Aliyekiuka ujenzi maghorofa Ilemela ‘hakamatiki’

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Mwandishi Wetu

SAKATA la ukiukwaji wa taratibu za ujenzi wa maghorofa matatu eneo la Nyasaka limeingia katika sura mpya baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, John Wanga, kuonyesha dalili za kuanza kumkingia kifua mmiliki husika.

Mmiliki au msimamizi husika alitakiwa kuwasilisha vibali vya ujenzi huo kama anavyo kufikia Novemba 30, mwaka huu lakini hadi Raia Mwema linafanya mahojiano maalumu na Wanga wiki iliyopita alikuwa hajatekeleza agizo hilo.

Wakati viongozi na wataalamu wa mamlaka husika wakithibitisha kuwa ujenzi wa maghorofa hayo ulikiuka taratibu zinazotakiwa, mkurugenzi huyo amesema hahitaji kujua uzembe uliochangia tatizo hilo, badala yake ataendelea kumsubiri mmiliki amwonyeshe vibali vya ujenzi huo.

Kauli hiyo ya Wanga imekuja huku ikidaiwa kuwa msimamizi wa ujenzi wa maghorofa hayo kwa sasa anatamba mtaani kwamba ametenga ‘fungu nono la kuwaweka sawa’ viongozi husika ili wamwandalie vibali feki vitakavyomnasua katika kashfa hiyo.

Miongoni mwa mamlaka zilizofuatilia na kuthibitisha kwamba ujenzi huo ulikiuka taratibu zinazotakiwa ni Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) ambayo tayari imeshachukua hatua ya kuusimamisha.



Katika mahojiano na Raia Mwema, Meneja wa CRB Kanda ya Ziwa, Evod Lyamuya, amekiri kwamba ujenzi wa maghorofa hayo ulikiuka taratibu zote zinazotakiwa.

“Pale taratibu zote zimevunjwa kwa ujumla,” alisema Lyamuya na kumtaja mmiliki wa maghorofa hayo kuwa ni Juma Changwe anayedaiwa kuwa nje ya nchi kikazi.

“Tulimwandikia barua ya wito, lakini aliyefika ofisini kwetu baada ya siku tatu ni mtoto wa Juma aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Juma. Tumempa maagizo… agizo la kwanza ni kuhakikisha anajenga uzio (kwenye majengo hayo), kisha taratibu nyingine zitaendelea,” amefafanua Lyamuya.

Aidha, hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Manju Msambya, alifuatana na wahandisi kadhaa wa manispaa hiyo, miongoni mwa wafuatiliaji wengine kwenda kujionea ujenzi wa maghorofa hayo ambapo alishangazwa jinsi wataalamu walivyoufumbia macho.

“Haiwezekani ujenzi wa ghorofa hili ukafika hatua hii bila ninyi kujua… kwa hiyo hata idara yenu haina ukaguzi? Mmeugeuza mradi wenu na kuidhalilisha serikali?”

“Sisi (Serikali) hatuna tatizo la mtu kujenga nyumba hata arobaini, lakini kwa hili ndugu zangu mtaona ninawafuatafuata,” alisema Msambya na kuwaagiza wahandishi wa manispaa hiyo kumpelekea ofisini kwake taarifa kamili kuhusu hatua walizochukua dhidi ya mmiliki wa ujenzi huo.

Mkaguzi wa Majengo wa Manispaa hiyo, Sylvanus Mashinji, amejitetea mbele ya mkuu huyo wa wilaya kwamba wamekwishamwandikia mmiliki wa majengo hayo barua ya kumtaka apeleke vielelezo vya ujenzi huo kwa wiki kadhaa sasa bila mafanikio.

“Tumemtumia (mmiliki) barua alete vielelezo ila bado hajaleta majibu, tarehe ya mwisho aliyotakiwa kuviwasilisha ilikuwa Novemba 30, mwaka huu,” amesema Mashinji na kuendelea: “Nilishapita kukagua majengo haya mara nyingi lakini nikaambiwa mhandisi wa ujenzi ambaye ni bosi wangu (hakumtaja) ndiye amekuwa akipita kukagua majengo haya, hivyo nikaona haina haja mimi kumwingilia.

“Unajua ukishaambiwa (anayefuatilia) ni mkubwa wako utahoji nini, lakini mimi nilianza kuhoji mwaka jana wakati ujenzi ukiwa kwenye msingi… mimi siwezi kumnyooshea kidole bosi wangu.”

Kwa upande wake, Mhandisi wa Manispaa ya Ilemela, Kidola Nkanda ameahidi kushirikiana na wataalamu wenzake kufuatilia kwa kina ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kuchunguza ili kubaini uwezo wa udongo wa eneo hilo na kujua kama msingi una uimara wa kuhimili uzito wa maghorofa hayo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Nkanda, iwapo ukaguzi utabaini kuwa maghorofa hayo yamejengwa chini ya kiwango cha uimara unaotakiwa, yatavunjwa ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea siku za usoni.

Siku chache kabla ya Mkuu wa Wilaya kwenda kujionea ujenzi wa maghorofa hayo, Nkanda alipohojiwa na Raia Mwema alikiri kwamba ujenzi huo haukufuata taratibu zinazotakiwa. “Tumefuatilia na kubaini jamaa (mmiliki wa majengo hayo) hakuwa na vibali,” alisema.

Wakati Nkanda akithibitisha hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Juma Kasandiko alipoulizwa na gazeti hili alidai kuwa ofisi hiyo haimfahamu mmiliki wa maghorofa hayo.

“Unajua Kidola amesema hajapata majibu ya kutosha maana mmiliki anachengachenga, bado hajajitokeza, bado anapiga chenga, labda nipe muda niwatafute wataalamu wanieleze,” alisema Kasandiko.

Kasandiko aliendelea kuitetea ofisi hiyo kwamba inapata kigugumizi cha kueleza ukweli halisi wa suala hilo kutokana na mhandisi aliyekuwa anafuatilia ujenzi huo (hakumtaja) kuhamishwa katika manispaa hiyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Wanga, ambaye awali alilieleza gazeti hili kwamba atafuatilia suala hilo na kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya wahusika waliofumbia macho ukiukwaji taratibu za ujenzi huo zinazotakiwa, kwa sasa amebadili msimamo huo katika mazingira tatanishi.

Wanga akizungumza na Raia Mwema ofisini kwake, alionyesha jazba na kutoa majibu tatanishi alipoulizwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya mmiliki wa majengo hayo na wataalamu waliozembea kiasi cha kutoa mwanya wa tatizo hilo.

“Hapa hatutafuti mzembe, tunasubiri [mmiliki] awasilishwe nyaraka, hapa issue (suala) si kuvunja [majengo], idara [ya ujenzi] bado haijaniletea taarifa ili tuamue cha kufanya,” alisema Wanga bila kueleza hatua atakazochukua dhidi ya mmiliki husika aliyekaidi kuwasilisha vielelezo vya ujenzi huo Novemba 30, mwaka huu kama alivyoagizwa.

Awali, Mkuu wa Wilaya, Msambya, alielezea kutoridhishwa kwake na maelezo aliyopata kutoka kwa wataalamu wa majengo wa manispaa hiyo kuhusu ujenzi wa maghorofa hayo.

“Nilimwelekeza Mkurugenzi (wa Manispaa ya Ilemela) akawaleta wataalamu ofisini kwangu, wakanipa maelezo ambayo hayakuridhisha,” alisema Msambya katika mahojiano na gazeti hili.

Mkuu wa Bodi ya Ubunifu na Usajili wa Majengo (AQSRB) Kanda ya Ziwa, Musa Gulaka, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Kanda ya Ziwa, Mjawa Mohamed na Ofisa Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Julius Chiza, nao wameahidi kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua stahiki.

Awali, maghorofa hayo yanayojengwa katika Mtaa wa Nyasaka yalishuhudiwa na Raia Mwema yakiwa hayana uzio na mabango yanayoonyesha majina ya mmiliki, mkandarasi, wataalamu wengine husika wa majengo na madhumuni ya ujenzi huo.

Ghorofa moja lilikutwa katika mazingira yanayohatarisha maisha ya wananfunzi wa Shule ya Msingi Pasiansi ambao wamekuwa wakilipanda na kufanya michezo mbalimbali ukiwemo wa kufukuzana.

Wakazi wa Nyasaka waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina wamedai kuwa msimamizi wa ujenzi wa maghorofa hayo amekuwa akitamba mtaani kwamba hakuna mtu wala mamlaka inayoweza kumchukulia hatua za kisheria kwani ‘amekwishaiweka serikali mfukoni’.

“Tumekuwa tukiona maofisa wa Manispaa ya Ilemela wanakuja kuweka alama za X kwenye majengo hayo kutokana na kukiuka taratibu za ujenzi wa maghorofa, lakini baadaye zinafutwa na ujenzi unaendelea kama kawaida,” amesema mkazi wa Mtaa wa Nyasaka.

Kwa upande wake, msimamizi wa ujenzi huo, Ibrahimu Juma alipoulizwa na gazeti hili kwa simu kuhusu suala hilo alikata na kuzima simu.

Raia Mwema
 
Tusiwahukumu Watendaji wa Manispaa ya Ilemela. Tusubiri kwanza uchunguzi ufanyike ili mbivu na mbichi ifahamike.
 
Back
Top Bottom