Ajali za viongozi sasa zawatisha wabunge

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,044
Posted Date::10/25/2007
Ajali za viongozi sasa zawatisha wabunge
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi

HUKU wakiwa na nyuso za huzuni baadhi ya wabunge na mawaziri wameshutushwa na kutishwa na matukio ya ajali za mara kwa mara, zinazowakumba viongozi nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana kuhusu kifo cha Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto, Salome Mbatia, walisema hofu imewatanda kutokana na matukio hayo ya ajali.

Waziri wa Fedha Zakia Meghji alisema ingawa ajali zinapangwa na Mungu, lakini matukio ya ajali dhidi ya viongozi ikiwemo wa serikali yanatia hofu.

Meghji alifafanua kwamba kifo cha Mbatia, ni cha kusikikitisha ambacho pia yeye binafsi kimemuogopesha.

Alisema kwa mara ya kwanza alivyosikia taarifa hizo juzi hakuamini, lakini kilichomstua na kumuogopesha ni pale aliposikia na kuona mazingira ya ajali.

Meghji alisema Mbatia amekufa kifo kigumu na kibaya, hali ambayo inatia majozi na simanzi nzito.

"Kwakweli nimepokea kwa mstuko taarifa za kifo cha marehemu Salome, nilikuwa kwa Mkullo (Mustapher- Naibu Waziri wa Fedha), nikasikia hizi taarifa tukastuka," alisema na kuongeza:,

"Ingawa kifo ni jambo la Mungu , lakini haya matukio ya ajali kwakweli yanatisha, ametoka Mudhihir (Mudhihiri-mbunge wa Mchinga, Kapuya (Profesa Juma-Waziri wa Ulinzi), sasa huyu, inaogopesha kwakweli, lakini sawa ni kazi ya Mungu".

"Kifo ni kifo, lakini amekufa kifo kigumu na kibaya, kibaya, kibaya kweli, inasikitisha kwakweli," alimalizia kwa majonzi.

Kwa upande wake mjumbe Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Wilson Masilingi, alisema ni kweli matukio ya ajali dhidi ya viongozi wakiwemo wa serikali yameongezeka, lakini uchunguzi utatoa matokeo ya chanzo cha ajali.

Masilingi alifafanua kwamba, kama mjumbe wa kamati anaamini uchunguzi pekee ndiyo utatoa majibu ya chanzo cha ajali hiyo.

"Ajali kweli zinatisha, Mwakanjuki (Brigedia Jenerali Adam-Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, alipata ajali sasa yuko Afrika Kusini, waziri wetu Kapuya, lakini nafikiri hili la Salome uchunguzi utasema chanzo ni nini," alisisitiza Masilingi.

Monica Mbega ambaye ni mbunge wa Iringa mjini na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, alisema amestushwa na msiba huo ambao umefanya taifa kupoteza mhimili muhimu wa maendeleo.

Hata hivyo, Mbega alisema ingawa ajali ni kazi ya Mungu lakini ni wakati sasa wa madereva nao kuwa makini wakati wanapoendesha magari barabarani.

Mbega alisema baadhi ya madereva wanapokuwa katika barabara za lami, hujisahau na kuendesha bila kuangalia hatari zinazoweza kutokea.

"Ingawa ajali hupangwa na Mungu, lakini madereva wanapaswa kuendesha kwa umakini, unaweza kukuta dereva anataka kuvuka gari eneo ambalo ni gumu bila kuangalia hatari iliyopo mbele," alisema Mbega.

Alisema taifa limepoteza mtu mchapakazi, mwenye msimamo, muwazi na ambaye hakuwa akikata tamaa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Utawala, Tatu Ntimizi alielezea kuguswa na kifo cha Mbatia na kusema kuwa taifa limepoteza kiongozi hodari.

Ntimizi alisema marehemu alichukua sifa na tabia za mumewe Dk Joseph Mbatia ambaye aliuona utendaji wake bora alipokuwa Naibu Waziri wa Afya (Ntimizi),

Alisema jambo la msingi ni kuendelea kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, alisema kwa kifupi tu:, " mwenyezi Mungu hakosei".

Matukio ya ajali dhidi ya viongozi wakiwemo wa serikali, kwa mara ya kwanza yalitokea kwa kifo cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Akukweti.

Kifo cha Mbatia ni pigo la pili kwa taifa, lakini tayari kumetokea matukio ya ajali ambazo chuchupu zilete msiba zaidi ambazo ni kwa Profesa Kapuya, Mudhihir na Brigedia Jenerali Mwakanjuki.
 
Hatuwezi sema sana, ila bado siamini kama mwenyezi mungu ni anaweza kupanga ajali kwa viumbe wake, hilo simo. Mkono wa mtu,maneno ya uchungu ya watanzania dhidi ya chama cha kijani,mmmmmmmmhhhhhhhhh, siamini. Mbatia apumzike kwa amani
 
Back
Top Bottom