aftermath of arumeru election

de2sab

New Member
Apr 5, 2012
1
0
SIOI SUMARI ALITOSWA NA VIGOGO WA CCM MKOA, WILAYA, WAFUASI 61 WA CHADEMA WATIWA MBARONI, WADAIWA KUVUNJA KIOO GARI LA KAMANDA WA POLISI

MAMBO mengi zaidi yamezidi kuibuka kuhusu uchaguzi wa Arumeru Mashariki uliomalizika juzi, baada ya taarifa kusema kuwa aliyekuwa mgombea CCM, Sioi Sumari alitelekezwa na viongozi wa chama hicho Wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha wanaodaiwa hakuwa chaguo lao wakati wa kura za maoni.

Wakati Sioi akidaiwa kutelekezwa, shamrashamra za Chadema kusherehekea ushindi wa mgombea wao, Joshua Nassari juzi ziliingia dosari baada ya wafuasi wake 61 kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuvunja kioo cha gari la Mkuu wa Operesheji wa jeshi hilo, Isaya Mngulu.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wajumbe wa timu ya kampeni za Sioi anayetoka wilayani Arumeru alisema mfano dhahiri wa kutengwa kwa mgombea huyo ni siku ya kupigakura ambako hakuna kiongozi yeyote aliyehangaika kuzunguka vituoni kukagua.

Alisema hali ilikuwa mbaya zaidi ilipofika wakati wa kukusanya masanduku ya kura na matokeo kutoka vituoni kabla majumuisho yaliyofanyika katika ofisi ya mji mdogo wa USA-River, ambako hakukuwa na kiongozi yeyote aliyejitokeza kusimamia wala kushuhudia majumuisho hayo.

"Huwezi kuamini kuwa hakukuwa na kiongozi wala mwakilishi yeyote wa CCM kwenye chumba cha majumuisho ya kura hadi ilipofika Saa 7:00 usiku, ndipo mgombea mwenyewe alipoamua kwenda kushuhudia na kusimamia kura zake," alisema mjumbe huyo ambaye ni kiongozi wa ngazi ya mkoa.

Mwandishi wa habari hizi aliyekesha kwenye kituo hicho cha majumuisho alimshuhudia Sioi akifika eneo hilo akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM), Benno Malisa pamoja na makada wengine watatu ambao hata hivyo, waliondoka baada ya dakika 40 na kumwacha mgombea huyo peke yake.

Sioi aliyekuwa akiwania kurithi kiti cha ubunge kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu baba yake, Jeremia Sumari, alibaki ukumbini hapo akiwa ameketi viti vya nyuma hadi alipoondoka ukumbini Saa 10:30 alfajiri, huku mwenzake, Joshua Nassari wa Chadema waliyekuwa wakichuana vikali akiwa ameketi mbele akiwa amezungukwa na kundi kubwa la viongozi wa kitaifa na mawakala wake.

Nje ya ukumbi wa majumuisho, pia walikuwepo viongozi kadhaa wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe waliokuwa wameweka kambi hapo na kukesha hadi matokeo yalipotangazwa kesho yake Saa 12:30 asubuhi.

Mbali ya Mbowe, baadhi ya viongozi wengine wa Chadema walikuwapo ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Mbozi Mashariki, David Silinde na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche.

Licha ya kususwa na kutelekezwa kwenye mchakato wa majumuisho ya kura, inadaiwa kuwa Sioi pia hakupewa fedha za kutosha na chama chake kwa ajili ya kampeni kwani hadi zinamalizika, CCM ilikuwa imetoa milioni 60 pekee tofauti na ilivyofanya kwa wagombea wengine kwenye chaguzi ndogo ambako chama hicho hubeba gharama zote.

"Mpaka usiku wa kuamkia Ijumaa, chama kilikuwa kimetoa milioni 60 pekee kwa kampeni nzima, fedha ambazo hazikutosha hata kulipa mawakala 327 na wale wa akiba ambao kila mmoja tulipanga alipwe Sh30,000. Yaani kama vile chama kilijitenga na kampeni za Sioi," alisema na kulalamika kiongozi mwingine aliyeongoza kampeni za mgombea huyo.

Kiongozi huyo ambaye kama mwenzake alizungumza kwa sharti la kutotajwa akiogopa ‘kushughulikiwa' alisema gharama za kampeni za mgombea huyo wa CCM zilikuwa zaidi Sh200 milioni ambazo zilitokana na michango binafsi za wanafamilia na marafiki.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alipoulizwa kuhusu madai hayo, alikataa kusema lolote akisisitiza kwamba hayo ni mambo ya ndani ya chama yanayostahili kuzungumzwa na kujadiliwa ndani ya vikao.

"Hao waliokuletea taarifa hizo siyo tu kwamba wanakwenda kinyume cha katiba na kanuni za CCM, bali pia wanatoa siri za ndani nje ya chama. Sisi tunatarajia kukutana kufanya tathmini ya uchaguzi huo na yale yanayostahili kuwekwa hadharani tutawaeleza na yanayofaa kufanyiwa kazi ndani ya chama pia tutafanya hivyo kwa maslahi na maendeleo ya chama chetu," alisema Chatanda.

Sioi akubali yaishe
Kwa upande wake, Sioi jana alitangaza kuyakubali matokeo hayo na kuahidi kumpa ushirikiano wa dhati mbunge mteule atakapomhitaji.

Sumari alishindwa kwenye uchaguzi wa ubunge baada ya kupata kura 26,757 ambazo ni sawa na asilimia 44.56 huku Nassari akipata kura 33,972 sawa na asilimia 54.91.

Sioi ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kukipongeza Chadema kwa kuibuka kidedea katika uchaguzi huo huku akikitaka kihakikishe kinatimiza ahadi kilizozitoa kwa wakazi wa jimbo hilo.

Sioi alisema kwamba amekubaliana na matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo,Trasias Kagenzi juzi alfajiri. Alisema ameridhishwa na matokeo hayo na kamwe hatarajii kwenda mahakanani kuyapinga.

Sioi aliwaomba wakazi wa Arumeru Mashariki kumpa ushirikiano wa kutosha mbunge mteule wa jimbo hilo huku akisisitiza ya kwamba hata yeye yuko tayari kufanya hivyo.

Pia alimtaka Nassari kutimiza ahadi zote alizokuwa akizitoa kwa wakazi wa jimbo hio wakati wa kampeni hasa za maji, elimu na miundombinu.

Shamrashamra
Wakati hali ndani ya CCM ikiwa hivyo, vijana 53 wa Chadema walikamatwa na kuachiwa huru baadaye na polisi juzi usiku wakati wakisherehekea ushindi wa Nassari.

Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema vijana hao, wameachiwa kwa dhamana kutokana na maombi ya mbunge huyo mteule kwa polisi.

"Kama ambavyo mbunge aliahidi kuwa asingeweza kuendelea na sherehe za ushindi bila vijana walioshikwa, tunafuraha kuwaeleza kuwa vijana 53 wameachiwa bado vijana saba ndiyo tunawashughulikia," alisema Mrema.

Vijana hao, walikamatwa na polisi katika operesheni kubwa iliyofanyika juzi usiku ikihusisha matumizi ya mabomu baada ya vijana hao kuandamana bila utaratibu na pia kudaiwa kuvunja vioo vya magari.

Polisi limeeleza kuwa vijana hao walikamatwa kwa kosa la kuvunja vioo vya magari likiwemo la Mngulu aliyekuwa mkuu wa operesheni wa polisi katika uchaguzi huo.

Tendwa asifu

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa amesifia ukomavu wa kisiasa uliojitokeza katika chaguzi ndogo za ubunge na udiwani zilizofanyika Aprili Mosi, mwaka huu jlicha ya kujitokeza kwa upungufu mwingi.

"Ukomavu wa kidemokrasia umejitokeza japo mapungufu ni mengi sana yaliyojitokeza pamoja na kuwapo kwa tume ambayo ilijaribu lakini hawakusitisha, sikuweza kuingilia maamuzi yale, kama kutoleana maneno machafu na kejeli ni jambo ambalo linaweza kuleta madhara makubwa, uvumilivu wa kisiasa unahitajika,'' alisema Tendwa.

Alikipongeza CCM kwa kuonyesha ukomavu wake wa kisiasa na Chadema kwa kushinda jimbo hilo na kuvitaka kwa vyama vyote vya siasa nchini kutekeleza kanuni na taratibu zote wakati wa uchaguzi ili kuboresha demokrasia ya nchi.
 
Back
Top Bottom