Aliyekeketa watoto 680 asema imetosha

Aliyekeketa watoto 680 asema imetosha

real G

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2013
Posts
5,227
Reaction score
5,302
UKEKE+PIC.jpg


Ni maneno yenye kujaa majuto kutoka kwa ngariba Esther Bhoke (38) mkazi wa Kijiji cha Kitarungu kata ya Nyansurura wilayani Serengeti mkoani Mara, ambaye ameamua kuachana na kazi hiyo na kukubali mikoba yenye zana zake za kazi iteketezwe hadharani.

Mama huyo mwenye watoto watano, wa kiume watatu na wa kike wawili ambao anakiri hakuwakeketa na hatawakeketa anasema, anajisikia kuwa na deni kubwa moyoni kutokana na ukatili aliowafanyia watoto hao na kuahidi kumrudia Mungu kwa toba.

Esther alifanya kazi hiyo msimu mmoja mwaka 2016 na kuwakeketa watoto zaidi ya 680 na kupata zaidi ya Sh1.5 milioni ambazo anakiri hazikumsaidia kimaendeleo na kusisitiza hakuna ngariba aliyefanikiwa kimaendeleo kwa kazi ya ukeketaji.

Anakiri ngariba watakaoendelea na kazi hiyo wako hatarini kwa kuwa mazingira yamebadilika, maana ukeketaji ulikuwa na misingi yake kimila, eneo la kufanyia, muda na wasimamizi, lakini sasa wanafanya usiku wa manane porini kwa kuhofia mkono wa sheria, mazingira hayo yalimtia hofu na kuamua kuachana na kazi hiyo.

Anasema baada ya kuugua na kufikia hatua ya kunyanyapaliwa kwa kudhaniwa ana Ukimwi alilazimika kwenda kwa mganga wa kienyeji na kupigiwa ramli kuwa mizimu inamtaka awe ngariba. “Sikuwa na ubishi, wazee wa mila wakanibariki,” anasema.

Baada ya kikao na baraza za wazee wa mila, asubuhi kitandani alikuta wembe uliotengenezwa na wahunzi, alipouliza akaambiwa ni vifaa vya kuanzia kazi, kisha akapewa shanga maalum za kuvaa wakati anawakeketa watoto kama kinga yake na kazi hiyo.

“Mama mkwe wangu kabla ya kufariki aliwahi kuniambia nikiwa mke wa kijana wake mkubwa natakiwa kuwa ngariba nisaidie watu na alinipa baadhi ya vifaa kwa maelezo yake na ya mganga na wazee wa mila nikajikuta nimeingia kwenye ukeketaji ambao ni ukatili kwani hauna kipimo rasmi cha kumkata kiungo mtoto,”anadai.

Anasema ukeketaji kwa mwaka huu unaweza kuanza likizo ya mwezi wa nne na wa sita badala ya Desemba kwa kuogopa kukamatwa. “Nilikuwa nimeshaandaliwa kwa kazi hiyo iliyopangwa kufanywa mapema, nililazimika kuomba ushauri kwa ngariba mstaafu, Christina Marwa akanishauri niachane na ukatili huo,”amesema.

Licha ya kuongozwa kwa sala ya toba na kuambiwa akiamini Mungu, mizimu haitamsumbua ana hofu kubwa ya kudhuriwa na wazee wa mila kwa kitendo chake cha kuachana na kazi hiyo, ikizingatiwa walikuwa wanamtegemea kufanya ukeketaji mapema.

“Wapo wazee ni hatari sana kwa dawa, wanaweza kunidhuru maana walinitegemea kufanya ukeketaji mapema mwaka huu, ninakabiliwa na wakati mgumu katika kipindi hiki,” anasema.

Ngariba mstaafu Christina Marwa anasema kuwa ukeketaji mwaka huu hautafuata taratibu zote za mila na desturi. “Wamebadili muda na pia watafanya nyumba kwa nyumba, hawatapeleka watoto maeneo maalum kwa hofu ya kukamatwa,”anasema.

Christina aliyestaafu mwaka 2015 akiwa amekeketa watoto zaidi ya 2000 anadai kuwa licha ya vitisho vya wazee lakini yeye hakubabaika na anaendelea na maisha yake, huku akimtaka ngariba mwenzake kusimama imara katika kupinga ukatili huo.

Mchungaji akiri mizimu ngoma nzito

Mchungaji wa Kanisa la Menonite Tanzania (Kmt) Jimbo la Serengeti Cliford Msyangi anasema ukeketaji unaongozwa na mizimu, kuondoa majini ni rahisi lakini mizimu inahitaji umakini kwa kuwa wanakuwa wameshikamana nayo, na asipofanya bidii ya kusimama kwa Mungu atapata matatizo makubwa.

Anasema kuwa vitendo vya ukeketaji ni dhambi kubwa kwa kuwa maandiko matakatifu yanabainisha kuwa wanaume ndiyo wameagizwa kutahiriwa kama sehemu ya usafi wala si wanawake kama wanavyofanya wazee wa mila.

Meneja Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti unaotekelezwa na Amref Health Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), halmashauri na wadau wengine kwa ufadhili wa UN Women, Godfrey Matumu anasema kwamba Esther ni miongoni mwa ngariba na wakunga wa jadi 78 kati ya 180 walioamua kujitokeza hadharani.

“Kuna ngariba na wakunga wa jadi 180 ambao mradi ulishawakutanisha na kuahidi kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, 78 wamejitoa hadharani ambao wameshaunda vikundi 11 vya ujasiriamali, naamini wasipotaka kubadilika sheria zitawabadilisha,”anasema.

Matumu anasema kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa makatibu wa wazee wa mila na utafiti wao, inaonyesha kuwa takwimu za ukeketaji zinazidi kushuka, “mwaka 2012 waliandikishwa watoto 15,274 na waliokeketwa ni 14,041,”anabainisha.

Anasema mwaka 2014 waliandikishwa watoto 14,122 na wakakeketwa 13,855, watoto 267 ndio walionusurika ama kwa kugoma ama wazazi wao kukataa na mwaka 2016 waliandikishwa watoto 5,621 lakini kati yao waliokeketwa ni 2,313.

“Kati ya watoto 2,313 waliokeketwa, Esther pekee alikeketa watoto zaidi ya 680, hivyo kuacha kwake kutasaidia kunusuru watoto wengi na elimu inazidi kushamiri kwa watoto na wengi wanakataa kufanyiwa ukatili huo,” anasisitiza.

Meneja huyo anasema mwaka 2012 watoto 176 walijitokeza kupinga kukeketwa na kujisalimisha kwenye maeneo mbalimbali, mwaka 2014 watoto 233 walikimbilia Kituo cha Nyumba Salama na mwaka 2016 watoto 762 walikimbilia Nyumba Salama, vituo vya polisi na makanisani.

Anabainisha kuwa kila mwaka wa ukeketaji watoto wanakufa na maiti kutupwa porini, “taarifa zinabainisha kuwa mwaka 2012 walikufa watoto saba, mwaka 2014 watoto tisa na mwaka 2016 watoto sita walikufa, wazazi, wazee wa mila na jamii hufanya siri, haya ni madhara makubwa ya ukeketaji.”

Afisa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji, William Mtwazi kutoka LHRCanasema kwamba wanategemea hivi karibuni kukutanisha viongozi wa wazee wa mila na koo zote sita kwa ajili ya kuteketeza nyembe za mangariba kutoka kila koo kama njia ya kutokomeza ukeketaji.

Anasema koo zinazojihusisha na ukeketaji wilayani humo viongozi wake walisaini mbele ya mkuu wa wilaya kuachana na ukeketaji ni Inchugu, Inchage, Warenchoka, Watatoga, Wakenye na Wangoreme.

“Tunategemea kuwapeleka Wazee Kilindi au Handeni Tanga wakajifunze namna ya kufanya unyago bila ukeketaji kama njia mbadala ya kuachana na ukeketaji, pia wanaendelea na utoaji elimu mashuleni na katika jamii kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo polisi na watu wa afya. Anasema wazee wa mila kuwa kigeugeu ni changamoto kwa kuwa wanayokubaliana wengine wanakiuka utekelezaji wa mikakati iliyopangwa.

Mtwazi ambaye ni mwanasheria anasema wadau wote wanaopinga ukatili wa kijinsia waunganishe nguvu hasa mwaka huu unaogawanyika kwa mbili ambao ukeketaji umepangwa kufanyika maeneo mengi, wafichueni ngariba, wazee wa mila na wazazi wanaojipanga kutekeleza ukatili huo.

Mkuu wa wilaya hiyo Nurdin Babu anasema wazee wa mila kuweka sahihi mbele yake kuwa wameapa kuacha ukeketaji ni imani tosha na watakaokiuka lazima watakamatwa kwani mkakati wa wilaya ni kuhakikisha wanasomesha watoto wa kike, kupiga marufuku ndoa za utotoni na ukeketaji.

Mwaka 2016 jumla ya majalada 20 yalifunguliwa polisi dhidi ya ngariba, wazee wa mila na wazazi waliobainika kujihusisha na ukeketaji, kesi nane zilifikishwa mahakamani, ngariba wawili akiwemo nguli Christina ambaye alibwaga manyanga na kuteketeza mikoba kanisani mwaka 2015 na 2016 akakamatwa akikeketa watoto anatumikia kifungo cha miaka minane,wazazi wawili na mshika unga mmoja.


Chanzo: Mwananchi
 
Yaani miAfrika bhana.., sijui tukoje! Shit hole country kabisa, lack logical reasoning inatusumbua!
 
Back
Top Bottom