hakuna maana yoyote kwa Rais kutembelea masoko kwa madai ya kujionea hali halisi ya bei zilivyopanda halafu hakuna kitu kinachobadilika baada ya hapo.
Wala hakuna maana yoyote Rais kutembelea hospitali anakuta wagonjwa wanalala sakafuni halafu baada ya hapo hakuna kinachoendelea.
Wagonjwa hawawezi kupona kwa kutembelewa na Rais, wala bei haziwezi kushuka kwa sababu Rais katembelea soko.
Wagonjwa wanapata huduma bora na bei zinashuka kwa maamuzi ya kisera na kimwelekeo.
Rais kama kiongozi wa juu anapaswa kuwapanga viongozi watendaji wake ili waweze kutekeleza majukumu yao . Ndiyo maana tunaamini kwamba wakati umefika wa Rais kuwaongoza watendaji wengine na wao wawaongoze watendaji wa chini yao hadi tufike wakati ambapo hata mwenyekiti wa kijiji au mtaa anatembelea wananchi na kutatua kero zao.
Kwa upande mwingine, sababu ya Mbowe kumshukia Kikwete aache kuendelea kuahidi, kumetokana na ukweli kuwa wakati wa kampeni CCM ndicho chama kilichoongoza kwa ahadi nyingi.
Mathalani, Rais aliahidi kuwa serikali itaanza kujenga kiwanda cha mbolea mwaka huu, hadi sasa bado haijaeleweka hata ni wapi kiwanda hicho kitajengwa na sasa tunaelekea katikati ya mwaka.
Wakati akizitembelea wizara, Rais alidai kuwa anasikitishwa na viongozi kutembelea mashangingi huku wananchi wanakula mlo mmoja, lakini bado mashangingi yameshamili wakati wananchi wanaendelea kuteseka.
Hoja ya Mbowe si kumhukumu Kikwete katika muda huu ambao kimsingi bado ni mapema, hoja ya Mbowe ni kumuasa Rais kuendelea kuporomosha ahadi. Hii ni hoja ya kizalendo inayopaswa kuungwa mkono.
Upungufu wa Rais kutotulia na kuweka mambo sawa sote tumeuona, kwa muda mfupi tangu aingie madarakani amekuwa akitofautiana na hata mawaziri wake kuhusu mwelekeo wa masuala ya msingi.
Mathalani Rais alitangaza bei ya umeme isingepanda na kwamba lazima TANESCO ihakikishe bei inashuka, muda mfupi baadaye waziri wake wa fedha anakanusha, na kwamba bei ya umeme lazima ipande.
Nasisitiza kauli ya Mbowe kwamba Rais akae ikulu aipatie nchi visheni, tofauti na hapo atakuwa hapingani na kauli yake kuwa nchi haiwezi kuendeshwa kwa misheni town.
Source:
Nchi haiendeshwi kwa misheni town