Ajira za serikali kumponza Waziri Kairuki

MP CHACHANDU

JF-Expert Member
Dec 4, 2016
875
616
KATIKA sehemu ya kwanza ya uchambuzi huu jana, ilielezwa jinsi mawaziri 13 wa serikali ya awamu ya tano wanavyokabiriwa na mtihani mgumu kutekeleza bajeti ya kwanza ya serikali kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti Aprili 4.

Pia, baadhi ya mawaziri kivuli walibainisha kuwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 umekuwa wa kusuasua na kuna hatari mipango mingi ya maendeleo isitekelezeke ingawa mawaziri wana muda wa siku 122 kutekeleza bajeti zao kabla ya mwaka wa bajeti kufikia kikomo Juni 30.

Katika mwendeleo wa uchambuzi huu, leo tunaiangalia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mtihani mgumu alionao Waziri Angellah Kairuki katika utekelezaji wa bajeti ya wizara hii ni changamoto ya ajira, malimbikizo ya madeni na malalamiko ya muda mrefu ya watumishi wa umma kutopandishwa madaraja.

Ikumbukwe kuwa Juni 22, mwaka jana, Rais John Magufuli, wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, alitangaza kusitisha ajira mpya serikalini na upandishaji vyeo watumishi wa umma ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa.

Alisema uhakiki huo uliolenga kuokoa mabilioni ya shilingi ambayo serikali ilikuwa inayapoteza kutokana na kulipa watumishi hewa, ungekamilika baada ya kipindi cha mwezi mmoja hadi miwili.

"Katika kipindi cha mwezi mmoja hatutawapandisha vyeo wafanyakazi, ninaomba wafanyakazi waelewe hili, kwa sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata wafanyakazi ambao hawapo. Tunafanya ukaguzi wote, tukishamaliza wafanyakazi wataendelea kupandishwa vyeo," alisema Rais Magufuli siku hiyo.

Uamuzi huo umeendelea kupingwa vikali na wakosoaji wa serikali hususani Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo imekuwa ikidai uhakiki wa watumishi hewa ni mbinu ya serikali kukwepa kutoa ajira kwa wananchi wake na kuwaongeza mshahara watumishi wa umma.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba 4, mwaka jana, Rais Magufuli alibainisha kuwa licha ya serikali yake kusitisha ajira kupisha uhakiki wa watumishi hewa, alitoa kibali cha ajira kwa wanajeshi waliokuwa mafunzoni na wataalamu wa afya waliokuwa wanahitajika kwenye Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Ikiwa imebaki miezi minne kabla ya kufika kikomo kwa bajeti ya serikali na siku 34 kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti ya pili ya serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli, Waziri Kairuki anaonekana kuwa na mtihani mgumu kutoa ajira zaidi ya 70,000 zilizoahidiwa katika mwaka huu wa bajeti ili akwepe kibano cha wabunge kwa kuwasilisha bajeti 'hewa' bungeni.

Katika ukurasa wa 57 wa kitabu chake cha bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, Kairuki anaeleza kuwa wizara yake mwaka huu wa fedha itasimamia ajira na upandishaji vyeo kwa watumishi wa umma.

Na katika utekelezaji wa mpango huo, Desemba 7, mwaka jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Florence Temba, aliiambia Nipashe kuwa serikali itaajiri watumishi 71,496 kwenye sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya, kilimo, mifugo na viwanda mwaka huu wa fedha.

Hata hivyo, licha ya kutaja idadi ya watumishi wapya wanaotarajiwa kuajiriwa katika mwaka huu wa fedha, Temba hakuweka bayana ni lini hasa ajira hizo zitaanza kutolewa licha ya kuwa ilikuwa imebaki miezi sita mwaka wa bajeti kumalizika.

Temba alitoa maelezo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, aliyeulizwa na Nipashe kuhusu hatima ya vijana wanaosubiri ajira serikalini tangu wahitimu masomo yao mwaka 2015.

Katika mchanganuo wake, Temba alisema sekta ya elimu kutakuwa na ajira 28,957, afya 10,870, kilimo 1,791, mifugo 1,130, huku maeneo mengine ambayo hakuyataja, yakitarajiwa kuwa na ajira 28,748.

Siku saba baadaye, yaani Desemba 14, serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish, ilitangaza kuwa itatoa ajira kwa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari waliohitimu stashahada na shahada za ualimu mwaka 2015.

Hata hivyo, wahitimu katika kada tajwa hizo bado hawajaajiriwa hadi sasa huku Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikieleza kuwa kitendo cha serikali kutotoa ajira katika mwaka huu wa fedha "ni bomu".

Katika mahojiano na Nipashe jana, Ruth Mollel, Naibu Waziri Kivuli, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, alisema: "Kwa kweli bila ajira, vijana litakuwa ni bomu nchini. Uhalifu utazidi, mambo mengi yataendelea kutokea. Suala la ajira ni la msingi sana."

Alisema kambi ya upinzani kwa kushirikiana na kamati za kudumu za Bunge watafuatilia utekelezaji wa bajeti ya wizara ya Kairuki na kuhoji sababu za serikali kutoajiri wananchi wake katika mwaka huu wa fedha.

Wakati Wizara ya Kairuki ikitoa ikiyasema hayo, hivi karibuni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Ezekiah Oluoch, aliiambia Nipashe kuwa kwa sasa kuna walimu 30,000 mtaani ambao hawana ajira licha ya kuhitimu masomo yao.

Alisema hao ni wale waliomaliza masomo mwaka 2015 na kwamba walitarajiwa kuongezeka baada ya wengine kuhitimu mwaka jana.

Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Obadia Nyongela, pia aliiambia Nipashe mwishoni mwa mwaka jana kuwa kuna madaktari 1,700 mtaani ambao wana sifa, lakini hawajaajiriwa.

"Kama mwaka huu (2016) utaisha bila vibali vya ajira kutoka, maana yake mpaka mwakani kutakuwa na madaktari 2,866 wasio na ajira licha ya kuwapo kwa upungufu wa wataalamu hao," alisema Dk. Nyongela.

Aidha, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Ephata Kaaya, alisema wanaendelea kuzalisha wataalamu hao kwa sababu Tanzania bado ina upungufu wa madaktari.

MALIMBIKIZO YA MADENI
Mbali na changamoto ya ajira, katika mwaka huu wa fedha, Kairuki anatakiwa kutekeleza bajeti ya wizara yake ya kusimamia na kudhibiti mishahara hewa katika utumishi wa umma kwa kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, kuchambua na kuhakiki madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma, kuandaa mfumo utakaowezesha kuwapatia makazi ya gharama nafuu watumishi wa umma.

RUSHWA NA VVU
Kitabu cha bajeti ya Wizara ya Kairuki pia kinaonyesha mwaka huu inatakiwa kufungua ofisi ya Sekretarieti ya Ajira Zanzibar ili kurahisisha mchakato wa ajira kwa ajira za muungano na kuimarisha uhusiano wa kiutendaji.

Wizara hiyo pia inatakiwa kutoa elimu kwa watumishi kuhusu maadili ya kazi na kujiepusha na mazingira hatarishi ya maambukizi ya Virus vya Ukimwi (VVU), magonjwa sugu yasiyoambukizwa na mapambano dhidi ya rushwa na kukamilisha mwongozo wa kupendekeza na kupanga mishahara na maslahi katika utumishi wa umma.

TUHUMA 3,000
Wizara ya Kairuki katika mwaka huu wa fedha pia inatakiwa kuchunguza tuhuma 3,406 zilizopo na mpya zitakazojitokeza, kuendesha kesi 578 zilizopo mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa uchunguzi na kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa jengo la ghorofa tatu katika kampasi ya Tabora.

MIRADI 300
Wizara hiyo katika bajeti ya mwaka huu inapaswa kukamilisha miradi 300 chini ya Mpango wa Kuendeleza Miundombinu katika sekta za afya, elimu na maji pamoja na kuandaa mikutano minne ya kikanda na kimataifa na mingine minne ya kitaifa juu ya Uongozi na Maendeleo Endelevu.

Kairuki pia anatakiwa kuhakikisha wizara yake inafanya uhakiki wa matamko ya rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma 500 na kufuatilia utekelezaji wa mkakati wa uhakikisha asilimia 80 ya vituo vya afya na zahanati vinakuwa na hadhi siyo chini ya Nyota Tatu ifikapo Juni 2018.

Kairuki pia anapaswa kufuatilia utekelezaji wa mkakati wa kupunguza vifo vya kina mama na watoto kwa asilimia 20, kutoka watoto 54 kati ya 1,000 na kina mama 410 kati ya 100,000 wanaokufa kwa kuanza na Mikoa ya Mwanza, Geita, Kigoma, Mara na Simiyu ifikapo Juni 2018.

NYUMBA ZA MWINYI, KIKWETE
Waziri huyo pia anatakiwa kuhakikisha wizara yake inatoa huduma kwa viongozi wastaafu wa kitaifa na wajane wa viongozi 16 pamoja na kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na kuanza ujenzi wa nyumba ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.


Chanzo: Nipashe
 
PM bwana mwenzake hua akiona vitu vinachelewa hua anaingia jikoni mwenyewe, yeye anatishia?
Hii ni script nyingine hakuna ukweli hapa.
 
Ushauri kwa vijana walioathirika na swala la ajira, usiamini hiko ambacho amekisema waziri mkuu usipoteze muda kabisa kuweka matumaini ya hayo maneno kifupi hiyo ni sanaa.
 
acha uongo vibali vinatoka utumishi
Ajira zilisimamishwa na raisi kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa, mama Anna kilango malecela akasema mkoani kwake shinyanga hakuna watumishi hewa akatumbuliwa, bado ruhusa ya kuajiri haijatoka
 
Back
Top Bottom